Utoaji ajira bado mjadala bungeni
Mbunge wa Kibamba (CCM) Issa Mtemvu akiuliza swali kwenye Wizara ya Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, katika kipindi cha maswali na majibu bungeni leo. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Mbunge wa Kibamba (CCM) Issa Mtemvu, leo ameibua tena sakata la utaratibu wa utoaji ajira akitaka usawa kwa maeneo wanayotoka watu.
Dodoma. Mbunge wa Kibamba (CCM) Issa Mtemvu, leo ameibua tena sakata la utaratibu wa utoaji ajira akitaka usawa kwa maeneo wanayotoka watu.
Hata hivyo Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene ameliambia Bunge leo Alhamisi Mei 25, 2023 kuwa, Serikali imeshaunda timu inayofuatilia aina gani ya utoaji ajira itumike.
Wakati wa majadiriano kwenye bajeti ya utumishi, suala la ajira lilichukua nafasi kubwa wabunge wakihoji ajira za upendeleo na kutaka kuwe na mgawanyo kwa wilaya au majimbo.
Katika swali la msingi mbunge huyo ameuliza Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia malalamiko ya ajira za kada ya afya na elimu kutolewa kwa waombaji wanaotoka maeneo machache ya nchi.
Katika swali la nyongeza ambalo liliulizwa pia na Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, wabunge hao wamezungumzia utaratibu unaotolewa kwamba unatakiwa uangalie mgawanyo wa ajira zitolewazo kwa kutazama maeneo wanayotoka.
Simbachawene amesema ajira zinatolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1.2 cha Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la 2 na Kanuni D.6 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 na Kanuni 12 (1) ya Utumishi wa Umma za Mwaka 2022.
Amesema kanuni hizo zinataja kuwa, ajira kwa nafasi zilizo wazi katika utumishi wa umma hujazwa kwa ushindani wa wazi kwa kufanya usaili na kupata washindi katika nafasi husika.
“Naomba niliarifu Bunge lako kuwa, Serikali haitoi ajira kwa kuzingatia maeneo, waombaji wa kazi Serikalini huchukuliwa kuwa na haki sawa na hupimwa na kuchujwa kwa vigezo vinavyofanana bila upendeleo.