Utukutu wa Gaddafi ndani ya Chuo cha kijeshi

Wednesday October 20 2021
Gadaffi pc
By William Shao

Hata baada ya kujiunga na jeshi la nchi hiyo katika Chuo Kikuu cha Jeshi Benghazi, Muammar Gaddafi aliendeleza sifa yake ya uasi. Huko nako alijaribu kuandaa migomo. Aligoma hata kujifunza lugha ya Kiingereza kwa sababu kwake hiyo ilikuwa ni lugha ya wakoloni.

Akiwa chuoni hapo, ndipo msimamo mkali wa Gaddafi ulianza kujulikana zaidi. Ofisa Mwingereza katika chuo hicho, Kanali Ted Lough, baadaye alisimulia habari za Gaddafi akiwa katika chuo hicho na kudai kuwa alikuwa ‘katili asilia’.

Kwa maelezo ya Lough, Gaddafi ndiye aliyehusika na mauaji ya mtoto mwanafunzi mmoja katika chuo cha jeshi cha Benghazi, ambaye alituhumiwa kwa kosa la kufanya ngono chuoni.

Simulizi za historia ya maisha ya Gaddafi zinasema mwanafunzi huyo alikamatwa na Gaddafi na wenzake waliokuwa na msimamo mkali, wakamfunga kamba miguu na mikono, wakamburuza hadi mahali pa kumfyatulia risasi kisha wakaanza kumfyatulia risasi.

Lakini, Gaddafi naye hakuponyoka madhila ya chuoni. Kwa sababu kile kilichodaiwa kuwa ni ujeuri, alikuwa akiadhibiwa mara kwa mara, na wakati mmoja alilazimika kutambaa kwa mikono na magoti kwenye changarawe, huku akiwa amebebeshwa mkoba uliojaa mchanga mgongoni wakati kukiwa na jua kali la utosi. Lakini, adhabu kama hizo zilifanya mawazo yake ya kimapinduzi yaimarike zaidi.

Wakati huu alianza kutofautiana waziwazi na Ufalme wa Libya uliokuwa chini ya Mfalme Idris ambao uliingia madarakani Jumatatu ya Desemba 24, 1951.

Advertisement

Wakati huo nchi hiyo ilikuwa na idadi ya watu takriban milioni moja, ambao wengi wao walikuwa Waarabu, lakini walikuwako pia na Waberberi, Watebu, Wayahudi, Wagiriki, Waturuki na Waitaliano. Serikali hiyo mpya ilikabiliwa na shida kubwa.

Mwaka 1951 Libya ilikuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani. Miundombinu yake mingi ilikuwa imeharibiwa na vita na pia kulikuwa na ukosefu mkubwa wa ajira. Kiwango cha vifo vya watoto wachanga kilikuwa ni asilimia 40 na kiwango cha kutojua kusoma na kuandika kilikuwa ni asilimia 94.

Ni asilimia moja tu ya ardhi ya Libya ambayo ilifaa kwa kilimo na asilimia nyingine tatu hadi nne ikitumika kwa ufugaji.

Mfalme Idris alikuwa Muislamu aliyefuata sana mafundisho ya kidini ikiwamo kutojikweza. Alikataa hata picha yake kuwekwa kwenye sarafu ya Libya na akasisitiza kwamba, hakuna kitu kitakachopewa jina lake isipokuwa Uwanja wa Ndege wa Tripoli Idris.

Utawala wake ulipiga marufuku vyama vya siasa kwa madai kwamba, vilileta fujo nchini mwake. Kuanzia 1952 na kuendelea, wagombea wote wa uchaguzi walikuwa wateule wa Serikali. Pengine kwa kushauriana na Mfalme Idris, mwaka 1954 Waziri Mkuu Mustafa Ben Halim alipendekeza kwamba Mfalme Idris atangazwe rais wa maisha.

Idris alimeleza Ben Halim atoe rasimu rasmi ya mipango hiyo, lakini wazo hilo lilipingwa na upinzani kutoka kwa machifu wa kabila la Cyrenaican.

Chini ya Mfalme Idris, Libya ilijikuta ndani ya ushawishi wa nchi za Magharibi na ilipokea misaada mingi kutoka katika nchi hizo, hususan Marekani.

Kampuni za mafuta ya nchini Marekani zikaanza kuwekeza kwenye sekta ya mafuta ya Libya. Utegemezi wa Libya kwa mataifa ya Magharibi ulianza kuwajenga hisia kali kutoka ulimwengu wa Kiarabu. Hisia za kitaifa za Kiarabu zilichochewa na Redio Cairo na kupokewa na Waarabu wengi. Julai 1967 kulikuwa na maandamano jijini Cairo dhidi ya nchi za Magharibi ambayo yalichochea pia maandamano kama hayo kuzuka mjini Tripoli na Benghazi kupinga Marekani kuiunga mkono Israeli dhidi ya mataifa ya Kiarabu katika Vita vya Siku Sita.

Wafanyakazi wengi wa mafuta kote Libya waligoma kwa mshikamano na vikosi vya Kiarabu vinavyopambana na Israeli.

Pamoja na hayo, Mfalme Idris hakuyumba. Aliruhusu hata kampuni za mafuta za nchi za Magharibi kuchimba mafuta nchini Libya. Aliruhusu hata sheria za nishati hiyo kupitishwa kuwasaidia wawekezaji hao.

Kufikia mwaka 1967 theluthi moja ya mafuta yaliyoingia katika soko la Ulaya Magharibi yalitoka Libya.

Ndani ya miaka michache, Libya iliendelea na kuwa mzalishaji wa nne wa mafuta kwa ukubwa duniani. Kufikia mwaka 1961, sekta ya mafuta ilikuwa na ushawishi mkubwa sana kwenye siasa za Libya kuliko suala lingine lolote. Mwaka 1962 Libya ilijiunga na shirika la nchi zinazouza petroli (OPEC).

Wakati yote hayo yakifanyika, Libya ilikumbwa na ufisadi na upendeleo. Kashfa kadhaa za ufisadi ziliwakumba hata maofisa wakubwa wa Serikali ya Idris.

Juni 1960 Idris alitoa waraka wa umma akilaani ufisadi, akidai kwamba rushwa na upendeleo “vitaharibu uwepo wa Serikali na sifa yake nzuri nyumbani na nje ya nchi”.

Utajiri huu wa mafuta pia ulijenga jamii mpya ya matajiri na kuweka pengo kubwa sana kati ya matajiri na maskini.

Matajiri hawa wapya ambao wengi wao ni wale viongozi wa Serikali ya Mfalme Idris au waliokuwa na uhusiano na viongozi hao, katika macho ya Walibya wengi, walianza kuonekana kama mabepari wa nchi za Magharibi.

Sekta ya mafuta iliyozidi kupanuka iliambatana pia na kuongezeka kwa biashara ya huduma na viwanda. Ajira zilianza kupatikana ghafla katika biashara ya ujenzi na mahoteli.

Kukosekana kwa wafanyakazi wenye ujuzi kulimaanisha kwamba, watu waliojua tu kuzungumza Kiingereza wangeweza kudai mshahara walioutaka. Matokeo ya mabadiliko haya ni kwamba idadi ndogo ya watu ilitajirika kwa haraka.

Wakati Mfalme Idris akijitahidi kuwa kiongozi bora wa kisasa, changamoto yake kubwa zaidi ilikuwa kushughulikia wimbi la utaifa wa Kiarabu ambao uliukumba ulimwengu wa Kiarabu katika ile miaka ya vuguvugu la harakati za miaka ya 1950 na 1960.

Imani ya utaifa ilihubiri kuwa Waarabu wangeweza kupata tena utukufu wao wa zamani ikiwa wataungana na kuwa taifa moja. Vijana wa Libya waliamini kuwa chini ya kinga ya itikadi hii ya utaifa wa Waarabu wangekuwa bora zaidi.

Dhana kama hizo ziliwavutia ili waondoke katika kile walichokiita “mifuko ya mamlaka ya Magharibi”. Serikali mpya ya Kiarabu ya Rais Nasser wa Misri na Abdul Karim Kassem wa Iraq zilionekana kama pumzi nzuri ya hewa safi kwa vijana hao.

Mawazo haya mapya yalienea kwa urahisi nchini Libya kupitia vyombo vya habari, hususan kupitia kituo cha redio cha ‘Sauti ya Waarabu’ ambacho kilitangaza kutoka Cairo na ambacho kilieneza propaganda za utaifa wa Kiarabu bila kuchoka.

Kutokana na upatikanaji wa redio za bei nafuu, vijana wengi wa Libya waliisikiliza sana ‘Sauti ya Waarabu’ ambayo ilikuwa ndiyo pekee iliyowapa habari za kinachoendelea duniani nje ya Libya.

Propaganda hizi za Kiarabu zilisambazwa kupitia mamia ya walimu wa Misri, Wapalestina na Wasudan ambao walikuwa wameletwa kufundisha katika shule na vyuo vikuu vya Libya kwa sababu ya uhaba wa wenyeji waliokuwa na sifa.

Mmoja wa waliokuwa wasikilizaji makini wa redio hii, na ambaye alikuwa akiwahutubia wanafunzi wenzake kinachoendelea kwenye ulimwengu wa Waarabu, ni Muammar Gaddafi.


Aliibukaje kutoka jeshini hadi akawa mwanasiasa? Tukutane kesho.

Advertisement