Utupaji taka ovyo wawaibua viongozi Maswa, watoa onyo

Muktasari:
Jukumu la usafi wa mazingira ni la kila mwananchi, mji safi hujengwa kwa ushirikiano baina ya wananchi na viongozi
Simiyu. Hali ya utupaji taka ovyo imeendelea kuutia doa Mji wa Maswa mkoani Simiyu, hali inayozua taharuki miongoni mwa wakazi wake huku viongozi wa Serikali wakihofia madhara ya kiafya na kuharibika kwa mandhari ya mji huo.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 8, 2025, baadhi ya wakazi wa Maswa wameelezea kukerwa na ongezeko la uchafu kwenye maeneo ya makazi, hasa yale yenye msongamano mkubwa, jambo wanalosema linahatarisha afya za watu hususan watoto.
Slivester Lugembe, mkazi wa Mtaa wa Unyanyembe amesema baadhi ya wananchi wameanza kutumia eneo la makaburi kama sehemu ya kutupia taka, hali inayowaletea usumbufu wakazi wa maeneo jirani.
"Kuna mabaki ya chakula, matunda yaliyooza na taka ngumu zinatupwa hapa. Hali hii inatufanya tupate hewa chafu na inaweka maisha yetu hatarini," amesema Lugembe.
Hata hivyo, amedai kuwa ukosefu wa maeneo rasmi ya kutupia taka katika baadhi ya mitaa umesababisha watu kutumia vichochoro na maeneo ya wazi kama madampo ya muda.
Hata hivyo, wakati Mwananchi inasaka kutaka kujua chanzo hasa cha kadhia hiyo ni kipi hususan kwenye makazi ya watu, Amosi Ntobi, mkazi wa Mtaa wa Stendi Mpya, amesema ni ucheleweshaji wa kusombwa kwa taka hizo.
Amesema kwa sasa taka ngumu zinatupwa hovyo kila mitaa hasa kwenye makazi ya watu kwa sababu magari ya kubeba taka hizo hayapiti kwa wakati.
"Hali hii inatishia afya zetu hasa watoto. Mbu na wadudu wengine wamejaa, watoto wanacheza karibu na malundo ya taka. Hatuwezi kuendelea kufumbia macho hali hii," amesema.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Unice Daud anayeishi Mtaa wa Biafra A, amesema baadhi ya wakazi wanachafua mazingira kwa makusudi.
"Ni aibu mtu mwenye akili timamu kutupa taka barabarani au kwenye mifereji ya maji. Hili ni suala la maadili na uwajibikaji. Kila mmoja wetu anatakiwa kuchukua hatua," amesema Yunice.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa, Caroline Shayo amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa.
Ametaja miongoni mwa mikakati ni kuongeza maeneo rasmi ya kutupia taka na kuimarisha utekelezaji wa sheria ndogo za usafi.
"Tunaanza operesheni maalum kuhakikisha kila mwananchi anazingatia usafi. Tutatoa onyo la mwisho kabla ya kuchukua hatua kali zaidi," amesema Shayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa amesema juhudi za halmashauri zimejikita kwenye elimu kwa umma na uboreshaji wa miundombinu ya usafi, lakini baadhi ya wakazi bado wanakiuka taratibu.
Ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu kulinda mazingira yao kwa kutoa taarifa za wale wanaohusika na uchafuzi wa mazingira.
"Hatutaendelea kuvumilia watu wanaotupa taka hovyo. Hili ni suala la afya ya jamii nzima. Sheria ndogo zinaruhusu kutozwa faini au kufikishwa mahakamani kwa watakaobainika," amesema Mtipa.
Amesisitiza kuwa, jukumu la usafi wa mazingira ni la kila mwananchi na kwamba, mji safi hujengwa kwa ushirikiano baina ya wananchi na viongozi.