Uuzaji bidhaa za viwandani nje umeshuka kwa Sh700 bilioni

Gavana wa Banki Kuu  Prof Benno Ndulu

Muktasari:

  • Februari mwaka huu, Serikali ilikusanya Sh1.4 trilioni zikilinganishwa na Sh1.04 trilioni zilizopatikana Februari 2016. Mapato hayo ni sawa na asilimia 98.9 ya lengo.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikihimiza safari ya kuelekea uchumi wa viwanda, mauzo ya bidhaa za viwandani yameshuka hadi kufikia dola bilioni moja za Kimarekani (sawa na Sh2.3 trilioni), ripoti ya tathmini ya uchumi ya Benki Kuu (BoT) imeeleza.

Mwaka jana mauzo hayo yalifikia dola 1.32 bilioni za Kimarekani (sawa na Sh3.03 trilioni).

Tathmini hiyo iliyotolewa juzi inaeleza kushuka huko kwa mauzo kulichangiwa na kushuka kwa usafirishaji wa bidhaa za chuma na bati pamoja na mafuta ya kula.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa deni la nje limeongezeka mpaka dola 17.56 bilioni (sawa na Sh40.39 trilioni) wakati la ndani likifika Sh10.65 trilioni na kufanya jumla ya Sh51.04 trilioni.

Deni la nje liliongezeka kwa dola 102.2 milioni (235.06 bilioni) kutoka Februari mpaka Machi ilhal la ndani likipanda kwa Sh166.8 bilioni ndani ya muda huo.  Ripoti inaeleza sehemu kubwa ya mikopo iliyochukuliwa ilielekezwa kufidia pengo la bajeti.

 Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Diana Mwiru alisema kutofanya vizuri kwa sekta ya uzalishaji si jambo jema kwa kuwa huathiri sehemu nyingi.

“Viwanda hutumia malighafi za ndani, ajira na kuipa uhai sekta ya usafirishaji. Kutofanya vizuri kwa sekta hii, maana yake watu wengi wanakosa uhakika wa kipato,” alisema Dk Diana.

Dk Diana alisema katika biashara, mkopo huwa na manufaa ukielekezwa katika uzalishaji na kinyume chake ni kujiongezea mzigo.

“Juhudi za Serikali kubana matumizi yasiyo ya lazima na kupunguza mianya ya rushwa inapaswa kuondoa ulazima wa kukopa kwa ajili ya matumizi ya kawaida,” alisema.

Itakumbukwa kuwa hadi Februari, Serikali ilikuwa imetumia asilimia 34 tu ya Sh11.8 trilioni zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na miongoni mwa sababu zilizoelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ni kutokopa kutoka nje kama ilivyopangwa.

Ripoti ya BOT inaonyesha kuwa hali ilikuwa nzuri katika sekta ya madini na utalii ambako mapato yake yaliongezeka. BoT inabainisha thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi kwa mwaka unaoishia Machi 2017 imeongezeka kwa Sh451.5 bilioni.

Ongezeko hilo ambalo ni kutoka dola 8.98 bilioni za Kimarekani zilizopatikana Februari mwaka 2016 mpaka dola 9.17 mwaka huu limechangiwa na kuimarika kwa mauzo ya dhahabu na utalii.

Mapato ya utalii yalipanda kwa asilimia 4.1 na kuliletea Taifa dola 2.13 bilioni (sawa na Sh4.9 trilioni) baada ya idadi ya watalii walioingia nchini kuongezeka.

Ripoti pia inaonyesha kuwa thamani ya usafirishaji wa mazao imepanda hadi dola 896.7 milioni (sawa na ongezeko la asilimia 17.8), ikichangiwa zaidi na mauzo ya korosho yaliyoongezeka kwa kiwango na thamani huku mauzo ya kahawa, katani, chai na karafuu yakishuka.

Ufasirishaji wa mazao yasiyo ya kilimo, hasa dhahabu, uliimarika zaidi na kuliingizia taifa dola 1.47 bilioni (sawa na Sh3.38 trilioni) baada kuongezeka kwa bei na kiwango kilichouzwa nje.