Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uvumilivu, bidii, imani vilivyobadili maisha ya Benedicta

Benedicta Mrema akiwa katika majukumu yake.

Muktasari:

  • Simulizi ya Benedicta Mrema ni ushuhuda kuwa bidii, uvumilivu na imani vinaweza kubadili maisha. Ni hadithi ya binti aliyekataa kukata tamaa licha ya vikwazo vilivyoonekana kuzima kabisa mwanga wa elimu yake.

Dar es Salaam. Katika jamii nyingi za Kitanzania, ndoto za mtoto wa kike mara nyingi hukwama njiani kutokana na changamoto za kiuchumi, mila na mitazamo potofu.

Hata hivyo, simulizi ya Benedicta Mrema ni ushuhuda kuwa bidii, uvumilivu na imani vinaweza kubadili mkondo wa maisha.

Ni hadithi ya binti aliyekataa kukata tamaa licha ya vikwazo vilivyoonekana kuzima kabisa mwanga wa elimu yake.

Mwenyewe anaamini kwamba elimu ni silaha ambayo ukiamua kuibeba kwa umakini, hakuna atakayekuzuia kufika unapotaka kama ilivyokuwa kwake alivyopambana kwa njia mbalimbali kufikia ndoto yake ya kupata elimu.

Benedicta alizaliwa katika familia ya kipato cha chini mkoani Kilimanjaro. Wazazi wake walikuwa ni wakulima na wafugaji wadogo katika kijiji cha Mweka kilichopo Moshi vijijini.

Mapato ya wazazi wake yalitosheleza kupata mlo wa familia iliyokuwa na jumla ya watoto tisa yeye akiwa mtoto wa nne.

Akiwa mdogo, Benedicta alionyesha bidii ya kipekee darasani. Ndoto yake ilikuwa moja tu kusoma hadi chuo kikuu na kuwa mtaalamu atakayesaidia jamii yake, aliguswa zaidi na hali ya umaskini katika kijiji chake.

Kwa kutambua hali ya uchumi wa familia yake, baada ya kumaliza mtihani wa darasa saba akaanza kufikiria kutafuta shughuli ya kufanya ili apate fedha zitakazomuwezesha kujiandaa na elimu ya sekondari.

Hapo ndipo alishauriwa na dada yake aliyekuwa Moshi mjini aende akafanye kazi za ndani katika kipindi cha miezi mitatu anachosubiri matokeo.

Kwa ushauri huo, Benedicta alielekea Moshi mjini ikiwa ni mara yake ya kwanza kabisa kwenda mjini na kuishi mbali na nyumbani akiwa bado mdogo.

Alipata kazi ya ndani nyumbani kwa mwalimu, maisha hayakuwa rahisi. Aliamka alfajiri kuandaa kifungua kinywa, kusafisha nyumba, kufua na kupika. Upweke ulimwandama, lakini hakuruhusu umzime nguvu.

Bahati yake, mwalimu aliyemwajiri alithamini elimu. Alipogundua shauku ya Benedicta ya kusoma, alizidi kumpa hamasa na kumshawishi kuendelea kusimamia mawazo hayo kwa kile alichoamini elimu ni ufunguo wa maisha.

“Nilijua nimeenda pale kufanya nini hivyo sikuruhusu kitu chochote cha kunirudisha nyuma, nilifanya kazi yangu nikijua siku moja nitaondoka na nitaenda shule,”.

Benedicta Mrema akiwa katika majukumu yake.

Hata hivyo matokeo yalivyotoka Benedicta hakuwa miongoni mwa waliofaulu, huo ukawa mtihani mwingine kwake kwani alielewa anakwenda kuiongozea mzigo familia yake kumuwezesha kupata elimu.

Kwa familia isiyo na uwezo wa kumpeleka shule binafsi, ndoto zake zilionekana kufifia.

“Nilihisi dunia imenigeuka, lakini sikutaka ndoto yangu iishie hapo, kila nilipoangalia hali ya familia yangu nikasema lazima nisome, swali likawa nitasomaje bila kuwaingiza wazazi wangu kwenye umaskini zaidi,”anasema.

Ilimlazimu kurudi nyumbani kwao kujipanga upya na kwa bahati alikutana na kasisi wa kanisani ambaye baada ya kumuelezea shauku yake ya kusoma akakubali kubeba gharama za ada.

“Nilienda shule ya kanisa na zile fedha nilizokusanya wakati nafanya kazi nilizitumia kununua vifaa muhimu vilivyohitajika shuleni, hata hivyo mambo hayakuwa rahisi, nikiwa shuleni nilikutana na changamoto kadha wa kadha ambazo kwa namna moja au nyingine zingeweza kunifanya nikatishe masomo.”

Changamoto hizo bado hazikumkatisha tamaa aliendelea na masomo hadi alipohitimu kidato cha nne, hata hivyo hakupata alama zilizomuwezesha kuchaguliwa shule ya Serikali akajikuta anaingia tena kwenye msongo wa mawazo ni kwa namna gani ataendelea na shule.

Ilimlazimu kutafuta njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na dada yake kuomba michango kwa watu aliokuwa anafanya kazi nao, hatimaye akafanikiwa kupata ada ya kulipa katika mojawapo ya shule za sekondari jijini Dar es Salaam.

Hata huko mambo hayakuwa rahisi, bado mzigo wa gharama za elimu ulikuwa mzito kwake wakati mwingine kuwa hatarini kukosa mitihani, kwa msaada wa mkuu wake wa shule alifanikiwa kumlipia kiasi cha ada kilichosalia na hatimaye akafanikiwa kufanya mtihani wa  kidato cha sita.

Baada ya kuhitimu kidato cha sita ilimlazimu kutafuta shughuli ya kufanya, ndipo aliposikia tangazo la kazi ya ulinzi hivyo naye akaenda kujaribu bahati yake.

“Siku ambayo nimepeleka maombi ya kazi kwenye ofisi za ile kampuni ya ulinzi, kulikuwa na tenda mpya ya kwenda kulinda hoteli huko Zanzibar, hivyo ikawa kama bahati kwetu tukaambiwa kesho yake twende tukiwa tumejiandaa kwa ajili ya kwenda kuanza kazi.”

Taarifa ile aliipokea kwa mitazamo miwili, kwanza ilikuwa ni furaha ya kupata kazi lakini pia ilimtengenezea hofu ya kwenda kuanza maisha mapya mahali ambapo hajawahi kufika.

“Nilikuwa na wasiwasi mkubwa sijawahi kufika Zanzibar naendaje kuishi huko sina ndugu wala ninayemfahamu, lakini kila nikikumbuka kwamba nahitaji pesa ili niweze kuendelea na hatua inayofuata kwenye elimu nikapiga moyo konde na kwenda kuanza maisha mapya,” anasema.

Hakufahamu chochote kuhusu ulinzi hivyo alilazimika kujifunza ili kuyaelewa vizuri majukumu yake na hatimaye akabobea kwenye kazi hiyo aliyoifanya kwa jasho na damu.

Alifanya kazi hiyo hadi pale matokeo yalipotoka na kuonesha amepata alama zinazomuwezesha kujiunga na chuo kikuu na wakati ulipofika alianza masomo yake ya elimu ya juu.

“Chuoni nako mambo hayakuwa rahisi, nilipata mkopo lakini kutokana na maisha yetu kiasi unachopata unatakiwa kujibana usaidie pia nyumbani na sikuwa tayari kuona familia yangu inakosa mahitaji muhimu, hivyo bado nikawa naendelea kujibana.”

Kwa sasa Benedicta ni Kaimu Meneja wa Idara ya Habari na Utetezi wa Shirika la Hakielimu akijikita kwenye uhamasishaji elimu ya watoto wa kike.

Anasema maumivu aliyopitia ndiyo yaliyomjenga. Lakini zaidi ya hayo, yalimfungua macho kuona jinsi elimu ya mtoto wa kike ilivyo muhimu na nyeti katika jamii.

Benedicta anasema kila anapokutana na msichana anayekaribia kuacha shule kwa sababu ya umaskini au changamoto za kifamilia, moyo wake huumia.

“Naona kama ninajiona mimi wa zamani. Najua maumivu ya kuona ndoto yako inakatizwa au kukumbana na vikwazo vinavyotaka kurudisha nyuma jitihada za kuifikia.”

Hata hivyo, pamoja na kuguswa kwake na changamoto za wasichana wa pembezoni, Benedicta anakiri kukerwa na wimbi jipya la wasichana ambao, licha ya kuwa na fursa za kusoma, hawataki kujituma.

Anasema anahuzunishwa kuona baadhi yao wakitumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyojenga mustakabali wao.

“Inaniuma sana. Wapo wasichana wana kila kitu ada inalipwa, vitabu vipo, wazazi wanajitahidi lakini hawana nidhamu ya kujisomea. Muda mwingi wanatumia kwenye simu, wakifuatilia maisha ya watu wengine badala ya kujenga maisha yao.”

Benedicta hapingi matumizi ya teknolojia, anasisitiza kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuwa chombo cha kujifunza, kuwasiliana na kupata fursa. Tatizo, anasema ni pale inapotumika vibaya na kuwa uraibu unaopoteza mwelekeo wa maisha.

“Nilisimama usiku kucha nikiwa kazini kwenye lindo ili nipate fedha ambazo zingenisaidia kujiendeleza kielimu. Halafu leo unaona mtu anaacha kusoma kwa sababu tu ameshindwa kuachana na simu kwa saa chache? Hilo linaniumiza,” anasema.

Kwa mujibu wa Benedicta changamoto si umaskini pekee, bali pia mabadiliko ya vipaumbele.

Anawaonya wasichana kuwa sifa za mtandaoni, picha na video haviwezi kuchukua nafasi ya elimu na ujuzi wa kweli.


Ushauri wake kwa wasichana

Benedicta anasema ni muhimu kwa watoto wote kutambua  thamani ya muda. “Hili si la watoto wa kike hata wa kiume wanapaswa kujua muda ukipita haurudi. Dakika unazotumia kwenye mambo yasiyo na tija zinaweza kuwa daraja la kufikia ndoto zako.

“Watumie mitandao ya kijamii kwa manufaa kujifunza, kufuatilia kozi za mtandaoni, kuungana na watu wenye malengo chanya. Wajilinganishe na malengo yao, si maisha ya watu wengine mtandaoni. Kila mtu ana safari yake. Usipoteze muda kuishi kivuli cha mtu mwingine,” anashauri.

Kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, Benedicta anasema ndiyo nyenzo kubwa inayompa msichana sauti, uwezo wa kujitegemea na nguvu ya kubadili jamii.

Hivyo, kuichezea au kuipuuzia ni sawa na kuchezea mustakabali wa kizazi kijacho.