Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO-Kambi ya upinzani yaitaka Serikali kutilia mkazo mjadala wa elimu

Muktasari:

  • Wakizungumza jana katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, wabunge wa kambi hiyo walisema hali ya elimu ni mbaya na Serikali inaandaa kizazi kisichoweza kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeitaka Serikali kutilia mkazo ushauri uliotolewa na marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wa kuwapo kwa mjadala wa kitaifa wa elimu.

Wakizungumza jana katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, wabunge wa kambi hiyo walisema hali ya elimu ni mbaya na Serikali inaandaa kizazi kisichoweza kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema, Taifa limebahatika kuwa na Rais mwalimu.

Alisema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni mwalimu, mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli ni mwalimu.

“Leo Tanzania tupo wapi? Na rasilimali kubwa kuliko zote diniani ni rasilimali watu na rasilimali watu tuliyonayo sasa haijitambui na ili ijitambue lazima iwe na ufahamu,” alisema Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Kama Rais Mkapa anaomba mjadala wa elimu na amekuwa akilirudia mara kwa mara. Rais Kikwete amezungumza haya. Rais Mwinyi amesema nchi inaongozwa kama gari bovu. Mwalimu Nyerere alilisema hadi anaingia kaburini. Tuwe na mjadala mpana wa kitaifa, Tanzania ni yetu sote, watoto hawa wanaumia.”

Mbatia alisema vitabu vinavyosambazwa sasa vya shule za msingi ni vibovu na akamtaka Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ajiulize tatizo lipo wapi, na nani amelisababisha.

Akizungumzia hilo, waziri kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Susan Lyimo alisema, “Hakuna nchi iliyoendelea pasi na kuwekeza katika elimu.”

Katika kusisitiza hilo, Lyimo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) alisema, “Tutaliokoa Taifa na nchi na watoto wetu kama tutakuwa na elimu bora inayokidhi mahitaji ya wakati huu.”

Alisema mjadala huo unapaswa kuratibiwa na wizara ya elimu na si Tamisemi.

“Wizara ya Elimu ndiyo msimamizi wa sera na hata waziri kudai kuna makongamano mbalimbali hayana tija, katika makongamano watu wanajadili na kuondoka, tunataka tume kwelikweli.”

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda alijibu hoja za wabunge kuhusu mjadala wa elimu na kusema Serikali ipo tayari kwa mjadala huo.

Lyimo ambaye kitaaluma ni mwalimu, alisema kuna haja ya Wizara ya Elimu kuwa na tume kama ile ya Jaji Joseph Warioba ambayo itakusanya maoni kwa wananchi na wadau mbalimbali juu ya mfumo wetu wa elimu na kuja na mapendekezo.

Akizungumza katika mkutano huo, waziri kivuli wa Utumishi na Utawala Bora, Ruth Mollel alisema; “Kama elimu haitakuwa nzuri, inakwenda kuathiri moja kwa moja katika utumishi wa umma.

Mollel ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa Utumishi na Utawala Bora katika Serikali ya Awamu ya Nne alisema, “Hao hao ndiyo watakuwa wanaharibu Taifa, kwani hawatakuwa na uelewa, hawawezi kujituma na kujiamiani na madhara yake tutashindwa kushindana katika soko la dunia.”