VIDEO: KKKT yawapa tuzo walioshuhudia muungano wake

Muktasari:

  • Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limewatambua wazee wawili walioshuhudia utiaji saini muungano wa makanisa saba na kuunda KKKT.

Arusha. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limewatambua na kuwapa tuzo maalum wazee wawili, Mchungaji Johansen Rutabingwa (96) na Elirehema Mwanga (86), walioshuhudia muungano wa makanisa saba yaliyounda KKKT.

 Muungano huo ulifanyika Juni 19, 1963 ambao hadi sasa unatimiza miaka 60.

Kutambuliwa kwa wazee hao ni ishara ya kuthamini uasisi wa kanisa hilo na kwa mujibu wa Mkuu wa KKKT, Askofu Frederick Shoo, wazee hao walishuhudia utiwaji saini ya muungano huo.

Hayo yamejiri leo, Jumatatu Agosti 21, 2023 na Askofu Shoo wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya kanisa hilo, yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira mkoani Arusha.

KKKT yawapa tuzo walioshuhudia muungano wake

Katika hafla hiyo pia Askofu Shoo aliwakabidhi tuzo maalumu wazee hao, akisema Mchungaji Mwanga wakati huo alikuwa mwanzilishi wa kanisa la Usambara Digo huku Mutabingwa akiwa mwakilishi wa vijana wakati huo.

"Awali yalikuwa makanisa saba yaliyotajwa kwa maeneo na makabila, ndivyo walivyofanya wamisionari. Wazee baada ya kupata uhuru, roho mtakatifu akawaongoza kwanini msiwe na kanisa moja la Kilutheri, hawa wazee hapa wao walikuwepo walishuhudia kuwekwa saini kwa makubaliano yake Juni 19, 1963.

"Kuna watu hawapendi umoja wa kanisa, hawapendi muungano wanasema sisi ni kanisa moja lakini ni federation ya yale makanisa, mimi nasema huo ni upotoshaji wa makusudi wa historia ya kanisa, sisi ni kanisa moja la KKKT, tunakemea roho ya upotoshaji inayotaka kueneza histori ya uongo," amesema.

Makanisa hayo saba ya Kilutheri yaliyoungana ni la Kilutheri la Iraqw, Kanisa la Kiinjili la Tanganyika ya Kaskazini Magharibi, Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kaskazini, Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kati, Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kusini, Kanisa la Kilutheri la Uzaramo-Uluguru na Kanisa la Kilutheri la Usambara-Digo.