VIDEO: Makonda atoa maelekezo ya CCM kwa Majaliwa

Makonda atoa maelekezo ya CCM kwa Majaliwa

Dodoma. Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda, amesema chama kimempa miezi sita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhakikisha anasimamia, kuratibu, kuondoa na kufuta migogoro ya ardhi inayosababisha wananchi wateseke.

Makonda alitoa kauli hiyo jana jijini hapa katika mapokezi aliyoandaliwa na CCM Mkoa wa Dodoma.

Katika mkutano huo, Makonda hakueleza ni kikao gani, kilichofanyika wapi na lini kilitoa maagizo hayo kwa Majaliwa.

akizungumzia kuhusu kauli ya Makonda, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda aliliambia Mwananchi, kuwa miongoni mwa majukumu ya CCM ni kuisimamia Serikali iliyoiweka madarakani hivyo agizo hilo ni halali.

Katika mkutano wake wa jana, Makonda alisema CCM inamtaka Waziri Mkuu kushughulikia migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara na ile ya muda mrefu.

Alisema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ina migogoro inayotokana na mipaka, Wizara ya Maliasili na Utalii ina migogoro inayohusiana na hifadhi wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayo migogoro ya ardhi.

“Chama kinamtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awe amesimamia na kuratibu kuondoa na kufuta migogoro yote ya ardhi inayosababisha wavuvi, wakulima, wafugaji na wananchi kuteseka chini ya ardhi yao,”alisema.

Alisema anajua kuna baadhi ya watu wanamuangalia na kuhoji kwa umri huo anawezaje kutoa maagizo ya aina hiyo kwa kiongozi mkubwa.

“Aliyeagiza sio mimi ni CCM, kuendelea kwa migogoro hii kunawapa wapinzani sifa wasizostahili.” alisema

Makonda alisema anafahamu iliundwa timu ya mawaziri ikazunguka nchi nzima na kuna maeneo ambayo Rais, Samia Suluhu Hassan alisharidhia wananchi warejeshewe ardhi.

“Migogoro hii ndani ya miezi sita chini ya sekretari ya CCM na Katibu Mkuu wetu Daniel Chongolo, tunasubiri ripoti ya Kassim Majaliwa jinsi alivyoshughulikia pamoja na mawaziri wake. Sijapewa jukumu la kupamba watu, nitasema kero za wananchi na wala sio sifa isiyostahili,”alisema Makonda.

Alisema dhuluma ya ardhi imewafanya baadhi ya watu kutamani kujiua na wengine wanajilaumu kwa nini walizaliwa hapa Dodoma.

“Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa nakupenda na nakuheshimu lakini hapa nilipo sio heshima yangu, si matakwa yangu tena, chama kinakupa miezi miwili hadi Desemba (mwaka huu) tusisikie mwananchi wa Dodoma analia juu ya ardhi,” alisema.

Alisema itakapofika Januari Mosi, mwakani watu waende kula Sikukuu ya mwaka mpya bila migogoro tena ya ardhi.

Akizungumzia kero ya maji jijini Dodoma, Makonda alisema CCM inawataka wote waliopewa dhamana ya kushughulika na changamoto hiyo kuhakikisha wanafanya kazi kikamilifu kwa sababu maji ni kipaumbele cha jiji.

Alisema CCM inazitaka pia kamati zote za siasa za mikoa kuhakikisha zinawasemea watu wenye migogoro ya ardhi ili changamoto hiyo imalizwe na wale wanaokwamisha wachukuliwe hatua.

Makonda pia aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya ambao majukumu yao ni mtambuka kwa wizara zote, kuhakikisha Ilani ya uchaguzi ya CCM inatekelezwa bila mkwamo.

“Chama kinataka mtu akija kulalamika kwako wewe mtumishi wa umma umpeleke katika ofisi husika ama kuandika barua ya kumwelekeza anapotakiwa kwenda. Akitokea mtu alienda kwenye ofisi fulani kwa jambo ambalo wewe unaweza kulitekeleza lakini halikupata majibu, chama kitashughulika na wewe,” alisema.

Awali akizungumza katika mapokezi hayo, Mwenyekiti wa CCM Mkoani Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa alimtoa hofu Makonda na kumtaka kuendelea na mwendo huo huo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumza kauli hiyo, Dk Mbunda alisema utatuzi wa migogoro ya ardhi ni suala lililopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.

Alisema ingekuwa wakati wa awamu ya pili wakati Rais alikuwa Ali Hassan Mwinyi na Mwenyekiti wa chama alikuwa Mwalimu Julius Nyerere, maagizo hayo angepewa hata Rais.

“Lakini kwa sababu Rais ndiye huyo huyo mwenyekiti wa chama, huwezi kumpa maagizo mwenyekiti wa chama unatakiwa kumpa mtu mwenye cheo cha kiutendaji. Hiyo ni sahihi kabisa kwa sababu moja ya majukumu ya chama ni kuisimamia Serikali iweze kutekeleza zile ahadi ilizotoa kwa wananchi wakati wa uchaguzi,” alisema.