Vifo ajali Mbeya vyafikia 19, majeruhi wawili kati 10 hali tete

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Urlich Matei akizungumza jioni hii ofisini kwake kuelezea ongezeko la idadi ya vifo katika ajali iliyotokea mapema leo mkoani humo.

What you need to know:

  • Katika ajali hiyo iliyotokea saa 3 asubuhi ya leo Juamnne watu nane waliopoteza maisha papohapo, ambapo hadi sasa vifo vimeongezeka kufikia 19.

Mbeya. Idadi ya vifo katika ajali iliyotokea leo Jumanne, Agosti 16, 2022 imeongezeka kutoka nane hadi 19 huku ikielezwa majeruhi wengine wawili kati ya 10 hali yao ikiwa mbaya.

Asubuhi ya leo Jumanne, ilitokea ajali iliyohusisha lori lililokuwa limebeba mchanga kwa kufeli breki na kugonga magari matatu katika maeneo ya Shamwengo kata ya Inyala mkoani hapa ambapo watu nane waliopoteza maisha papohapo.

Akizungumza jioni hii Kamanda wa Jeshi mkoani humo, Urlich Matei amesema hadi kufikia muda huu vifo vimefikia 19 huku wengine wawili kati ya 10 majeruhi wakiwa katika hali mbaya.

Amesema waliopoteza maisha ni wanaume 12, wanawake sita na mtoto mmoja huku akieleza kuwa chanzo ni uzembe wa dereva wa lori hilo, Muhsin Gumbo aliyeshindwa kumudu gari hilo.

"Hadi kufikia muda huu vifo vimefikia 19 huku majeruhi wakiendelea kupata huduma katika hospital ya rufaa, chanzo kikubwa ni kufeli kwa breki za lile Lori lakini uzembe wa dereva wa gari hilo, Gumbo mkazi niwasihi madereva kuwa makini," amesema Matei.

Kamanda huyo amesema miili minne ya marehemu imelazwa hospital ya Inyala, mitano Rufaa na 10 ipo Igawilo na kwamba bado hawajatambua kila mmoja kujua kama kuna wa familia moja.