Vijana 37 waliokuwa wakijitolea utendaji wa mitaa Iringa waandamana

Baadhi ya vijana 37 ambao walikuwa wakijitolea utendaji wa mitaa Manispaa ya Iringa wakiwa na mabango ya kumshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Raisi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete baada ya kurejeshwa kazini.

Muktasari:

Siku moja baada ya vijana 37 waliokuwa wanajitolea kufanya kazi za utendaji kwenye mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Iringa kupata ajira, wamefanya maandamano kutoa shukrani zao kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.

Iringa. Vijana 37 waliokuwa wanajitolea kufanya kazi za utendaji katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Iringa, wameandamana kutoa shukrani zao kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete baada ya kuwarejesha kazini.

Kulingana na Ridhiwani, wasifu wa vijana hao ambao baadhi yao wamejitolea kwa miaka tisa unaonyesha wana sifa ya kufanya kazi waliyokuwa wakiifanya.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa (CCM), Ritha Kabati ndiye aliyekuwa wa kwanza kuibua sakata la vijana hao kuondolewa, baada ya kuonekana walishindwa katika usaili.

Vijana hao wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakijitolea kufanya kazi za utendaji kwenye mitaa, lakini baada ya ajira mpya kutangazwa waliomba na kukosa kwa madai ya kukosa sifa.

Wakizungumza katika Ofisi za CCM, Iringa Vijijini leo Alhamisi, Novemba 23, 2023 vijana hao wamesema walikata tamaa baada ya kuondolewa mpaka pale walipopewa fursa ya kurudi kazini.

"Nilianza kujitolea Kata ya Nduli na baadaye nilileta tena maombi ya kuendelea kujitolea, nimahamishiwa Mtaa Mfalanyaki Kata ya Kihesa ni miaka mitau sasa," amesema Furaha Mtonyole, mmoja wa vijana hao.

Ameshukuru kwa kupata nafasi ya kurejea kazini akiingia kwenye ajira mpya baada ya agizo la naibu waziri huyo.

Kijana mwingine ambaye amekuwa akijitolea, Catherine Masangula amesema nafasi waliyopewa wataitendea haki.

"Asante kutuona sisi vijana wanyonge, nimejitolea miaka tisa na nimefanya kazi mitaa yote ya Kata ya Makorongoni. Ajira zilipotangazwa niliomba, nikaitwa kwenye usaili na nikawa nimefeli. Niliumia sana, lakini leo wanyonge tumetetewa," amesema Masangula.

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Iringa Constantine Kihwele amesema vijana hao walikuwa na haki ya kuendelea na kazi kama ambavyo walionekana wanafaa kujitolea na kikaimu nafasi za utendaji wa mitaa.

"Kuna wakati mambo huwa yanafanyika visivyo na tunaambiwa ni maelekezo ya juu, tunashukuru sana kwa hatua hii naibu waziri, lipo jambo la kujifunza," amesema Kihwele.

Ridhiwani amesema vijana wengi wamekuwa wakijitolea kufanya kazi, lakini linapofika suala la ajira huwa wanaonekana hawafai.

"Yapo maelekezo ya sera ya kutoa kipaumbele kwa vijana wanaojitolea, lakini kama hawa wamefanya vizuri kwa miaka yote, imekuwaje kwenye ajira waonekane hawafai?" amehoji Ridhiwani na kuongeza;

“Kati ya vijana 47 wa kujitolea, 37 walionekana wamefeli baada ya usaili. Nyie watu muogopeni Mungu. Asiyefaa hana sababu za kumkaimisha, wote waliofanya usaili wana sifa.

“Mmepewa nafasi ya kuwafanyia usaili hamjawapa ajira. Naagiza vijana wote waliofanyiwa usaili Iringa warudishwe kazini,” amesema.

Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amesema tayari maagizo hayo yanafanyiwa kazi.

Jana Jumatano, Ridhiwani aliagiza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuwapatia ajira vijana hao 37 kati ya 47 waliokuwa wamekaimu utendaji wa mitaa na kuonekana hawana sifa baada ya kufanyiwa usaili wapatiwe ajira.

Alisema baada ya ofisi yake kuitisha na kukagua wasifu wa vijana hao, wote wana sifa za kuajiriwa tofauti na kilichofanyika kuwaweka pembeni, licha ya kujitolea kwenye nafasi hizo.

Ridhiwani alisema hayo wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.

“Kati ya vijana 47 wa kujitolea, 37 walionekana wamefeli baada ya usaili. Nyie watu muogopeni Mungu. Asiye faa hana sababu za kumkaimisha, wote waliofanya usaili wanazo sifa,” alisema na kuongeza;

“Mmepewa nafasi ya kuwafanyia usaili hamjawapa ajira. Naagiza vijana wote waliofanyiwa usaili Iringa warudishwe kazini.”