Viongozi wilaya ya Mwanga wapewa siku saba kujisalimisha
Muktasari:
Serikali imetoa wiki moja kwa viongozi wa Wilaya ya Mwanga kujisalimisha kwa madai kuwa wanashirikiana na wavuvi haramu kuhujumu bwawa la nyumba ya Mungu lililopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mwanga. Serikali imetoa wiki moja kwa viongozi wa Wilaya ya Mwanga kujisalimisha kwa madai kuwa wanashirikiana na wavuvi haramu kuhujumu bwawa la nyumba ya Mungu lililopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Amesema watakaokaidi agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza leo Alhamisi Desemba 24, 2020 naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amesema viongozi hao wamekuwa wakikwamisha kazi ya kuwakamata wavuvi haramu katika bwawa hilo.
Naibu waziri huyo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lang'atabora kilichopo jirani na bwawa la nyumba ya Mungu wilayani humo.
"Zipo taarifa za baadhi ya viongozi wa ngazi ya wilaya hii kushirikiana wavuvi haramu, wote wanaojijua wamefanya hivyo nawapa wiki moja wajisalimishe.”
"Wote wanaojihusisha na uvuvi haramu ni maadui zetu, ikumbukwe hili ni kama shamba la wakazi wa eneo hili lakini kuna watu wanaliharibu makusudi licha ya kuwa kuna viongozi tuliowaweka hapa na tunawaamini. Viongozi wote wanaoshirikiana na mtandao wa wavuvi haramu tunawajua na majina yao tunayo, wasipo acha tutawashughulikia,” amesema Gekul.
Amesema, “naomba viongozi hawa wajisalimishe mara moja na ninawapa wiki moja watubu dhambi zao na warudi kwenye mstari, wasiporudi hatutawaonea huruma kwa sababu ndio wanaotuangusha na kutukwamisha katika kutekeleza majukumu yetu ya kuhakikisha bwawa linakuwa salama.”