Vita ya vigogo CCM hapatoshi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inakutana jana kuchuja majina ya wagombea wa nafasi za uongozi mkoa, ambao baadhi yao watakuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.

Dodoma/mikoani. Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imekutana jana kuchuja majina ya wagombea wa nafasi za uongozi mkoa, ambao baadhi yao watakuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.

Miongoni mwa watakaopitia mchujo huo wa leo ni Waziri wa Nishati, January Makamba, waliowahi kuwa mawaziri Alhaji Haji Mponda, Dk Mary Nagu, Balozi Philip Marmo, Sophia Simba na Dk Anthony Diallo.

Waliowahi kuwa wakuu wa mikoa; Mecky Sadick, Henry Shekifu, Loata Sanare, waliowahi kuwa wakuu wa wilaya; Lembrice Kivuyo, Christopher Kangoye. Wengine ni wabunge Tarimba Abbas na Josephat Gwajima na mbunge wa zamani, James Lembeli na aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Adam Kimbisa.

Jana, ilikutana CC na leo ni NEC ambapo mchujo huo ni mwendelezo wa uchaguzi ndani ya CCM ulioanza mwanzoni mwa mwaka huu na sasa umefikia ngazi ya mkoa baada ya kumalizika uchaguzi wa wilaya uliofanyika mwezi uliopita.

Wagombea watakaochujwa leo yamo majina ya waliowahi kushika nafasi za uongozi serikalini na ndani ya CCM kwa wengine kuwa wajumbe wa CC na NEC, wabunge, naibu Spika na mawaziri.


Uchaguzi wa mwaka huu

Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika uchaguzi wa mwaka huu zaidi ya wana-CCM milioni mbili walijitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.

Idadi hii ya wagombea kwa mujibu wa Shaka haijawahi kutokea katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika kwenye chama hicho.


Waliojitokeza

Miongoni mwa majina hayo wengine walitemwa na vikao vya CCM walipoomba kugombea ubunge wala kuwemo kwenye nafasi za uteuzi wa ngazi mbalimbali za uongozi.

Baadhi ya majina ambayo yataingia kwenye mchujo wa leo ni Adam Kimbisa, aliyewahi kuwa mjumbe wa NEC na CC, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na ameomba kugombea uenyekiti wa CCM mkoa.

Majina mengine ni Dk Mary Nagu, aliyewahi kuwa mbunge na nafasi kadhaa za uwaziri, ikiwamo Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto na Waziri wa Katiba na Sheria anagombea ujumbe wa NEC.

Pia, Balozi Philip Marmo aliyewahi kuwa mbunge, Naibu Spika, nafasi kadhaa za uwaziri na baadaye aliteuliwa kuwa balozi anagombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara.

Vigogo wengine waliojitokeza ni Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Dk Anthony Diallo aliyewahi kuwa mbunge, mjumbe wa NEC na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, anatetea nafasi yake ya uenyekiti wa mkoa.

Mwingine ni aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa katika mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro, Mecky Sadick anayewania nafasi ya mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza.

Vigogo wengine walioamua kurejea ulingoni ni Henry Shekifu anayetetea nafasi yake ya mwenyekiti wa Mkoa wa Tanga. Aliishawahi kuwa mbunge na mkuu wa mkoa katika mikoa ya Mtwara na Manyara na mwingine ni Abdurahman Abdallah.

Pia, kwenye nafasi hiyo ya wenyekiti wa Mkoa wa Tanga yumo mfanyabiashara Mohamed Said anayetetea nafasi yake ya NEC.


Dodoma

Waliojitokeza nafasi ya uenyekiti Mkoa wa Dodoma ni Adam Kimbisa anayerudi kwenye nafasi hiyo akipambana na mwenyekiti wa sasa, Godwin Mkanwa na Felister Bura aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu.

Wanaogombea ujumbe wa NEC ni Robert Muwinje aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma na Ismail Jama anayetetea nafasi yake.


Tanga

Nafasi ya mwenyekiti Mkoa inagombewa na Henry Shekifu anayetetea nafasi yake na Abdurahman Abdallah aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Pangani.

NEC wanaogombea ni Mohamed Said anayetetea nafasi yake, Omari Mwesingo aliwahi kuwa MNEC Wilaya ya Mkinga na Najim Msenga aliyewahi kuwa MNEC Wilaya ya Lushoto.


Manyara

Mwenyekiti wa sasa wa Mkoa, Simon Lulu anatetea nafasi yake akipambana kwenye nafasi hiyo na Balozi Philip Marmo na Peter Toima.

Nafasi ya katibu wa itikadi na uenezi ni Mosses Komba, Iddi Sulle na Johannes Darabe. NEC waliochukua ni Joachim Muungano, Dk Mary Nagu na Lenganasa Soipey.


Arusha

Aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare na aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembrice Kivuyo ni miongoni mwa makada 17 wa chama hicho wanaowania nafasi ya mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, akiwamo Zelothe Steven anayetetea nafasi yake.


Shinyanga

Wanaogombea uenyekiti wa CCM mkoa wako 15, wakiwamo Donald Magesa, mbunge wa zamani wa Kahama, James Lembeli na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Hamisi Mgeja.


Mwanza

Wanaogombea nafasi ya uenyekiti wa Mkoa wa Mwanza ni mwenyekiti wa sasa, Dk Anthony Diallo, Mecky Sadick na Simon Mayunga Mangelepa ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi Mkoa wa Mwanza anayemaliza muda wake.


Mara

Wanaogombea nafasi ya mwenyekiti mkoa ni Samuel Kiboye anayetetea nafasi yake na wanachama wengine 24 ambao ni Flora Mundeba, Ziara Munasa na Rose Nyamsogora.

Wengine ni aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Magori Alphonce, mkuu wa wilaya wa zamani, Christopher Kangoye na Patrick Chandi.

Wengine wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ni Cosmas Regu, Mirumbe Joshua, Kagina Zongori, Maulid Shaaban, Icon Nestory, Leonard Kitwara, Abednego Range, Emmanuel Mang’arawe na Samwel Alfred, John Kasereka, Dk Malima Bundala, Ephraim Opundo, Silvanus Msore, Emmanuel Mtaki, John Marande, Kyabwene Misana na Marwa Kebohi.


Dar es Salaam

Wanaogombea nafasi ya NEC ni aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, January Makamba ambaye ni mbunge wa Bumbuli na Waziri wa Nishati.

Pia, yumo Iddi Azzan ambaye ni mbunge wa zamani wa Kinondoni, mbunge wa sasa wa Kinondoni, Tarimba Abbas na Josephat Gwajima ambaye ni mbunge wa Kawe.


Katavi

Wagombea wa NEC ni Girlbet Sampa anayetetea nafasi yake, Buhula Chasama, Raphael Peleleza na Teonas Kibabila.

Morogoro

Miongoni mwa wanaogombea nafasi ya uenyekiti mkoa ni aliyewahi kuwa mbunge wa Malinyi na pia Waziri wa Afya, Alhaji Haji Mponda.


Mkutano Mkuu na NEC

Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM na NEC ni vikao vya juu vya CCM vyenye maamuzi makubwa hasa kwa wanaowania nafasi za uongozi serikalini kama vile Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Spika na ubunge.

Viongozi watakaokwenda kuchaguliwa kwenye mikoa wengi wao watakuwa wajumbe wa NEC na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa. Na ndio watakaokuwa na uamuzi kwa wanaofaa kupeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi za uongozi serikalini.

Wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) inajumuisha wenyeviti wote wa mikoa na makatibu wao, wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC), ndani ya CC kuna wanaoingia kwa nafasi zao kama vile Spika wa Bunge, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Makamu wa Rais).

Wajumbe wengine wa NEC ni wajumbe wote sekretarieti ya Taifa, wenyeviti na makatibu wa jumuiya (Umoja wa Vijana wa CCM-UVCCM, Wazazi na Umoja wa Wanawake-UWT), wajumbe wa kapu (15 bara na 15 visiwani), wabunge watano na wawakilishi watano.

Wajumbe hao wa NEC pia ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa wakiungana na wajumbe wengine ambao ni wenyeviti, makatibu wenezi na makatibu wa mikoa, wenyeviti na makatibu wa jumuiya zote wa mikoa, wabunge wote, wawakilishi wote, wajumbe wa kuchaguliwa kutoka wilayani (kila wilaya wajumbe watatu), wenyeviti, makatibu na makatibu wenezi wa wilaya.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni, uchaguzi ngazi ya wilaya na mkoa ni muhimu katika upatikanaji wa wajumbe watakaoweka vizuri mustakabali wa chama katika chaguzi za Serikali ngazi ya Taifa.


Kuondolewa makatibu NEC

Wakati wa mchujo wa wagombea urais ndani ya CCM, wajumbe wa NEC kwenye mkutano wa Septemba, 2015 uliofanyika ukumbi wa ‘White House’ Makao Makuu ya CCM, wajumbe walimpokea mwenyekiti wa CCM (wakati huo Jakaya Kikwete) kwa wimbo wa ‘tuna imani na Lowassa.’

Lowassa ndiye aliyeonekana kuwa kinara miongoni mwa makada 38 walioomba kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akionekana kuwa na wafuasi wengi ndani na nje ya chama.

Kuanzia hapo, CCM baadaye ilibadili katiba yake na kuwaondoa makatibu wa mikoa na wilaya kuwa wajumbe wa NEC, ikielezwa kwamba wao ni waajiriwa na walipaswa kuonyesha utii kwa mwajiri wao na si kujiingiza kwenye siasa za makundi.

Hata hivyo, mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni yaliwarejesha makatibu hao kuwa wajumbe wa NEC na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM baada kuonekana wenyeviti hawakuwa wanafikisha maelekezo ya chama yaliyokuwa yanatolewa kwenye NEC kwa ukamilifu na wengine walikuwa hawafikishi kabisa.

Pia, CCM ililazimika kuwafukuza uanachama baadhi ya wanachama wake na wengine kuwaonya baada ya kubainika kujiingiza kwenye makundi ya wagombea urais.

CCM ilimfukuza uanachama kada wake mkongwe aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Sophia Simba.

Pia, ilitoa msamaha kwa Adam Kimbisa na kumpa onyo kali Emmanuel Nchimbi na alifungiwa kugombea nafasi yoyote kwa kipindi cha miaka minne.

Pia, mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa wakati huo, Ramadhani Madabida alifukuzwa uanachama.

Wenyeviti waliofukuzwa uanachama ni Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara) huku mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke akipewa onyo kali.

Wengine waliovuliwa uanachama ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Madenge, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Assa Simba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, Mwenyekiti Mkoa wa Shinyanga Ernest Kwirasa, Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Nesta Msabatavunga, Mjumbe wa Halamshauri Kuu (NEC) ya CCM, Ali Sumaye, Mjumbe wa NEC Arumeru, Mathias Manga.

Wengine zaidi ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Longido Leiza alifukuzwa uanachama pamoja na Mwenyekiti wa CCM Arusha Mjini, Saileli Molleli, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Gairo, Omary Hawadhi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Muleba, Mwenyekiti wa CCM Babati, Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bunda, Mjumbe wa NEC Gureta.