Vyama vipya vya siasa 18 vyaomba usajili, sita vyapata
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imepokea maombi ya wanasiasa wanaohitaji usajili wa muda wa vyama 18 vipya vya siasa.
Endapo vyama hivyo vitakidhi masharti ya usajili wa muda na ule wa kudumu, Tanzania itafikisha idadi ya vyama vya siasa 39.
Kwa mujibu wa tovuti ya ofisi hiyo, hadi kufikia jana kulikuwa na idadi ya vyama vyenye usajili wa kudumu 20 kabla ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Fransis Mutungi jana kueleza ameshapokea maombi mengine ya kuanzisha vyama 18.
“Tulikuwa na maombi 17, lakini juzi tumepata ombi jingine la chama kimoja, lakini hadi sasa ni vyama sita tu katika maombi hayo ndivyo vimekidhi masharti ya kupata usajili wa muda, sio kila ombi litakidhi,” alisema Jaji Mutungi, alipokuwa katika mahojiano maalumu na Mwananchi hili ofisini kwake jana.
Jaji Mutungi alisema baada ya kukidhi sifa kwa baadhi ya vyama hivyo, vitaingizwa katika mpango wa bajeti kwa ajili ya uhakiki wa wanachama.
Msingi wa kauli hiyo ulitokana na swali aliloulizwa kuhusu hatima ya usajili wa Chama cha Umoja Party kinacholalamikia ofisi hiyo kunyimwa usajili wa muda, licha ya kufanyia marekebisho ya usajili wa muda.
Chama hicho kiliomba usajili wa muda Aprili mwaka 2021 na kutimiza vigezo vyote vya kikanuni huku kikirekebisha madai ya mapingamizi manne; mawili kutoka chama cha CUF na Kampuni ya ANORIS kuhusu kufanana nembo ya mikono huku CCM ikiwasilisha madai ya kufananisha rangi za bendera.
Bila kutaja majina ya vyama hivyo Jaji Mutungi alisema: “Tuna vigezo vya kufikia kabla ya kupata usajili wa muda, kabla ya kutangaza chama husika, kuna mapingamizi, kuna chama kinataka usajili lakini kina bendera inayofanana na chama kingine, mwingine atakuja na jina linafanana na chama fulani,” alisema.
“Kwa hiyo tunapofikia hatua ya kutangaza lazima tujihakikishie mambo mengi, baada ya hapo tunatoa usajili wa muda na vinapewa siku 180 kutafuta wanachama kabla ya kufanyia uhakiki, baada ya hapo unaweza kukuta ni vyama viwili tu, kati ya hivyo ndio vimetimiza masharti, ndio tunatangaza.”
Alisema baadhi ya vyama vinajenga maswali katika uanzishaji wake kutokana na presha inayojitokeza. “Ndio maana tumekuwa makini sana, tunafanya kazi ya uchunguzi maeneo mengi hadi uhamiaji, ukiona tumekupa usajili ujue tumepita maeneo mengi. Sheria haijanipa ukomo wa usajili.”
Alipoulizwa kuhusu msingi wa ongezeko hilo la vyama katika Taifa maskini, Jaji Mtungi alisema: “Unajua siri ya vyama ni ngumu sana, kuna wengine wamechoka chama walichopo, wanatoka na kuanzisha kingine. Wengine wanaona vyama vilivyopo hatuvitaki, wanaanzisha chama chao fresh”.
Alifafanua kuhusu mazingira ya utitiri wa vyama hivyo na tija ya Taifa: “Nakuelewa, unamaanisha watu wanataka vyama imara vya siasa lakini inategemeana na aina ya watu tulionao ndani ya nchi. Tuna political activism tu (siasa za kiharakati), vyama vinaanzishwa kwa sababu tofauti.”
Akitoa maoni yake kuhusu usajili wa vyama hivyo, Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alitoa tahadhari akisema ongezeko hilo linaweza kuzalisha vyama vya ukanda, udini na ukabila.
“Nashauri tuongeze masharti angalau chama kipate asilimia tano ya kura zote katika uchaguzi, chini ya hapo kisitambuliwe kisheria ila kiungane na chama kingine.”
Kuhusu Katiba
Kuhusu mchakato wa maboresho ya Katiba, Jaji Mutungi alisema mchakato huo haujakabidhiwa ofisi ya msajili.
“Ila hii ni fursa, itasaidia kuyakutanisha makundi yote pamoja. Wanasiasa wasije wakabweteka wakifikiri kwamba Rais Samia ametoa rungu kwa wanasiasa kusimamia mchakato huo, wamepotea,” alisema.
“Naomba hilo wazo walifute, pindi rais alipoagiza utekelezaji wake uanze mara moja alikuwa na maana kuna mchakato wa maandalizi. Baraza la vyama vya siasa linatakiwa kupenyeza hoja kupitia mkutano ambao utaandaliwa kwa kuzingatia taratibu zake kukutanisha wadau,” alisema Jaji Mutungi.
Pia alikiri kuwepo mkwamo katika mchakato wa Katiba ulihusisha kundi moja la wanasiasa, akisema anatamani mchakato huo kwa sasa utafanikiwa kupitia ushirikishaji wa makundi yote ya kijamii.
“Hadidu za rejea zitakazozingatiwa kwenye mkutano zitatengenezwa na utaratibu mwingine lakini siyo Ofisi ya Msajili vyama vya siasa. Mkutano upo kwenye maandalizi ya kuitishwa, utahusisha wote na utafikia hatua utahusisha wataalam kutathimini mawazo yaliyowasilishwa na wadau,” alisema.