Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waandamana wakidai kudhulumiwa ardhi Dodoma

Wakazi wa Mtaa wa Muhuji Jijini Dodoma wakiwa wamesimamisha shughuli katika ofisi za Jiji la Dodoma wakitaka wasikilizwe.

Muktasari:

  • Leo saa 5 asubuhi wakazi hao waliandamana hadi nyumbani kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mlimwa C jijini hapa wakitaka wasikilizwe juu ya kile wanachodai jiji kuwadhulumu maeneo yao ikiwa ni pamoja na kubomolewa nyumba zao.

Dodoma. Zaidi ya wakazi 200 wa Mtaa wa Muhuji Kata ya Kizota jijini Dodoma, wamesimamisha shughuli za katika ofisi za Jiji la Dodoma kwa takriban saa moja, huku wakitaka wasikilizwe madai yao ya kubomolewa nyumba zao.

Mapema leo Julai 5, 2023 saa tano asubuhi, wakazi hao waliandamana hadi katika makazi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mlimwa C jijini hapa wakitaka wasikilizwe kero yao ya kudhulumiwa maeneo yao na kubomolewa nyumba zao na Jiji.

Wakiwa jirani na makazi hayo ya Waziri Mkuu walielekezwa na ofisa mmoja waende ofisi za Jiji la Dodoma kwani tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Godwin Gondwe wamepigiwa simu ili wawasikilize.

Majira ya saa 6 mchana wakazi hao ambao walifika eneo hilo wakiwa wamekodi ‘Coaster’ na baadhi wakiwa na bodaboda walianza safari ya kuelekea ofisi za Jiji la Dodoma.

Walifika katika ofisi hizo saa 6:30 mchana na kuanza kuimba nje ya ofisi hizo wakitaka wasikilizwe.

“Tuna imani na Mama Samia, oyaaaa oyaaa oyaaa, Samia kweli kweli….” Walisikika wakiimba wimbo wenye maneno hayo nje ya ofisi za Jiji la Dodoma.

Ilipofika saa 6:45 mchana huku shughuli zikiwa bado zimesimama, alitoka Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe ili kuwasikiliza, huku akiwataka kutafuta eneo lingine la kuzungumzia kutokana shughuli katika eneo hilo kusimama.

"Ndugu zangu hii ni ofisi kuna kazi zinaendelea, naomba mtafute eneo tofauti ili kazi zingine ziendelee naomba mwende kwenye ukumbi wa jiji, atakuja Mkuu wa Wilaya kuwasikiliza," amesema Meya huyo, lakini wakazi hao  waligoma kuondoka wakitaka Mkuu wa Mkoa na Wilaya wafike katika ofisi hizo hizo ili  kuwasikiliza.

Ilipofika saa 7:30 mchana wakazi hao walikubali kuacha shughuli ziendelee huku wakiendelea kusubiria Mkuu wa Mkoa nje ya ofisi za jengo hilo.

Akieleza sababu ya maandamano hayo kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufuatiliaji ya Makazi katika Mtaa wa Muhiji, Shaban Simba amesema jiji la Dodoma limebomoa nyumba 47 katika mtaa huo, huku likiwaacha wakazi wa maeneo hayo wakiwa wanaishi kwenye nyumba za jirani, ndugu jamaa na marafiki.

Amesema jambo linalowaumiza wenye fedha wameanza kujenga katika maeneo yao na kwamba kila wanapohoji hawapewi majibu sahihi wakati baadhi ya familia zikiendelea kuteseka.

Kwa mujibu wa Simba, Mkuu wa Wilaya aliwahi kufika eneo hilo na kutoa maelekezo ya kusitisha ujenzi hata hivyo wanashangaa kuwa licha ya marufuku hiyo, leo wameshuhudia ujenzi ukiendelea.

“Wanajenga wakiwa na askari, sasa sisi nani atatusikiliza, wenye fedha wanatushinda tukaamua tuende kwa Waziri Mkuu. Hatuendi popote tunasubiria hapa hapa, shughuli zitaendelea ila hapa hatuondoki," amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema tangu Jumatatu wanazunguka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya wakiomba wakisikilizwe lakini wamekuwa wakipigwa danadana.