Waandishi wa habari watakiwa kuchangamkia fursa
Muktasari:
- Waandishi wa habari wanaoandika habari za jamii za pembezoni wametakiwa kuchangamkia fursa ya ruzuku itakayotolewa kwao ili kuibua changamoto zinazowakabili jamii hizo.
Arusha. Waandishi wa habari wanaoandika habari za jamii za pembezoni wametakiwa kuchangamkia fursa ya ruzuku itakayotolewa kwao ili kuibua changamoto zinazowakabili jamii hizo.
Mratibu wa miradi wa nchi za mashariki ya mbali, Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika wa shirika la Journalist for Human Rights (JHR), Siyabulela Mandela ameyasema hayo jijini Arusha Septemba 4 kwenye mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na chama cha waandishi wa habari za jamii za pembezoni (MAIPAC).
Mandela amesema waandishi hao wanaoandika habari za jamii ya pembezoni watawezeshwa ruzuku ya kuandika kea undani habari za jamii hizo za pembezoni.
Amesema waandishi hao wanapaswa kuandika juu ya athari za jamii kwa upande wa haki za binadamu, wanawake na watoto na Uviko 19.
Mmoja kati ya waandishi wa waliopatiwa mafunzo hayo, Baraka Ole Maika amesema jamii za pembezoni ikiwemo Wamasai na Wadatoga wanakabikiwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kwenye maeneo wanayoishi.
"Tunaishukuru MAIPAC kwa kutuandalia mafunzo haya ya siku tatu ambayo kwa namna moja au nyingine yatakuwa chachu ya kutujengea uwezo zaidi wa taaluma yetu," amesema Ole Maika.
Mwandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd wa Mkoa wa Kilimanjaro, Janeth Joseph amesema kupitia mafunzo hayo akejengewa uwezo zaidi wa kuandika habari za jamii ya pembezoni.
Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma amesema waandishi hao wanapaswa kujituma kuandika habari za jamii hizo ili mafanikio ya masomo hayo yaonekane.