Waandishi watumia msiba kumpa ujumbe Nape

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akisaini kitabu cha maombolezo muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza inapofanyika shughuli ya kuaga miili ya waandishi watano waliofariki jana wakiwa kwenye ziara ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Waandishi wa habari wametumia msiba wa wenzao watano waliofariki katika ajali ya gari kuiomba Serikali kuboresha sheria na mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari.

Mwanza. Waandishi wa habari wametumia msiba wa wenzao watano waliofariki katika ajali ya gari kuiomba Serikali kuboresha sheria na mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari.


Maombi hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti na wawakilishi wa tasnia ya habari waliotoa salamu za rambirambi wakati wa hafla ya kutoa heshima za mwisho kwa waandishi watano na dereva wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa waliofariki dunia katika ajali jana Januari 11 zinazoendelea uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.


Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko ndiye alikuwa wa kwanza kuiomba Serikali kuboresha sheria na mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari kwa kuiombq wizara yenye dhamana kurekebisha kasoro zilizopo.


"Nitumie fursa hii kumwomba Waziri Nape Nnauye ambaye ndiye muasisi wa Sheria ya Huduna ya Habari ya mwaka 2016 kuwezesha waandishi wa habari kufanya kazi katika mazingira bora," amesema Soko.

Majeneza yaliyobeba miili ya waandishi wa habari watano waliofariki katika ajali wakiwa kwenye ziara ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel yakiwa yamewasili katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kwa ajili ya shughuli ya kuagwa na ndugu, jamaa na marafiki. Picha na Mgongo Kaitira


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ni miongoni mwa waombolezaji walioko uwanja wa Nyamagana akiwa ndiye mgeni rasmi katika tukio la kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.


Akizungumzia sharti la kiwango cha elimu, kiongozi huyo wa wanahabari aliomba waandishi wanaojiendeleza kielimu waruhusiwe kuendelea kutekeleza majukumu yao.


Mkurugenzi mtendaji wa Klaubu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan ndiye aliyepigilia msumari wa moto kuhusu sheria na mazingira ya kazi kwa wanahabari akisema wengi wa waandishi wa habari nchini wakiwemo baadhi ya marehemu wanaoagwa hawajalipwa mishahara na stahiki zao kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.
"Ninapozungumza sasa, hapa mbele yangu wapo waandishi wa habari waliolala ambao leo tunawaaga hawajalipwa mishahara yao kwa miaka miwili. Kama yupo aliyelipwa, basi amelipwa miezo minane iliyopita," amesema Karsan na kuibua miguno na makofi kutoka kwa waombolezaji.

Waombolezi wakiangua vilio baada ya kuwasili katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza inapofanyika shughuli ya kuaga miili ya waandishi wa habari watano waliopoteza maisha kwenye ziara ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza Picha zote na Mgongo Kaitira


Ametaja madhaifu yaliyopo kwenye sheria na udimamizi mdogo wa mamlaka husika kuwa miongoni mwa sababu zinazoyoa mwanya kwa waajiri kutotimiza wajibu wa malipo sahihi na stahiki kwa watumishi wa vyonbo vya habari.


"Waajiri hawalipi mishahara kwa madai ya kukosa fedha; lakini tunakutana nao baa. Fedha ya kwenda baa zinapatikana isipokuwa ya kuwalipa mishahara waandishi," amesema ba kuhoji Karsan huku akipigiwa makofi na waomboleza ambao pia walisikika wakinong'onezana