Wabunge wa upinzani kupeleka sakata la Sh1.5 tril kwa wananchi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akiomba mwongozo bungeni wakati wabunge wakichangia mjadala wa taarifa  za utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali na Hesabu za Serikali za Mitaa katika Kipindi cha Januari 2018 hadi Januari 2019. Picha na Anthony Siame

Dodoma. Baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuisafisha Serikali kuhusu sakata la Sh1.5trilioni ikisema “hakuna upotevu wala wizi wa fedha hizo” wabunge wa upinzani wamesema sasa wanalipeleka suala hilo kwa wananchi.

Wakati wabunge hao wakieleza nia yao hiyo, Spika Job Ndugai amelieleza Mwananchi kuwa, “Taarifa sahihi ni ya mwenyekiti wa kamati (ya PAC), hao wengine lazima wapige siasa waonyeshe kuna wezi na nini hata kama hakuna kilichoibiwa. Hizo ni siasa za kawaida, wapinzani watapinga.”

Amesema, “Taarifa ya kamati na hao wanaosema maneno ya uongo ni wana kamati pia. Kamati imekaa mwaka mzima na hao watu, ikumbukwe kuwa wenyeviti wa kamati hizo mbili (LAAC na PAC) ni wapinzani pia, hivyo hawawezi kuandika taarifa feki.”

Mwishoni mwa wiki iliyopita, taarifa ya PAC ya 2018 iliyosomwa bungeni na mwenyekiti wake, Naghenjwa Kaboyoka ilisema hakuna upotevu wala wizi wa fedha hizo.

Alisema katika kuchambua ripoti ya ukaguzi huo maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kamati ilibaini suala la tofauti ya Sh1.5 trilioni ya mapato ya Serikali na makusanyo kwa mwaka wa fedha 2016/17 halikuwapo baada ya marekebisho ya hesabu kufanyika.

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo baadhi ya wabune wa kambi ya upinzani walisema hawakubaliani na majibu hayo, hivyo suala hilo watalipeka kwa wananchi majimboni kwao. “Pale tunachohoji ni nani aliruhusu fedha hizo zikaenda kutumika bila idhini ya Bunge, kwa nini zitumike kinyume na maagizo ya Bunge na ni fedha nyingi, sasa mjadala ndiyo kwanza umeanza lazima moto uwake na ukweli ujulikane,” alisema Hamidu Bobali, mbunge wa Mchinga (CUF) akizungumzia uamuzi wao wa kupeleka suala hilo kwa wapigakura wao.

Utata wa matumizi ya fedha hizo uliibuliwa na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe wakati akichambua ripoti ya CAG ya 2016/17.

Tangu suala hilo lilipoibuliwa Aprili mwaka jana kumekuwapo na mijadala mara kadhaa ndani na nje ya Bunge, hasa kutoka kwa wapinzani uliokuwa ukitaka maelezo ya kuwapo kwa tofauti ya uwiano wa mapato na matumizi ya kiasi hicho cha fedha ambacho Zitto alidai hazionekani.

Wakati mjadala huo ukiwa moto, Aprili 20, 2018 Rais John Magufuli akiwaapisha majaji wapya Ikulu jijini Dar es Salaam alilizungumzia suala hilo akisema hakuna fedha iliyoliwa na kama ingekuwa hivyo, watendaji waliohusika wangechukuliwa hatua.

Hata hivyo, Kaboyoka wakati akihitimisha hoja yake mwishoni mwa wiki bungeni, alisema pamoja na taarifa hiyo, lakini kulikuwa na mambo mengi ya ajabu ambayo kamati haikuyaingiza kwenye taarifa yao na akaomba CAG apewe nafasi ya kufanya ukaguzi maalumu katika baadhi ya maeneo ambayo hakuyataja.

Katika maelezo yake, Bobali alisema kelele walizozipiga sasa wanazihamishia kwa wananchi na lazima watawasha moto hadi ukweli ujulikane.

Alisema hakuna ubishi kuwa fedha hizo hazikupotea, bali zilitumiwa isivyo na kwamba, ni lazima wajue zilitumika kwa matumizi gani na kwa ruhusa ya nani.

Bobali alishauri Hazina kufumuliwa kwa madai kuwa ndiko kinapoanzia kichaka cha dharau na matumizi ya hovyo.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema hata kabla ya kwenda kwa wananchi, bado watabanana bungeni kwa kuwa wameshapata ukweli wa kiasi zaidi ya kile walichokuwa wanaelezwa.

Mdee ambaye ni Waziri kivuli wa Fedha na Uchumi, alisema wabunge wa chama tawala hawataweza kuuzima ukweli wa jambo hilo.

Alitaja kiasi cha fedha zenye utata kuwa ni zaidi ya Sh1.5 trilioni ambazo wameshazibaini na sasa wanafanya uchunguzi zaidi kubaini kama kuna upotevu mkubwa zaidi ya huo.

Katika mchango wake bungeni, mbunge wa viti maalumu (Chadema), Catherine Ruge alitaja Sh1.5 trilioni na kuongeza kuwa kuna kiasi kingine cha Sh900 bilioni, lakini kauli hiyo baadaye ilipingwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akaagiza mchango huo ufutwe kwenye kumbukumbu za Bunge.

Alipokuwa akichangia hoja hiyo iliyofutwa na Naibu Spika, Ruge alisema, “Baada ya hoja ya Sh1.5 trilioni kufungwa, zimeibuka hoja nyingine na sasa hatuzungumzii 1.5 trilioni tunazungumzia 2.4 trilioni.”

“Mheshimiwa Naibu Spika naomba niweke rekodi clear (sawa), sio kazi ya CAG kusema kama kuna wizi, kazi ya CAG ni kufanya ukaguzi na kutambua mapungufu yaliyopo na mamlaka zinazohusika ku-take charge (kuwajibisha).”

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Rhoda Kunchela alisema uchunguzi wa CAG ulibaini ukweli na hakuna shaka yoyote, lakini kinacholeta shida ni kuwa upotevu huo unahusika na maeneo aliyoyataja kuwa ya wakubwa. “Kuanzia sasa tunajikita kuwapa taarifa sahihi wananchi na kuendelea kujipanga ndani ya Bunge ili kuziba mianya ya upotoshaji ingawa wingi wa wabunge wa CCM ni kikwazo kwetu,” alisema.