Wachungaji KKKT wampinga Dk Shoo

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dk Fredrick Shoo

Muktasari:

  • Siku chache baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dk. Fredrick Shoo kuagiza kiti cha Askofu Dk Edward Mwaikali kurejeshwa Dayosisi ya Konde Tukuyu, wachungaji wa majimbo matano kati ya saba wamepinga maagizo hayo.


Mbeya. Siku chache baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dk Fredrick Shoo kuagiza kiti cha Askofu Dk Edward Mwaikali kurejeshwa Dayosisi ya Konde Tukuyu, wachungaji wa majimbo matano kati ya saba wamepinga maagizo hayo.

Novemba 16, Dk Shoo alifanya ziara mkoani hapa kufuatia mgogoro wa kanisa hilo baada ya waumini kumtuhumu Askofu Dk Mwaikali kuhamishia mali za kanisa na kuzipeleka makao makuu ya Konde jijini Mbeya.

Katika kikao kilichofanyika Tukuyu, kikiwahusisha viongozi wa Serikali, akiwamo Kamanda wa Polisi Mkoa, Urlich Matei na Msajili wa jumuiya za dini kilicholenga kumaliza mgogoro huo, Dk Shoo aliagiza hadi kufikia Novemba 22 kiti cha Askofu kirejeshwe Dayosisi ya Tukuyu, ambapo wachungaji wameweka ngumu wakidai hawakufurahishwa na vitendo vya kiongozi huyo.

Wakizungumza jana jijini hapa kwenye kikao kilichohusisha wachungaji 67 kutoka majimbo matano kati ya saba, walisema hawakubaliani na uamuzi ya Dk Shoo kwa kuwa amelifedhehesha kanisa na viongozi wao.

Nyibuko Mwambola, mchungaji wa jimbo la Mbeya Mashariki alisema hawakubaliani na ubabe, uonevu na unyanyasaji aliofanyiwa Askofu Mwaikali.

Alisema hawakutarajia vyombo vya dola vitumike kuwalazimisha viongozi wa Dayosisi kufika kituo cha Polisi ili kukutana nao kwa mazungumzo badala ya kutumika kwa ofisi ya Dayosisi.

Agosti 22, 2021 waumini wa kanisa la KKKT Dayosisi ya Konde Tukuyu walifanya vurugu wakipinga Askofu Mwaikali kuhamisha mali za kanisa hilo kuzipeleka makao makuu ya Ruanda Mbeya hadi Jeshi la Polisi lilipoingilia kati.