Wadau: Nishati mbadala suluhu changamoto ya umeme nchini

Baadhi ya wadau wakifuatilia kongamano la mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia lililofanyika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Wakati Tanzania ikijielekeza kwenye matumizi ya nishati jadidifu katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kupikia, wadau wamependekeza nishati hizo zitumike pia kama chanzo mbadala cha umeme.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijielekeza kwenye matumizi ya nishati jadidifu katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kupikia, wadau wamependekeza nishati hizo zitumike pia kama chanzo mbadala cha umeme.

Wamesema kufanya hivyo, kutatoa jawabu la kudumu la changamoto ya umeme inayojitokeza mara kwa mara, hasa kipindi cha ukame kutokana na maji kusalia kuwa chanzo kikuu cha kuzalisha nishati hiyo.

Pendekezo hilo la wadau linakuja, kipindi ambacho Tanzania imeelekeza juhudi zake kuendana na ulimwengu kwa kuacha matumizi ya nishati zilizozoeleka kupikia, yaani kuni na mkaa, badala yake kuhamia katika nishati safi.

Novemba mosi na 2, mwaka huu Wizara ya Nishati ilifanya mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia ulioibuka na msimamo wa kuundwa kikundi kazi kitakachokuja na mkakati wa miaka 10 wa kulitekeleza hilo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wadau hao wanasema uwepo wa vyanzo vingi vya nishati ya umeme utasaidia upatikanaji wa huduma hiyo kwa uhakika na nafuu.

Kulingana na wadau hao, chanzo kinachotumika sasa, yaani maji kama msingi wa uzalishaji umeme kunalifanya Taifa liendelee kuwa na umeme usio wa uhakika, hasa nyakati za ukame.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Climate Action Network Tanzania, Dk Sixbert Mwanga anasema tafiti nyingi zinaonyesha Tanzania ina kiwango kikubwa cha nishati safi inayotosheleza mahitaji ya wananchi wake.

Anasema nishati jadidifu ni chanzo kingine muhimu kitakachowezesha uzalishaji umeme bora kwa bei rahisi na kutosheleza mahitaji ya nchi.

“Nishati mbadala zilizopo ukifuatilia zinatosha na uzuri wa hizi hazihitaji kufuatwa na gridi ya Taifa, badala yake zenyewe ndiyo zinaifuata gridi ili ziende kufidia wengine wenye upungufu.”

Kulingana na Dk Mwanga, hatua ya kutumia umeme wa gridi kwa ajili ya kuusambaza katika maeneo mbalimbali nchini, inaigharimu Serikali fedha nyingi za kuunganisha mifumo mbalimbali, zikiwemo nyaya.

“Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kwanza tu kwa kupanua ule mtandao ambazo zingetumika kuwekeza kwenye uzalishaji, kulingana na chanzo cha eneo husika na baada ya kutosheleza ndiyo tukaanza kutafuta namna ya kuhakikisha tunaingiza nishati iliyozidi kwenye gridi ya Taifa ili kuona kama kwenye msongo mkubwa inaweza kusaidia wengine au la,” anasema.

Anakazia hoja yake hiyo kwa kutolea mfano wa kilichotokea mkoani Kigoma, kwamba katika uhalisia gridi ya Taifa ndiyo iliyoufuata mkoa huo na gharama kuwa zimetumika kulifanikisha suala hilo.

Anasema hali ingekuwa kinyume chake, iwapo vingetumika vyanzo vya nishati mbadala vilivyopo mkoani humo kuzalisha umeme wake na kuanza kuusambaza kwa wakazi wa eneo husika, kisha ziada ndiyo iingizwe kwenye gridi ya Taifa kwa ajili ya matumizi ya wengine.

“Kigoma ina mito mikubwa kama Malagalasi, ina jua na mambo mengine, umeme ungezalishwa kupitia vyanzo hivyo kwa ajili ya matumizi ya wananchi, badala ya kusubiri gridi ya Taifa ndiyo waunganishwe nao,” anasema.

Anapendekeza kila mkoa uzalishe umeme kulingana na vyanzo ulivyonavyo. “Tukifanya hivi tunaleta kitu kinaitwa demokrasia ya nishati, lakini mambo ya kusubiri gridi ya Taifa kwanza yanahatarisha kupotea kwa umeme kwa kuwa hatuna nguvu ya kulidhibiti hilo,” anasema.

Dk Mwanga anataja hatua nyingine ni Serikali itoe ruhusa kwa watu binafsi watakaozalisha umeme zaidi ya mahitaji yao, kuuza kwa wengine au kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

“Changamoto tuliyonayo ni kwamba ukizalisha umeme wako nyumbani ukatosheleza mahitaji, ziada inayobaki huna uwezo wa kuingiza kwenye gridi ya Taifa, hilo suala limebaki kuwa mjadala,” anasema.

Anataka kuwepo utaratibu utakaowawezesha watakaozalisha umeme nyumbani kwao waruhusiwe kuuza ziada kwa watu wengine au Serikali.

“Tunaweza kuongeza umeme kwa kasi, wapo watu wengi wanashindwa kuendesha hicho kitu kwa sababu wamepata hasara baada ya Tanesco kushindwa kuchukua umeme uliobaki,” anasema.

Suala la kodi na tozo katika vifaa vya kuzalishia umeme wa nishati mbadala, analitaja kuwa kikwazo kingine kinacholikwamisha Taifa kupata uhakika wa nishati hiyo.

“Kwenye betri na vifaa vingine vya kuhifadhia umeme huo kodi yake ni kubwa na Serikali haiingizi ruzuku, badala yake inaingiza kwa upande wa Tanesco ili gridi iendelee kutanuka.

Katika kufanikisha matumizi ya umeme wa nishati mbadala, anasema Serikali inapaswa kuangalia eneo la ushuru, hasa wa vifaa vya kuzalisha umeme.

Hoja ya matumizi ya vyanzo mbadala kuzalisha umeme, inaungwa mkono na Mtaalamu wa Misitu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Profesa Romanus Ishengoma, anayesema ni vigumu kuwa na nishati ya umeme ya uhakika iwapo mamlaka hazitatazama vyanzo vingi.

“Tunaweza kuwa na nishati stahimilivu, umeme wetu mwingi unatokana na maji, yakipungua kwenye mabwawa uzalishaji pia unapungua, tuangalie vyanzo vingi,” anasema.

Nishati ya gesi ni chanzo kingine kilichotajwa na Profesa Ishengoma kuwa jawabu la changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme.

“Umeme usiuangalie kwa mabwawa makubwa na vitu vikubwa, kuna vyanzo vidogo vinaweza kutumika kama mito midogo, hii inaweza kuzalisha umeme, lakini nishati jadidifu ni eneo lingine tunalopaswa kuligeukia,” anasema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mtendaji Mkuu wa Safi Power, Fred Mallya anayesema changamoto ya umeme haipo Tanzania pekee, isipokuwa mataifa mengine yameamua kuwekeza kuitokomeza.

“Kikubwa ni chanzo cha umeme wenyewe, tulitumia mafuta kwa miaka mingi, baada ya kuona yana athari za mazingira tukaacha ndiyo tumekuja na maji,” anasema.

Pamoja na matumizi ya maji, anasema ni muhimu kuvigeukia vyanzo vingine vitakavyowezesha upatikanaji wa nishati ya uhakika.

Anavitaja baadhi ya vyanzo hivyo ni jua, akifafanua kuwa kwa Tanzania nishati hiyo hupatikana kwa wingi, lakini bado haijaanza kutumika vema kuzalisha umeme.

Anasema upepo ni chanzo kingine muhimu kinachopaswa kutumika kuzalisha nishati hiyo kwa kuwa katika baadhi ya maeneo unapatikana kwa wingi.

Anasisitiza matumizi ya vyanzo vingi vya nishati hiyo huongeza nguvu, chanzo kikuu kinapozidiwa kwa sababu mbalimbali.

“Zile sehemu ambazo gridi haifiki tuhakikishe tunafunga nishati mbadala wananchi wapate umeme,” anasema.

Anapendekeza sekta binafsi iruhusiwe kuingilia soko la uuzaji na usambazaji umeme wa nishati yoyote, ili kupunguzia mzigo gridi ya Taifa.

“Kama sekta binafsi itaruhusiwa kufanya biashara hii, maana yake mahitaji yatapungua kwenye gridi, hivyo Tanesco haitazidiwa,” anasema.

Wakati Mallya anasema hayo, tayari Serikali imeanza kubaini na kutumia vyanzo mbalimbali vya nishati kupata umeme wa uhakika.

Miongoni mwa juhudi zinazofanywa ni pamoja na uendelezaji wa nishati ya joto ardhi kama sehemu ya kuongeza vyanzo vya umeme nchini.