Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wa haki jinai watakiwa kusaidia vita makosa ya wanyamapori

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Jaji Amour Khamis,akizunguzma na wadau wa haki jinai leo jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na  Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori duniani (WWF), Oktoba 13, 2022 inaonesha katika kipindi cha mwaka 1970 hadi 2018, idadi ya wanyamapori duniani imepungua kwa asilimia 69.

Arusha. Wadau wa Haki jinai nchini wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu, waendesha mashitaka na wapelelezi waandamizi, wametakiwa kuboresha utendaji kazi wao ikiwemo kusimamia misingi ya maadili ya kazi zao ili kusaidia vita dhidi ya makosa ya wanyamapori.

Aidha wametakiwa kuwa na viwango stahiki vya utoaji huduma, ambapo kwa kufanya hivyo mbali na kutekeleza majukumu yao kikazi watakuwa wamelinda na kutetea maslahi ya kiuchumi na kuimarisha ulinzi, usalama, amani na utulivu wa taifa.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Oktoba 15, 2022 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Jaji Amour Khamis wakati akifunga mafunzo ya namna bora ya ushughulikiaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ikiwemo ujangili na mazao ya misitu kwa wadau hao.

Jaji huyo amesema maadili ni nyenzo muhimu katika utoaji huduma bora kwani ni suala mtambuka linalogusa kila hatua ya utendaji wa mnyororo wa haki jinai likiwagusa wao.

Amesema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 13,2022 na Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori duniani (WWF), inaonyesha idadi ya wanyamapori duniani imepungua kwa asilimia 69  katika kipindi cha mwaka 1970 hadi 2018 ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Taarifa hiyo inaonesha kuwa idadi ya wanyamapori imepungua na waliopo wamedhoofika kwa ubora kutokana na kuharibiwa kwa mifumo asilia ya ardhi na bahari, uvunaji uliopitiliza wa wanyama na mazao ya misitu na mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema Jaji Khamis.

Amesema kwa hapa nchini taarifa ya Taasisi ya Utafiti waa Wanyamapori (Tawiri), inaonyesha kati ya mwaka 2009-2014, idadi ya tembo pekee ilipungua kutoka 109,051 mpaka kufikia 43,521 sawa na asilimia 60.

Jaji Khamis amesema kuwa kupungua kwa wanyamapori nchini kulichagizwa na udhaifu wa usimamizi wa mipaka, sheria dhaifu za kusimamia wanyamapori, adhabu ndogo zilizokuwa zinatolewa kwa makosa ya wanyamapori, udhaifu wa vyombo vya kusimamia sheria za wanyamapori na uwepo wa rushwa.

Amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa uhifadhi wa wanyamapori na misitu ya asili vipo hatarini na hivyo inahitajika mipango na hatua madhubuti za kukabiliana na hali hiyo na kuwa vita dhidi ya makosa ya wanyamapori ni ya jamii yote.

"Ni muhimu kwetu kuendelea kushirikiana kama wadau katika harakati za mapambano dhidi ya makosa hayo, wote tufanye kazi zetu ipasavyo na kusimamia misingi ya Katiba, Sheria na taratibu na hivyo kutoa maamuzi ya haki bila kumuonea mtu yeyote,” amefafanua.

Awali Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Joachim Tiganga amesema mafunzo hayo yametolewa kwa wakati muafaka ambapo suala la uhifadhi ni moja ya vipaumbele vya taifa na yatasaidia kuongeza ufanisi kwa kiasi kikubwa kwao kuanzia namna bora ya uendeshaji na upelelezi wa mashauri hayo.

“Mnaona namna ambavyo serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye utalii na hakuna uhifadhi hakuna utalii,sisi kama wadau tumeweza kukaa pamoja kuwa na uelewa wa pamoja,” amesema.

Naye Mkuu wa mashitaka Mkoa wa Mara, Valence Mayenga amesema mafunzo hayo yamekuwa nyenzo muhimu kwao hasa katika kulinda rasilimali za taifa, hifadhi na wanyamapori na kuwa wamekumbushana juu ya mbinu bora za upelelezi, uendeshaji wa mashauri na uandishi wa hukumu kwa Majaji na Mahakimu ambao wanatoa uamuzi.