Wadau wanolewa kupambana ufisadi

Arusha. Wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali na binafsi kutoka Tanzania bara na visiwani  wamejengewa uwezo wa kitaalamu jinsi ya kuzuia, kuripoti  na kudhibiti  ufisadi pamoja na ubadhirifu na kuweza kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa wahusika.

Hayo  yamesemwa  leo Machi 6 jijini hapa na Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Chama cha wataalamu wa kupambana na ubadhirifu na ufisadi (ACFE) Tanzania, Pauline Mtunda wakati akizungumza katika mafunzo hayo.
Mtunda amesema kuwa lengo  la mafunzo hayo ni kuweza kupata uelewa na ufahamu zaidi kuhusu masuala ya ufisadi unaotokea  mahala pa kazi na namna ya kuweza kudhibiti na kuchukuliwa kwa hatua mbalimbali za kisheria.

"Tunaangalia fedha za umma zinapelekwa wapi kwani asilimia  70 ya fedha za umma zinatumika kwenye manunuzi na ndipo  fedha nyingi huwa zinaibiwa  na tunachofanya  sisi ni kuhakikisha pasiwepo na wizi katika sekta mbalimbali ili fedha ziweze kutumika kihalali kwa faida ya jamii na nchi yetu kwa ujumla," amesema .

Kwa upande wake Meneja wa operesheni kutoka chama cha wataalamu wa kupambana na ubadhirifu na ufisadi Tanzania (ACFE TANZANIA), Abduel Kelakela amesema kuwa chama hicho makao yake makuu yapo nchini Marekani ambapo lengo kubwa ni kuhakikisha kama nchi wanapiga  hatua katika kupambana na matukio  ya ubadhirifu na ufisadi na  hatimaye kuweza kuokoa fedha za nchi.

Amesema wamekuwa wakitoa mafunzo hayo mara tatu kwa mwaka ambapo yameleta manufaa makubwa sana kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi lengo likiwa ni  kudhibiti   na kuzuia ubadhirifu usitokee.


"Ripoti ya dunia inayotolewa na chama hicho Marekani inasema kuwa asilimia 5 ya mapato ya kila taasisi hupotea kila  mwaka kwa ajili ya ubadhirifu ufisadi na rushwa hivyo elimu zaidi inatakiwa kutolewa  ili kuziba  na kudhibiti  mianya hiyo  kwa kiwango kikubwa ili isitokee tena,"amesema Kelakela.

Aidha amesema kuwa, taasisi nyingi zimekuwa na wahasibu , wataalamu na maafisa utumishi ambao  wanakuwa na uwezo  wa kudhibiti  kwa kiwango kidogo tofauti na kuwepo kwa wataalamu waliobobea katika maswala hayo ambao  wana uwezo wa kudhibiti kwa asilimia 50, hivyo ni vizuri kuwepo  na wataalamu wabobezi katika taasisi mbalimbali .


Kwa upande wa  baadhi  ya washiriki wa mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali-Zanzibar, Dk Mwanahamis Adam amesema mafunzo yanasaidia sana kupata mbinu mpya za kuweza kupambana na maswala ya ufisadi kwani asilimia kubwa ya wanapiga fedha hizo wamekuwa wakitumia  mbinu  mbalimbali hivyo kupitia  mafunzo hayo wataweza kuokoa  fedha ambazo  zimekuwa zikiibiwa  kwa njia mbalimbali.

Naye Meneja wa miamala ya kadi kutoka benki ya NMB makao makuu, CPA Said Sungura amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa kampuni yake kwani wanaweza kupata uelewa zaidi wa mbinu  zinazotumika na mafisadi katika kuiba fedha na namna ya kuweza kuzifuatilia na kuweza kujiridhisha namna wizi huo ulivyotumika.