Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wataka uvunaji maji ya mvua uundiwe mkakati  

Muktasari:

  • Bodi hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali na kupunguza athari za upungufu wa maji unaojitokeza mara kwa mara wakati wa misimu ya ukame.

Moshi. Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani imezishauri halmashauri zote za Kanda ya Kaskazini kuingiza katika sheria ndogo za utoaji wa vibali vya ujenzi sharti la kuwepo kwa miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 11, 2026 katika kikao cha wadau wa mamlaka za maji, viwanda na wamiliki wa mashamba makubwa, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani, Segule Segule, amesema utekelezaji wa sharti hilo utasaidia kupunguza athari za upungufu wa maji.

Amesema upungufu huo wa maji hujitokeza mara kwa mara wakati wa misimu ya ukame, hivyo uwepo wa miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua utasaidia kuongeza upatikanaji wa maji katika kipindi hicho.

Amesema pia kuwa matumizi ya teknolojia za uvunaji wa maji ya mvua yatachangia katika uhifadhi wa rasilimali za maji na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya kawaida.

Wadau mbalimbali kutoka mamlaka za maji, viwanda na wenye mashamba makubwa, Kanda ya Kaskazini wakiwa katika kikao cha pamoja Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

Aidha, amesema teknolojia hizo zitaongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kusaidia upatikanaji wa maji hata katika vipindi vya ukame.

"Tunao mwongozo maalumu ambao tunaomba wenzetu wa halmashauri kupitia sheria ndogo ndogo wanapotoa vibali vya ujenzi kuwepo na ulazima wa kuweka kipengele cha kuweka miundo mbinu ya kuvuna maji ya mvua," amesema Segule.

Amesema; "Haya maji yote ya mvua tukiyavuna kwenye majumba yetu tutapunguza sana maji yanayoenda baharini bila kutumika lakini tunapunguza uhaba wa maji katika matumizi mbalimbali."

Segule amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanavuna maji ya mvua na kuweka miundombinu ya kuvuna maji hayo ili kupunguza na kukabiliana na upungufu wa maji hasa nyakati za ukame na kiangazi.

"Tukitunza maji kwenye mabwawa tunakuwa tumevuna yale maji ya mvua ambayo yakizidi yanaenda baharini. Wakati wa kiangazi tunalia hatuna maji, ilhali mengi yanaishia baharini," amesema Segule.

Ameongeza kuwa njia ya kuvuna maji ni muhimu kwa kujihakikishia usalama na upatikanaji wa maji kwa wakati unaohitajika. "Katika muktadha huo, tunasisitiza wananchi kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua," amesema.

Mmoja wa wadau, Hossea Mollel, amesema kuwa kikao hicho kimeibua mawazo na mapendekezo chanya yatakayosaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa maji, hususan katika vipindi vya ukame.

"Mawazo haya ni mazuri na yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya maji kwenye matumizi mbalimbali ya wananchi, hususani katika kipindi hiki chenye athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naye, Mdau mwingine, Bibiana Olambo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kulinda mazingira na kuhakikisha vyanzo vya maji vinabaki salama kwa manufaa ya jamii.

"Kikao hiki kimetusaidia kukutana wadau na tumewekeana mikakati mbalimbali ya kukamilisha mwaka 2026/2027," amesema Olambo.