Wafanyakazi wa Tanga wawasilisha hoja 16 wakitaka hatua za haraka kuboresha mazingira ya kazi
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Batilda Burian akijumuika kusherehekea sikukuu ya Mai Mosi na wafanyakazi katika uwanja wa Mkwakwani kimkoa jijini Tanga.
Tanga. Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Mkoa wa Tanga limeiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kutatua kero 16 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi na huduma kwa jamii.
Shirikisho hilo limesmea changamoto hizo zinaathiri moja kwa moja tija na ufanisi wa wafanyakazi.
Mratibu wa Tucta Mkoa wa Tanga, Athuman Kayumba ameeleza mambo 16 kwenye maadhimisho ya Mei Mosi, jijini Tanga kwamba kuongezeka kwa matatizo ni kikwazo katika sekta mbalimbali na kuomba Serikali kuyafanyia kazi kwa haraka.
Miongoni mwa hoja hizo ni maombi ya kupandishwa mishahara ya wafanyakazi ili kuendana na hali halisi ya maisha.
Shirikisho hilo limeeleza kuwa gharama za maisha zimepanda kwa kasi kubwa katika huduma muhimu, na kuwaweka wafanyakazi katika wakati mgumu wa kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Batilda Burian akipokea maandamano ya wafanyakazi kwenye maashimisho ya sikukuu ya wafanyakazi May Mosi katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
“Tunaiomba Serikali kuongeza mishahara ili kulinda utu wa mfanyakazi na kuhakikisha maisha bora,” amesema.
Kuhusu madai ya wafanyakazi, Kayumba ameeleza kuwa kuna malimbikizo mengi yasiyolipwa kwa wakati madai yanayohusisa likizo, uhamisho, matibabu na saa za ziada hali inayopunguza morali ya kazi.
Shirikisho hilo limeiomba Serikali kuhakikisha madai hayo yanalipwa bila kuchelewa na kuongeza kuwa kuchelewesha malipo ni kuwanyima haki wafanyakazi huku wakionya kuwa hali hiyo huathiri utendaji.
“Malipo ya haki za wafanyakazi yasicheleweshwe kwani ni msingi wa ufanisi kazini,” anasema mratibu huyo.
Kuhusu ajira, Kayumba amedai kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, baadhi ya waajiri hawatoi mikataba au hutoa mikataba isiyo halali, hali ambayo inachangia unyonyaji mkubwa kwa wafanyakazi.
Pia, wameomba Serikali kuwachukulia hatua waajiri wanaokiuka sheria hizo na wamependekeza ukaguzi wa mara kwa mara ufanyike sehemu za kazi, lengo likiwa ni kulinda haki za wafanyakazi.
“Serikali isimamie kikamilifu sheria za ajira ili kuondoa unyonyaji mahali pa kazi,” anasema Kayumba.
Kuhusu wastaafu Kayumba amezungumzia ucheleweshaji wa stahiki zao kwamba wafanyakazi wengi wanastaafu bila kupata haki zao kwa wakati, hasa nauli za mizigo zimekuwa changamoto kubwa.
“Ni aibu kwa mfanyakazi kuhudumu miaka mingi na kuondoka bila haki zake,” anasema Kayumba kwenye risala hiyo.
Amesema katika mabaraza ya wafanyakazi, baadhi ya waajiri hawazingatii sheria huku wengine hawafanyi vikao au hulipa posho pungufu, hali ambayo imekuwa ikidhohofisha majadiliano ya pamoja.
Kayumba ameiomba Serikali kusimamia utekelezaji wa sheria hizo kikamilifu na kupendekeza ufuatiliaji wa karibu ufanyike ili kusaidia kulinda haki za wafanyakazi.
Pia, wamelalamikia kuwepo kwa mishahara chini ya kima cha chini huku sekta zilizoathirika zikiwa ni majumbani, hotelini na afya binafsi huku wakiomba Serikali kuchukua hatua.
Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amesema Serikali imezipokea changamoto hizo.
Amesisitiza kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya waajiri wanaokiuka sheria huku akiagiza viongozi kusimamia haki za wafanyakazi.
Wafanyakazi wakisherehekea Mai Mosi kimkoa katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Dk Batilda amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi. Aidha, amehimiza utekelezaji wa sheria zote za kazi lengo likiwa ni kuhakikisha haki zinazingatiwa kikamilifu.
“Serikali itaendelea kulinda haki za wafanyakazi na kuchukua hatua kali kwa wanaokiuka sheria,”anasema.