Wagonjwa wa Moyo Malawi Kutibiwa nchini

Muktasari:

  • Wagonjwa wa magonjwa ya moyo nchini Malawi wanatarajia kupatiwa matibabu hapa nchini kufuatia uhaba wa matibabu ya moyo nchini humo.

Dar es Salaam. Wagonjwa wa magonjwa ya moyo nchini Malawi wanategemea kuanza kutibiwa hapa nchini kupitia Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kufuatia mazungumzo ya serikali ya Malawi na Tanzania kupitia Balozi wa Tanzania nchini Malawi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Peter Kisenge katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini hapa.

"Taasisi yetu ilituma madaktari saba  kwenda nchini Malawi mnamo April 8 - 10, 2023 kwa nia ya kutoa huduma ya magonjwa ya moyo Malawi kutokana na uhaba wa madaktari wa moyo nchini humo,"

Amesema kwamba hatua hiyo ni kufuatia mazungumzo ya Uongozi wa Malawi na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole katika kutafuta namna ya kuwasaidia wagonjwa hao nchini humo.

"Walichagua taasisi yetu kwa sababu JKCI ndio taasisi bora ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ndio maana taasisi yetu ikapewa Kipaumbele," amesema Dk Kisenge.

Pia Dk Kisenge amesema hatua hiyo inawapa fursa ya kueneza 'Utalii Tiba ambayo ni adhma ya Rais Samia Suluhu katika kutangaza huduma bora za kiafya zinazotolewa na hospital kubwa za hapa nchini.

"Madaktari wetu walivyokwenda waliwaona wagonjwa 700 na kati yao 523 walikutwa na Magonjwa ya moyo ambao wanatakiwa kuja nchini kitibiwa na kati ya hao wapo ishirini ambao wanahitaji matibabu ya haraka, " amesema Dk Kisenge.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji (JKCI) Dk Angela Muhozya ambaye  alikuwa ni kiongozi wa Msafara wa Madaktari walioenda Malawi amesema kati ya wagonjwa waliowaona Kuna wagonjwa 200 ambao wanahitaji upasuaji mkubwa.

"Kama nchi na kama taasisi tunaangalia ni namna gani tunaweza kuisaidia Malawi kufika hapa nchini ili kupata huduma hizo kwani wao bado hawana taasisi kama yetu ambayo inaweza kutoa matibabu kama hapa kwetu," amesema Dk Muhozya.

Pia Dk Muhozya amebainisha kuwa mbali na Malawi, wanatazamia kupeleka huduma hiyo ya matibabu ya moyo katika nchi nyingine za jirani.

Naye Dk Stella Mongela ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Kwa watoto ambaye ni miongoni mwa madaktari saba ambao walienda Malawi amesema kati ya watoto 200 wenye matatizo ya moyo ambao waliwafanyia uchunguzi nchini Malawi, 80 wanahitaji uchunguzi zaidi ili kuona kama ni salama wao kuendelea na upasuaji.

"Changamoto kubwa Malawi ni kwamba watoto wengi huzaliwa na Matatizo ya moyo na wanachelewa kugundulika na changamoto kubwa zaidi ni uchache wa huduma Malawi," amesema Dk Mongela.

Dk Mongela amesema wamewasiliana na Malawi kuhakikisha wagonjwa ambao wanahitaji matibabu ya haraka wafikishwe hapa nchini ili wapate matibabu ya haraka kuokoa maisha yao.