Waislamu wahimizwa kujiepusha na ukabila, udini

Waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa wanatoka katika msikiti wa Ngazija jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuswali swala ya Eid El fitri leo Jumamosi Aprili 22, 2023. Picha na Emmanuel Msabaha

Muktasari:

  • Waumini wa dini ya Kiislamu wameaswa kutenda maadili mema, huku wakihimizwa kuhusu upendo kwa watu bila kujali dini wala makabila yao.

Dar es Salaam. Waumini wa dini ya Kiislamu wameaswa kutenda maadili mema, huku wakihimizwa kuhusu upendo kwa watu bila kujali dini wala makabila yao.

 Hayo yameelezwa na imam wa msikiti wa Ngazija jijini hapa, Sheikh Issa Ibrahim leo Aprili 22 wakati akitoa mawaidha ya sikukuu ya Eid El Fitr.

"Pendaneni bila kujali dini wala ukabila, kwani mtume anasema kwa yeyote atakaye mpenda na kumthamini mwenzake basi atapata swawabu kwa mwenyenzi Mungu," amesema.

Ameongeza kwa kusema mbali na kuwa na maadili mema wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha wanawalea watoto katika njia ipasayo, kwa kuwafundisha matendo mema.

"Dunia kwa sasa imeharibika wazazi pamoja na walezi hakikisheni mnawalea watoto wenu katika njia sahihi ili wanapokuja kuwa wakubwa wawe kioo kwa kizazi kinachofuata," amesema.

Kuhusu sikukuu hiyo amesema, ni vyema kwa mwislamu yeyote kuendelea kutenda mema na haki kama ilivyo kuwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani. 

"Msiishie hapa bali mkaendelee kutenda yale mema kama mlivyokuwa mnafanya kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani, heshima na utu baina ya mtu na mtu iwepo naye Allah atawajalia kheri," amesema.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kuswali swala ya Eid El fitri katika msikiti huo, Rajabu Saddick amesema atahakikisha anaenenda katika njia ipasayo kama ilivyo kuwa katika kipnd chote cha mwezi mtukufu.

"Kama Sheikh alivyotusii basi na mimi nina waasa Waislamu wenzangu wote duniani na hata wasio waislamu kuhakikisha wanatenda yale ambayo yanampendeza Allah na Mtume Mohamad.

"Nitafurahi kuona nchi yangu inaendelea kuwa na amani na ushirikiano kama ilivyo kuwa toka enzi na enzi,” amesema Saddick

Rehema Ommary yeye amewaasa wanawake wenzake kuhakikisha wanakuwa mfano bora kwa watoto wao, kwa kuwapatia elimu bora ya dini ambayo itawasaidia kuwa na maadili mema na sahihi katika jamii zao.

"Ningependa kuwaasa wanawake wenzangu kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi ya dini ili wanapokuja kuwa wakubwa wawe na mienendo mema na sahihi katika jamii zinazowazunguka," amesema.

Ameongeza na kusema mbali na kuwalea watoto katika misingi ya dini kama wazazi wanatakiwa kuhakikisha wanawapatia watoto elimu bora, kwaajili ya maendeleo ya taifa," ameeleza