Wajawazito watahadharishwa kutumia dawa hizi...

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Dk Eusebi Kessy akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Ofisini kwake, Rachel Chibwete.

Muktasari:

  • Serikali wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma yawatahadharisha wajawazito kuacha matumizi ya dawa za kienyeji zinazodaiwa kuongeza uchungu wakati wa kujifungua, kwani zinachangia vifo vitokananvyo na uzazi wilayani humo.

Chamwino. Serikali wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma yawatahadharisha wajawazito kuacha matumizi ya dawa za kienyeji zinazodaiwa kuongeza uchungu wakati wa kujifungua, kwani zinachangia vifo vitokananvyo na uzazi wilayani humo.

 Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Dk Eusebi Kessy wakati akifanya mahojiano maalumu na Mwananchi Digital, ambapo amesema, dawa hizo zimezoeleka kutumika kwa ajili ya kuharakisha uchungu.

“Madhara yake ni makubwa, maana zinawafanya watokwe na damu nyingi wakapojifungua, jambo ambalo linahatarisha si tu uhai wao, pia kwa watoto wanaotarajia kujifungua, Hii ni changamoto kubwa kwani dawa hizi hazijathibitishwa kitaalam,” amesema na kuongeza;

“Mara nyingi tabia hii ipo sana kwa wanawake wale ambao wanahisi wamepitiliza siku zao za kujifungua...huamua kutumia dawa hizo ili wajifungue haraka, hi ini hatari kwa afya zao, tuna kesi nyingi ambapo watumiaji wa dawa hizo wamepoteza maisha baada ya kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua.”

Daktari huyo anasema dawa hizo zimesababisha baadhi ya akina mama kupoteza maisha kutokana na kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua na hata kupoteza maisha ya watoto.

Anasema wanawake wengi waliotumia dawa hiyo ya kuongeza uchungu miji yao ya mimba huwa inachanika na kusababisha kutokwa na damu nyingi na wakicheleweshwa hospitalini wanaweza kupoteza maisha.

Katika kulithibitisha hilo, Mganga huyo amesema kuwa wanawake 14,090 walijifungua wilayani hapo kwa mwaka 2022, na kwamba waliopoteza maisha ni watano, huku asilimia 90 ya vifo vyao ikitokana na kupoteza damu nyingi wakati wanajifungua.

Aidha Dk Kessy ametoa wito kwa wajawazito kuanza kliniki mapema ambapo muda sahihi ni pale mimba inapofikisha wiki 12, na kwamba watapata chanjo na huduma zote muhimu wakati wa ujauzito ambazo zitamuwezesha kujifungua salama.

Hat hivyo, amesema licha ya kuwepo kwa changamoto hizo, bado wanawake wengi wanajifungulia kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zilizopo wilayani hapa.

“Takwimu zinaonyesha asilimia 98.6 ya wajawazito hujifungulia kwenye sehemu hizi za afya yaani zahanati, vituo vya afya na hopitali, huku asilimia zilizobaki, wanajifungulia njiani, nyumbani kwa msaada wa ndugu na kwa wakunga wa jadi,” amesema Dk Kessy.

Hata hivyo changamoto ya kutohudhuria kliniki kwa baadhi ya wajawazito kunamuumiza sana Dk Kessy ambapo amesema kuna wanawake wanabeba mimba maoaka wanafikia hatua ya kujifungua bila ya kuhudhuria kliniki.

Amesema wengi wa wanawake hao, ndiyo ambao hukutwa na changamoto za upungufu wa damu, kwani hawajafanya vipimo vyovyote vya kujua afya zao ikiwemo wingi wa damu kwa ajili ya usalama wao na watoto walioko tumboni.

Kauli hiyo inaungwa mkono na daktari wa upasuaji kutoka Hospitali ya Mvumi Misssion, Dickson Baltazar ambaye anasema changamoto hiyo ipo na ni kubwa katika wilaya hiyo kwani wajawazito wengi hasa wa vijijini wanapenda kutumia dawa hizo za kuongeza uchungu.

“Unakuta kutokana na sababu za kitaalamu mama anatakiwa kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, sasa akibeba mimba nyingine anataka ajifungue kwa njia ya kawaida bila kujua sababu zilizosababisha kufanyiwa upasuaji kwenye mimba iliyotangulia, hivyo analamisha kunywa dawa hizo ili apate uchungu,” amesema Dk Baltazar.

Amesema kesi hizo zimekuwa nyingi hasa kwa wanawake wanaotoka vijijini ambao hufikishwa hospitalini hali zao zikiwa mbaya baada ya kuvuja damu kutokana na mfuko wa uzazi kupasuka.

Daktari huyo amesema japo dawa hizo zinasababisha uchungu, lakini njia ya mtoto kutoka inakuwa haijafunguka, hivyo husababisha mtoto kuzaliwa akiwa amechoka, anashindwa kupumua na mwisho anapoteza maisha.

“Kibaya zaidi wanawake hao huwa hawakubali kuwa wametumia dawa za kuongeza uchungu, lakini wanapofika hospitalini huwa tunajua kutokana na hali anayokuja nayo kwa sababu wanakuwa na hali mbaya kuliko wenzao ambao hawajatumia hizo dawa,” amesema Dk Baltazar.

Kwa upande wa mmoja wa wakunga wa jadi kutoka Kijiji cha Chilonwa, wilayani Chamwino, Hawa Malima, amesema dawa hizo za kuongeza uchungu zimekuwa zikitumiwa tangu zamani na zimekuwa na mafanikio kwa akina mama wengi.

Kwa mujibu wa Mkunga huyo wa jadi, mama mjamzito anapewa dawa hizo pale anapoonyesha dalili za uchungu lakini hajifungui, hivyo anapokunywa humrahisishia kujifungua haraka.

Anataja dawa hizo kuwa ni upupu uliochemshwa na mizizi ya mgomba wenye mkungu wa ndizi ambazo huchemshwa na kupewa mama mjamzito ili kuharakisha uchungu.

Mkunga huyo anasema wanawake wengi walikuwa wanatumia njia hiyo kujifungua haraka na walikuwa hawalazimiki kwenda hospitalini tofauti na siku za hivi karibuni.

“Hata hivyo, wanawake ambao hawajifungui hata baada ya kupewa dawa hizo, hukimbizwa hospitalini kwa ajili ya msaada zaidi,” amesema na kuongeza;

“Changamoto huwa inatokea pale mjamzito amekunywa dawa hiyo na bado akashindwa kujifungua kwa wakati kwani wengi wao hupoteza watoto na hata maisha yao yanakuwa hatarini kutokana na kupoteza damu nyingi.”