Wajifungia kujadili mikakati ya kupambana na ukatili wa kijinsia
Wadau wa elimu katika Jiji la Tanga wakishiriki katika jukwaa la vita dhidi ya ukatili, unyanyasaji na unyonyaji wa kingono katika makundi mbalimbali ya kijamii, lililoandaliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania kwa kushirikiana na Tanzania Bora Initiative (TBI) pamoja na Kuckuck Production. Picha na Mbonea Herman.
Muktasari:
- Mkoa wa Tanga umeanza utekelezaji wa programu ya Fit for PSEAH? Forum Theatre inayolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu kuzuia ukatili, unyanyasaji na unyonyaji wa kingono katika makundi mbalimbali ya kijamii.
Tanga. Kutokana na Mkoa wa Tanga kuwa miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya vitendo vya ukatili katika makundi mbalimbali ya jamii, wadau wa elimu, Serikali na maendeleo wamekutana jijini Tanga kujadili mikakati ya kuzuia na kukabiliana na vitendo hivyo kupitia programu ya Fit for PSEAH? Forum Theatre.
Programu hiyo imeandaliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania kwa kushirikiana na Tanzania Bora Initiative (TBI) pamoja na Kuckuck Production, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya unyanyasaji, unyonyaji na ukatili wa kingono, sambamba na kuimarisha mifumo ya ulinzi, uwajibikaji na utoaji wa taarifa.
Tukio hilo limewakutanisha wanafunzi, walimu, wazazi, viongozi wa Serikali, maafisa elimu, maafisa ustawi wa jamii, maafisa maendeleo ya jamii, Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi pamoja na wataalamu wa masuala ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza katika programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Bora Initiative (TBI), Ismail Biro, amesema mradi huo unalenga kuunganisha nguvu za jamii katika kuzuia vitendo vya ukatili na kuhakikisha makundi yote yanapata ulinzi na msaada unaostahili.
"Kuzuia unyanyasaji, unyonyaji na ukatili wa kingono ni wajibu wa kila mmoja. Tunahitaji jamii yenye uelewa, uwezo wa kuchukua hatua na kujenga mazingira ambayo kila mtu analindwa na kuheshimiwa," amesema Biro.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za maendeleo na jamii ni muhimu katika kujenga mazingira salama yatakayowawezesha waathirika kupata msaada kwa wakati na wahusika kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Saimon Mdende, amesema matumizi ya mbinu ya Forum Theatre yameleta njia rahisi na shirikishi ya kutoa elimu kwa jamii kupitia maigizo yanayoakisi hali halisi ya maisha ya kila siku.
Amesema mbinu hiyo inawapa washiriki nafasi ya kuchambua changamoto zinazowakabili na kushiriki kutafuta suluhisho la pamoja.
"Mradi huu ni muhimu kwa sababu unawapa watu nafasi ya kueleza changamoto zao na kushiriki kutafuta suluhisho la ukatili unaotokea katika jamii," amesema Mdende.
Naye Afisa Elimu Taaluma wa Shule za Sekondari wa Jiji la Tanga, Salome Materu, amesema programu hiyo itawasaidia wanafunzi pamoja na jamii kutambua aina mbalimbali za ukatili, namna ya kujilinda na sehemu sahihi za kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo hivyo.
Amesema kupitia maigizo ya Forum Theatre, washiriki wamepata fursa ya kushuhudia matukio yanayofanana na hali halisi ya jamii, kuyajadili na kupendekeza hatua zinazoweza kusaidia kuyazuia.
"Kupitia Forum Theatre, washiriki wamepata nafasi ya kuona matukio yanayofanana na hali halisi ya jamii, kuyajadili na kupendekeza hatua za kuzuia vitendo hivyo," amesema.
Akizungumzia manufaa ya programu hiyo, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Old Tanga, Amina Salama Abdalah, amesema elimu waliyoipata imewawezesha wanafunzi kutambua haki zao na umuhimu wa kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili.
"Tumeelewa kuwa ukatili unaweza kutokea katika mazingira tofauti na kwa watu mbalimbali. Programu hii imetufundisha kutoa taarifa mapema, kusaidiana na kujenga mazingira salama shuleni," amesema Amina.
Mradi huo wa miezi 12 unaotekelezwa na Tanzania Bora Initiative kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania utaendelea kutekelezwa katika mikoa mingine, ikiwemo Arusha, Dodoma, Mbeya, Mtwara na Mwanza.
Wadau waliohudhuria programu hiyo wamehimiza wazazi, walimu, wanafunzi, viongozi wa Serikali na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kuzuia, kuripoti na kupambana na vitendo vya ukatili ili kujenga jamii salama, yenye heshima na ulinzi kwa kila mwananchi.