Wakopeshaji ‘kausha damu’ mtegoni Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza na wafanyabiashara katika Soko la Makumbusho

Muktasari:

  • Wingi wa taasisi na watu binafsi wanaotoa mikopo umiza 'kaushadamu' kwa wananchi, umemuibua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyeagiza wakamatwe.

Dar es Salaam. Huenda biashara ya mikopo ya ‘kausha damu’ ikawa si dili tena katika Manispaa ya Kinondoni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aagize kukamatwa kwa wakopeshaji hao.

Agizo la Chalamila ni matokeo ya hoja ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule aliyesema kumezuka taasisi na watu wengi binafsi wanaotoa mikopo hiyo.

Katika hoja yake hiyo, Mtambule amesema: "Tumekubaliana na wenzetu wa Jeshi la Polisi wataitwa wote (wakopeshaji) tuzungumze nao na kuwataka wazingatie utaratibu wa kisheria na wale wanaotoa mikopo bila vibali wafuate utaratibu."

Licha ya hatua hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, Chalamila ametaka hatua zaidi ikiwemo kukamatwa hasa wale wanaofanya biashara hiyo kinyume na matakwa ya sheria.

Chalamila ametoa agizo hilo leo Jumatano Agosti 16, 2023 katika mkutano wake na wafanyabiashara wa soko la Makumbusho jijini hapa.

"Kuna benki zimekuja hawa ambao hawana utaratibu Mkuu wa Wilaya (Mtambule) kamateni, shida yetu sisi viongozi unaweza ukatuma mtu kamata huyu akikuonyesha hela unakosa maneno," amesema.

Katika hatua nyingine, Chalamila ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Kinondoni kuwakamata na kuwahoji wanaotuhumiwa kupangishia wafanyabiashara vizimba katika soko la Makumbusho.

Ametaka hilo lifanyike kabla ya saa 10 jioni ya leo na kwamba kesho saa 2 asubuhi atahitaji taarifa ya kukamatwa kwao.

Hoja nyingine iliyoibuliwa katika mkutano huo ni wafanyabiashara kutozwa fedha Sh5,000 ili kupewa fomu ya mkopo kutoka benki ya NMB ilhali inapaswa kutolewa bure.

Katika hilo, Chalamila ametaka hadi kesho saa 2 asubuhi fedha hizo ziwe zimerudishwa kwa wenyewe na kwamba waliokusanya wakamatwe na Takukuru.

Mkuu huyo wa Mkoa, amekazia hatua iliyofanywa na Mtambule ya kusimamisha uongozi wa soko hilo, akisema hawapaswi kuwa sehemu ya watakaogombea tena nafasi hizo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Akizungumza katika mkutano huo, Diwani wa Kijitonyama, Damas Lusangija amesema miongoni mwa malalamiko ya wafanyabiashara katika eneo hilo ni uongozi hatua iliyochagiza uvunjwe.

Changamoto nyingine ni wafanyabiashara kuuziwa meza hadi Sh1 milioni ilhali zinapaswa kupangishwa kwa Sh15,000 kwa mwezi.

"Wafanyabiashara hawa walikuwa wanahitaji uongozi wa soko utakaotetea maslahi yao bila kubughudhi mapato yao," amesema Diwani huyo.

Akisoma taarifa ya hali ya soko hilo, Kaimu Ofisa Biashara Manispaa ya Kinondoni, Shadrack Francis amesema jumla ya wafanyabiashara 883 wanafanya shughuli zao katika eneo hilo.

Idadi hiyo, ameeleza inajumuisha wale wa vizimba (140) mama na baba lishe (34), meza za mitumba (235), fremu (228), mabanda tisa na stoo mbili.

Ameeleza katika soko hilo, Serikali imekuwa ikitoa kodi ya fremu Sh40,000 kwa mwezi na Sh15,000 kwa kizimba.

Kutokana na tozo na kodi hizo, Shadrack amesema mwaka Julai mwaka huu Sh18.45 milioni zimekusanywa na Manispaa ya Kinondoni kutoka sokoni hapo.