Wakulima Mbeya, Songwe kupewa miche ya kahawa bure

Meneja utafiti wa zao la Kahawa, Dismas Pangalasi akizungumza kwenye kikao cha wadau wa zao hilo kutoka mikoa ya Mbeya ,Songwe na Ruvuma. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Shirika lisilokuwa la kiserikali la wadau wa kilimo (Ansaf) limesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, litatoa miche bure kwa wakulima wa kahawa mikoa ya Mbeya na Songwe.

Mbeya. Shirika lisilokuwa la kiserikali la wadau wa kilimo (Ansaf) limesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, litatoa miche bure kwa wakulima wa kahawa mikoa ya Mbeya na Songwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Honest Mseri amesema leo June Mosi mkoani  Mbeya kwenye kikao kilichohusisha  wadau wa sekta ya Kilimo, maofisa kilimo wa Serikali, wakulima na wafanyabishara kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Ruvuma.

“Tumekutana kuona namna bora ya kuboresha kilimo cha kahawa kutokana na umuhimu wake, ni vama kuwepo na mifumo ya upatikanaji wa miche bora ambayo italeta matokeo mazuri na kuongeza uzalishaji utakaokidhi mahitaji ya masoko la ndani na nje,” amesema.

Amesema njia bora ya kuhamasisha wakulima kuwekeza zaid ni kuboresha mahitaji yao muhimu ikiwemo upatikanaji wa miche bora kwani wastani wa asilimia 90 ya kahawa, masoko yake yako nje ya nchi.

“Tumelazimika kukutana na wadau lengo ni kutengeneza mifumo ya ndani ya masoko na kuwavutia  wakulima kuzalisha kwa tija ili waweze kujikwamua kiuchumi na kutoa ajira kwa vijana, ”amesema.

Kwa upande wake, Meneja uzalishaji wa kampuni ya ukoboaji wa Kahawa ya Mbimba Mkoa wa Ruvuma, Labeli Ulomi amesema kuwa wastani wa eneo lenye hekta 25, 000 zilizopo mkoani Ruvuma, ambazo zinastahiri tumika katika uzalishaji wa zao hilo, hazijafanyiwa kazi.

“Hii ni fursa pekee kwa wakulima kuona namna bora ya kuwekeza, sambamba na hilo, wilayani Nyasa; kuwa na hekta 6,000 ambazo hazijazalishwa zao lolote la kilimo na biashara,” amesema.

Naye Meneja program za utafiti wa kahawa Kanda, Dismas Pangalasi amesema katika kuona kilimo hicho kinakuwa na tija wakulima 9,530 wamepatiwa mafunzo ya mabadiliko ya tabia nchi.

Naye Mkulima, Jeremiah Mwaje amesema mabadiliko ya tabia nchi ni changamoto kwani awali alikuwa alipata mavuno mengi lakini kwa sasa uzalishaji umepungua kutokana na ukosefu wa mbegu bora inayoweza kukabiliana na magonjwa