Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima wa chumvi watajwa chanzo uharibifu wa mikoko

Miche ya mikoko ikiwa imepandwa kwenye vitaru, katika Pwani ya Mbanja Manispaa ya Lindi mkoani Lindi. Picha na Bahati Mwatesa



Muktasari:

  • Mikoko si tu kwamba ni kimbilio muhimu kwa samaki, bali pia ni kinga dhidi ya mmomonyoko wa udongo na mabadiliko ya tabianchi.

Lindi. Wakulima wa chumvi katika Manispaa ya Lindi wametajwa kuwa miongoni mwa wachangiaji wakuu wa uharibifu wa miti ya mikoko hali inayohatarisha mazalia ya samaki na kuongeza kasi ya mmomonyoko wa udongo katika maeneo ya Pwani.

Wakizungumza jana Jumapili Julai 27, 2025 wakati wa zoezi la upandaji wa mikoko katika eneo la Mbanja, baadhi ya wananchi walieleza kuwa ukataji wa miti hiyo umeongezeka, hasa kwa ajili ya matumizi ya kujengea nyumba na kufungua mashamba ya chumvi.

Mkazi wa Mbanja, Romeo Andrew amesema licha ya mikoko kuwa nguzo muhimu katika mfumo wa ikolojia wa baharini, bado wananchi wamekuwa wakiikata kwa matumizi binafsi, ikiwemo ujenzi na kilimo cha chumvi.

Mratibu wa Mradi kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Jamii Ustawi na Mikoko (Hudefo), Abdi Khalifa akiwaelekeza wananfunzi aina ya mikoko. Picha na Bahati Mwatesa.

“Wananchi wengi wamekuwa wakiharibu mikoko kwa ajili ya kujengea nyumba kwani miti yake ni imara, lakini pia wakulima wa chumvi wanaikata ili kufungua mashamba yao. Hii ni hatari kwani samaki wanakimbia maeneo haya kutokana na kukosekana kwa chakula,” amesema Andrew.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Huduma Jamii, Ustawi na Mikoko (Hudefo), Abdi Khalifa amesema shirika hilo lilitumia maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani Julai 26 kutoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbanja kuhusu umuhimu wa mikoko.

“Jana tuliwapatia elimu wanafunzi kuhusu aina na umuhimu wa mikoko, leo tumewaleta pwani kupanda miche katika maeneo yaliyoathirika. Tunaamini watakuwa mabalozi wazuri katika familia na jamii zao,” amesema Khalifa.

Naye mwanafunzi wa shule hiyo, Sabra Kitenge alisema elimu waliyoipata wataifikisha kwa wazazi na marafiki ili kuokoa mikoko ambayo ni makazi na chanzo cha chakula kwa samaki.

“Nitawaambia wazazi kuwa mikoko ikiharibiwa, samaki wanapoteza chakula na sisi tunakabiliwa na mmomonyoko wa udongo,” alisema Sabra.

Zaidi ya miche 1,000 ya mikoko ilipandwa katika eneo la Mbanja na wanafunzi 30 wa shule hiyo ikiwa ni juhudi za kurejesha mazingira yaliyoharibiwa.