Wakulima wa korosho wapewa tahadhari kuhifadhi fedha nyumbani

Muktasari:

  • Wakulima wa korosho Kanda ya Kusini wametakiwa kuhifadhi fedha zao benki ili kuepukana na matatizo ya kiuhalifu hususan kipindi hichi cha msimu wa mauzo.

Mtwara. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abass Ahmed amewataka wakulima wa korosho kuacha kukaa na fedha nyingi za mauzo ndani badala yake wafungue akaunti benki ili kujiepusha na uhalifu vilevile kuweka akiba.

Kanali Abass amesema katika kipindi hiki cha msimu wakulima wengi hupata matatizo ya kiuhalifu kwa kukaa na fedha nyingi ndani badala ya kuzihifadhi sehemu salama ikiwemo benki.

Amesema kuhifadhi fedha benki inampa mwekaji nidhamu nzuri ya fedha kwa kipindi kirefu na kusaidia nyakati ngumu au za dharura.

“Suala la kuweka akiba ni muhimu maana yanaibuka masuala ya dharura ambayo yanahitaji fedha iwapo huna akiba unaweza kupata wakati mgumu lakini kama kuna akiba kwenye akaunti yako unatatua jambo lako kwa urahisi,” amesema.

Kanali Abass ameyasema hayo leo Novemba 2, 2023 wakati Benki ya NMB ilipokuwa ikizindua kampeni maalumu ya ‘Bonge la Mpango, Mchongo wa Kusini’ mahususi kwa wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za benki hiyo kwa wakulima na vyama vya ushirika.

“Nitumie nafasi hii niwasihi wana Mtwara kutumia fursa hii kwa nguvu kwani ni kwa manufaa yako binafsi, tujifunze kuweka akiba maana akiba ni msaada mkubwa na namna ambavyo itakusaidia ni ya kipekee,” amesema.

Kwa hiyo niwasihi ndugu zangu, kwa wenye akaunti za benki ya NMB huu ndio wakati wa kuzitumia vyema kwa kipindi hiki tunachoenda kufanya mauzo ya korosho zetu, tuwasihi wanunuzi wote kutulipa kwa kuweka fedha kwenye akaunti kwani ni salama na pia inakwenda kukuhamasisha kuweka akiba.

Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng’ingo amesema kuwa kupitia kampeni hiyo mkulima mmoja atakuwa akijishindia pikipiki moja kila mwisho wa wiki kupitia droo kwa muda wa wiki tano.

Vile vile wakulima watano watajinyakulia fedha taslimu Sh100,000 kila mmoja katika kila droo.

“Maana yake ni kwamba kila wiki tutashuhudia wakulima watano wakijishindia fedha taslimu itakayowekwa katika akaunti zao na mmoja pikipi,” amesema Faraja.

Amesema mpango huo unalenga kuhamasisha wakulima juu ya suala zima la uwekaji wa akiba kupitia akaunti zao benki na kupitisha malipo yao benki na kwa lugha nyepesi

Mkulima mmoja, Raphael Millanzi ameishukuru NMB kwa kuja na mpango huo kwa mara ya pili na kusema kuwa unawasaidia kuwa na utamaduni wa kuweka akiba katika njia salama lakini vile vile kupata zawadi ya pikipiki na fedha taslimu.