Wakulima wa pareto waonywa ubora
Ofisa wa Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) mikoa ya Mbeya na Songwe ,Mussa Malubano (kushoto) akikabidhi mchango wa saruji na mabati kwa Padri wa kanisa katoliki parokia ya Irambo Wilaya ya Mbeya, Ambrose Mponzi (kulia) leo Jumapili ,Desemba 3,2023. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) imewatahadhisha wakulima Mbeya na Songwe kuuza kwa wakati zao hilo ili kulinda ubora wa masoko.
Mbeya. Wakulima wa Pareto wameonywa kuacha tabia ya kuficha na kuhifadhi maua ya zao hilo katika sehemu zisizo salama hali inayo sababisha kupungua ubora wa sumu inayohitajika kwenye masoko ya ndani na nje .
Ofisa wa Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) Mikoa ya Mbeya na Songwe , Mussa Malubano amesema hayo leo Jumapili Desemba 3,2023 wakati akizungumza na wakulima baada ya kuchangia mabati na saruji kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Irambo Wilaya ya Mbeya vijijini.
“Kumeibuka tabia ya wakulima pindi wanapochuma maua na kuyakausha wamekuwa wakificha ndani kwa lengo la kuuza kwa bei kubwa pasipo kujua wanapunguza ubora na kuwa katika hatari kubwa ya kupata unyevu na kujikuta wakiuza kwa bei ya hasara,” amesema
Amesema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakikumbana na changamoto maua kutokuwa na ubora huku sababu kubwa ikiwa ni wakulima mara baada ya kukausha huyaficha ndani jambo ambalo limekuwa likiwasababishia hasara kubwa.
“Tuna taarifa wakulima mmeficha maua ya pareto ili ukifika mwishoni mwa Desemba mwaka huu , na Januari 2024 ndipo mtauza wakati mkiwa na mahitaji ya fedha ,jamani toeni muuze pesa zipo tutawalipa ili kutupunguzia gharama za kukausha upya yanapokuwa na unyevu,”amesema.
Ameongeza kuwa “Niwasihi toeni maua ingizeni sokoni kama mnahitaji fedha kwa ajili ya mahitaji mwishoni mwa mwaka na mwanzoni pesa zipo kikubwa tunahitaji maua yaliyo na ubora unaokidhi masoko na sio kupungua ubora,”
Katika hatua nyingine amesema katika kuhakikisha kilimo hicho kimekuwa na ubora tayari wametoa mbegu kwa wakulima mikoa ya Mbeya na Songwe sambamba na ujenzi wa mabati 100 ya kukaushia maua.
Malubano amesema licha ya kuwekeza kwenye sekta ya kilimo pia wamegusa kuchangia miradi ya elimu, afya na mahitaji mengine yanayogusa jamii ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali kugusa walengwa.
“Hatutaishia kwenye masuala ya kilimo na kijamii pia tunarejesha michango yetu hata katika madhehebu ya kidini kwa kutambua hata wakulima wetu ni miongini mwa waumini wanapata huduma za kiroho,”amesema.
Kwa upande wake Chifu wa wazalishaji wa zao la pareto Kanda ya Kusini, Herman Mwaifwani amesema kufuatia changamoto ya wakulima kutouza maua kwa wakati ufike wakati makampuni kabla ya kununua waanze kupima ubora ili kubaini yaliyopoteza sifa na kurejesha kwa walengwa.
“Tabia hiyo imeota mizizi na ndio sababu inapoteza sifa kwa masoko ya nje umefika PCT wekeni vigezo pindi wanapokuja kuuza ,kwanza mtazame imekaa ndani kwa muda gani maana wapo wakulima wanaficha kwa zaidi ya miezi mitano ili wauze kwa bei ya Juu ”amesema.
Pia ameshauri kampuni hiyo kuongeza bei ya kununua pareto kutoka Sh3,500 mpaka Sh5,000 kama Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe hali ambayo itahamasisha wakulima kuuza kwa wakati mara baada ya kukaushwa.
Kwa upande wake ,Paroko wa Kanisa hilo, Padre Ambrose Mponzi ameshukuru wadau hao kwa kuchangia mahitaji ya ujenzi wa kanisa hilo licha kuwepo na mahitaji mengine .
“Hii ni nyumba ya Mungu ,tunashukuru sana kwa mchango utatuvusha katika hatua fulani ,pia tuombe Watanzania wengine kujitokeza kuchangia ili tukamilishe kwa wakati kwani hilo tunalohudumu sasa ni dogo waumini wanajipana sana”amesema.