Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walikotoka, walichofanya majaji wapya walioteuliwa na Rais magufuli

Dar es Salaam. Juzi Rais John Magufuli alifanya uteuzi wa jumla ya majaji 21 kwa mpigo katika ngazi mbili za mhimili wa Mahakama nchini, ukiwa ni uteuzi mkubwa zaidi, kwa maana ya majaji wengi kuteuliwa kwa wakati mmoja katika historia ya Mahakama nchini.

Kabla ya hapo uteuzi mkubwa ulikuwa ni wa majaji 20 walioteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Agosti 2014, ukiwa punngufu ya jaji mmoja tu kulinganisha na uteuzi wa sasa.

Hata hivyo, wakati Rais mstaafu Kikwete aliteua idadi hiyo ya majaji katika ngazi moja tu (Mahakama Kuu), Rais Magufli amefanya uteuzi huo mkubwa kwa ngazi zote mbili, Mahakama Kuu (majaji 15) na Mahakama ya Rufani (majaji 6).

Hivyo utezi wa majaji 20 kwa Mahakama Kuu ndio uteuzi pekee hadi sasa mkubwa kuwahi kufanyika katika ngazi ya Mahakama, huku uteuzi wa sasa wa majaji sita wa Mahakama ya Rufani, ukiwa ndio uteuzi mkubwa zaidi katika ngazi hiyo.

Katika uteuzi wa juzi, majaji wateule sita wa Mahakama ya Rufani, wote walikuwa majaji wa Mahakama Kuu na majaji wateule 15, wanatoka katika nyanja maeneo tofauti.

Wapo waliokuwa na nyadhifa za uhakimu, usajili na wengine wametoka taasisi za umma kama vyuo vikuu, idara, ofisi za Serikali ikiwamo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wengine wakiwa ni mawakili wa kujitegemea.

Mwananchi linachambua kwa ufupi ili kujua nani alikuwa wapi kabla ya uteuzi huo na baadhi ya kazi walizowahi kufanya zikiwamo kesi walizowahi kuziendesha kwa wale waliokuwa mahakimu.

Majaji wateule wa Mahakama ya Rufani

Uteuzi huu wa majaji sita wa Mahakama ya Rufani kwa wakati mmoja, unaifanya mahakama hiyo sasa kuwa na jumla ya majaji 19 wa kawaida.

Mbali na majaji hao wa kawaida, pia kuna Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, ambaye anaifanya mahakama hiyo kuwa na majaji 20, huku yeye akiwa ndiye mkuu wa ngazi hiyo ya mahakama na mhimili wa Mahakama kwa jumla.

Majaji hao sita walioteuliwa ni Winfrida Beatrice Korosso, Barke Mbaraka Aboud Sehel, Lugano Mwandambo, Dk Mary Caroline Lavira, Ignas Pius Kitusi na Rehema Joseph Kerefu Sameji.

Jaji Korosso

Kabla ya uteuzi huo, Jaji Korosso, alikuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi. Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Agosti 2014, akiwa mmoja kati ya majaji 20 walioteuliwa na Rais mstaafu Kikwete. Kabla ya kuteuliwa katika wadhifa huo, alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP).

Miongoni mwa kesi alizozisikiliza ni ile iliyowavuta wengi kuifuatilia ya utoroshaji wa makontena 329 katika Bandari Kavu ya Azam (AICD).

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni maofisa wa TRA, maofisa wa AICD na raia wengine, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 110 likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.7 bilioni.

Washtakiwa wameshamaliza kujitetea baada ya Jaji Korosso kuwakuta na kesi ya kujibu na sasa kesi iko katika hatua ya majumuisho ya hoja huku ikitarajiwa kutolewa hukumu yake mwishoni mwa Februari.

Jaji Sehel

Kabla ya uteuzi huu alikuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara. Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Agosti 2014, naye akiwa miongoni mwa majaji 20 walioteuliwa na Rais mstaafu, Kikwete.

Akiwa Jaji wa Mahakama Kuu amesikiliza na kuamua kesi nyingi, lakini mojawapo ni kesi ya kikatiba ya hivi karibu iliyovuma sana, ya muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018.

Jaji Sehel ndiye aliyekuwa kiongozi wa jopo la majaji watatu waliokuwa wamepangwa kusikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa na wanasiasa watatu kutoka vyama viwili vya upinzani wakiongozwa na kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Hata hivyo Jaji Sehel hakuendelea na kesi hiyo baada ya Serikali kuweka pingamizi la awali ambalo lilisikilizwa na mmoja wa majaji wa jopo hilo, Jaji Dk. Benhajj Masoud, ambaye alikubaliana na pingamizi la Serikali na kuitupilia mbali kesi hiyo kabla ya kuendelea.

Jaji Mwandambo

Ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, akitokea Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, ambako alikuwa jaji wa kawaida.

Naye ni miongoni mwa majaji 20 walioteuliwa na Rais mstaafu, Kikwete, Agosti 2014.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji, alikuwa wakili wa kujitegemea katika kampuni ya uwakili ya Rex Attorneys.

Miongoni mwa kesi alizozisikiliza akiwa jaji wa Mahakama Kuu ni iliyowahusu waliokuwa wabunge wanane wa viti maalumu wa Chama cha CUF waliovuliwa uanachana.

Wabunge hao walikuwa wakiiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine ilizuie Bunge kuwaapisha wabunge waliokuwa wameteuliwa kujaza nafasi zao, kusubiri kesi yao ya msingi, maombi ambayo Jaji Mwandambo aliyatupilia mbali akisema kuwa mahakama hiyo haiwezi kuuzuia mhimili huo kutekeleza majukumu yake.

Jaji Lavira

Jaji Dk Lavira kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu Mbeya. Naye ni miongoni mwa majaji 20 walioteuliwa na Rais mstaafu Kikwete, Agosti 2014.

Kabla ya kuteuliwa katika wadhifa huo, alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha cha mkoani Iringa.

Jaji Sameji

Jaji Sameji, kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani juzi, alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi.

Miongoni mwa kesi alizowahi kuzisikiliza akiwa Jaji wa Mahakama Kuu ni ya viongozi wakuu wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na wenzake wanane.

Hilo lilikuwa shauri la maombi ya marejeo wakiiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ifanye mapitio ili kujiridhisha na uhalali na usahihi wa mwenendo na amri za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Hata hivyo, Jaji Sameji alilitupilia mbali shauri hilo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la awali lililowekwa na DPP, kuwa uamuzi na amri zilizokuwa zikilalamikiwa haziwezi kukatiwa rufaa wala kuombewa mapitio kwa kuwa hazimalizi shauri.

Jaji Kitusi

Jabla ya uteuzi wa juzi, Jaji Kitusi alikuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Dodoma. Alipanda ngazi hatua kwa hatua, akianzia uhakimu kisha msajili, ambako pia alishika wadhifa huo kwa ngazi mbalimbali.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na kabla ya nafasi hiyo alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

Awali kabla ya kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, alikuwa Msajili wa Mahakama Kuu na kabla ya hapo alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu.

Pia, Jaji Kitusi ni Rais mstaafu wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) ambaye alimaliza muda wake wa utumishi ndani ya chama hicho mwaka jana.

Majaji wateule wa Mahakama Kuu

Licha ya uteuzi wa majaji 15, katika ngazi ya Mahakama Kuu, mahakama hiyo imenufaika na ongezeko la majaji tisa, kwani majaji sita wameziba nafasi zilizoachwa wazi na majaji sita walioteuliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.

Kwa uteuzi huo, sasa Mahakama Kuu imefikisha idadi ya majaji 69 wa kawaida, huku Jaji Kiongozi, ambaye ndiye mkuu wa mhimili huo akifanya idadi ya majaji wa Mahakama Kuu kuwa 70 nchini kote.

Majaji hao wateule wa Mahakama Kuu wanaoapishwa leo kuanza majukumu yao mapya ni John Rugelekahyoza, Cyprian Phocus Mkeha, Wilbard Mashauri, Dunstan Beda Ndunguru, Seif Mwinshehe Kulita, Dk. Ntemi Nimilwa Kilikamajenga na Zepherine Nyarugenda Galeba.

Wengine ni Dk Juliana Laurent Masabo, Mustapha Kambona Ismail, Yohane Bokobora Masara, Dk. Lilian Mihayo Mongella, Fahamu Hamidu Mtulya, Athuman Matuma Kirati na Susan Bernard Mkapa.

Jaji Kahyoza

Jaji mteule Kahyoza kabla ya kuteuliwa juzi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani.

Alianza utumishi wa Mahakama mwaka 1995 akiwa hakimu, akianzia mkoani Iringa, kisha mkoani Tanga, ambako alikuwa Hakimu Mkazi wa mkoa huo.

Baadaye alihamishiwa Musoma, kisha akateuliwa kuwa Msajili Mahakama Kuu Mbeya, baadaye alihamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kisha akawa Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania ndipo akahamishiwa Mahakama ya Rufani hadi uteuzi wa juzi.

Jaji Mteule Mashauri

Jaji Mashauri ni mmoja wa mawakili ambao jina lake katika miaka miwili hii limesikika sana katika nyanja ya sheria, hasa kutokana na kesi ambazo amekuwa akiziendesha, ikiwamo ya viongozi tisa wa Chadema.

Kabla ya uteuzi wa juzi alikuwa ni Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, pia amekuwa akikaimu nafasi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa nyakati tofauti.

Kesi hiyo ya viongozi wa Chadema ni moja ya kesi ambazo zimelifanya jina lake livume sana kwa wadau wa sheria na hata umma kwa jumla.

Ndiye anayesikiliza kesi hiyo ya jinai inayowakabili viongozi wa chama hicho akiwamo mwenyekiti wa taifa, katibu mkuu, manaibu makatibu wakuu Bara na Zanzibar na wabunge wa majimbo mbalimbali.

Kesi hiyo imelifanya jina lake livume sana kutokana na mwenendo wake ikiwamo kuibua mgogoro na washtakiwa hao ambao walifikia hatua ya kumtaka ajiondoe kusikiliza kesi yao maombi ambayo aliyakataa.

Uamuzi wa Hakimu Mashauri kujiondoa katika kesi hiyo uliibua mashauri mengi ya ama kumpinga yeye binafsi au kupinga amri au uamuzi wake. Licha ya mashauri hayo kufika Mahakama ya Rufani lakini washtakiwa hao hawakuweza kumwondoa katika kusikiliza kesi hiyo.

Tukio kubwa zaidi ambalo bado linakumbukwa katika vichwa vya washtakiwa hao na hata ndugu jamaa na marafiki zao pale linapotajwa jina la Hakimu Mashauri ni la kuwafutia dhamana Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Hakimu Mashauri aliwafutia dhamana Mbowe na Matiko, Novemba 23, 2018, baada ya kukubaliana na maombi na hoja za upande wa mashtaka kufuatia hatua ya washtakiwa hao kusafiri nje ya nchi bila taarifa kwa mahakama na hivyo kushindwa kuhudhuria mahakamani wakati wa kesi yao.

Wanasiasa hao wamepambana kwa kila namna kufuta uamuzi wa Hakimu Mashauri kuwafutia dhamana bila mafanikio na mpaka sasa wako mahabusu katika gereza la Segerea wakisubiri usikilizwaji wa rufaa yao Mahakama ya Rufani kuhusiana na uamuzi huo wa kufutiwa dhamana. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa, Februari 18, mwaka huu.

Jaji Mteule Mkeha

Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Mkeha alikuwa Katibu wa Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB).

Kabla ya kwenda TRAB, Mkeha alikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wakati akiwa mahakamani hapo alisikiliza kesi mbalimbali ikiwamo ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Kesi nyingine ni ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na kesi ya mfanyabiashara maarufu nchini Yusufu Manji.

Katika kesi ya Lissu, aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi na kuidharau mahakama, upande wa mashtaka uliweka pingamizi ili Wakili Peter Kibatala asimtetee kwa madai kuwa ni mmoja wa mashahidi wake.

Hata hivyo Hakimu Mkeha katika uamuzi wake alitupilia mbali pingamizi hilo, akisema kuwa halina msingi na kuamuru Wakili Kibatala aendelee kumtetea mbunge huyo.

Katika kesi ya Gwajima ambaye pamoja na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi zake, Hakimu Mkeha aliitupilia mbali akisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka.

Pia, Hakimu Mkeha alitupilia mbali mashtaka yaliyokuwa yakimkabili Gwajima ya kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Policap Pengo.

Kabla ya kutupilia mbali mashtaka hayo, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo Hakimu Mkeha alikataa maombi ya upande wa mashtaka ya kupokea mkanda wa video (CD), kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka, uliodaiwa kuwa na picha za video zinazomwonyesha Gwajima akimtukana Askofu Pengo.

Majaji wateule wengine.

Majaji wengine walioteuliwa kuwa majaji wa Mahakama Kuu ni Dk. Kilikamajenga na Mtulya, wote kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto; Dk. Masabo, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mongella, Chuo Kikuu Kishiriki Ruaha, Iringa.

Wengine ni Kirati, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Ismail, kutoka Benki Kuu ya Tanzania; Galeba, kutoka kampuni ya uwakili ya ZG Africa Advocates na Masara, kutoka kampuni ya uwakili ya Kings Law Chambers.

Majaji wengine walioteuliwa na Rais Magufuli juzi ni Dunstan Beda Ndunguru, Seif Mwinshehe Kulita, Susan Bernard Mkapa na Upendo Elly Madeha.