Walimu wanaostaafu Moshi watahadharishwa kuepuka matapeli
Meneja wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu Moshi Vijijini (MRT Saccos), Bosco Simba, akizungumza na walimu wanaotarajia kustaafu katika Halmashauri hiyo. Picha na Janeth Joseph.
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja kufuatia kuongezeka kwa matukio ya wastaafu kutapeliwa mara baada ya kupokea mafao yao, hali inayosababisha baadhi yao kupoteza fedha na kuingia katika changamoto za kiuchumi.
Moshi. Walimu wanaotarajia kustaafu mwaka huu katika Halmashauri ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kujiepusha na mitego ya matapeli, huku wakisisitizwa kuwa makini na kutojihusisha na taasisi za kifedha ambazo hazitambuliwi kisheria ili kulinda mafao yao.
Tahadhari hiyo imetolewa leo, Mei 2, 2026, kupitia mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu Moshi Vijijini kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu namna ya kusimamia fedha zao, kutambua mbinu zinazotumiwa na matapeli hao, pamoja na kuchukua tahadhari stahiki wanapopokea mafao yao ya kustaafu.
Akizungumza, Meneja wa MRT Sacoss, Bosco Simba amesema walimu hao wakipewa mafunzo ya mara kwa mara itasaidia kuwaondoa katika wimbi la kutapeliwa ambalo limeongezeka siku za hivi karibuni.
“Tumetoa mafunzo haya kwa sababu kumekuwa na wimbi kubwa sana la watu kutapeliwa. Tukaona ni vyema tuwaandae wanachama wetu ili watambue kuwa sehemu salama ya uwekezaji ni katika Saccos yao waliyoianzisha wenyewe,” amesema Simba.
Baadhi ya walimu wastaafu katika Halmashauri ya Moshi Vijijini wakiwa kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu Moshi Vijijini (MRT Saccos). Picha na Janeth Joseph.
Amesema hadi sasa wanachama wa Sacoss hiyo wamewekeza zaidi ya Sh6 bilioni, huku taasisi hiyo ikiwa imefanikiwa kujenga mtaji wa ndani wa Sh15.9 bilioni unaotumika kutoa huduma kwa wanachama pamoja na kuwekeza katika taasisi nyingine zenye faida.
Aidha, amesema kuwa kwa sasa chama hicho kina mpango wa kujenga kitega uchumi kitakachojumuisha ofisi za chama na hoteli, mradi unaotarajiwa kugharimu Sh2.7 bilioni ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa wanachama hao.
“Tunaamini uwekezaji huu utaifanya Sacoss yetu kuendelea kuwa imara kwa vizazi vijavyo, na mpaka sasa tuna jumla ya wanachama 3,000 tangu tuanze Sacoss hii mwaka 1998 ikiwa na wanachama 98,” amesema Simba.
Akizungumza, mtaalamu wa afya ya akili na ustawi, Dk Paschal Kang'iria amesema maandalizi ya kustaafu yanapaswa kuanza mapema ili kuepusha msongo wa mawazo unaoweza kujitokeza baada ya kuacha kazi.
“Ni muhimu mtu kuanza kujijengea mazoea ya shughuli nyingine kabla ya kustaafu. Hii humsaidia kuendelea kuwa na shughuli za kumuingizia kipato na kupunguza hatari ya changamoto za afya ya akili,” amesema.
Aidha, alisisitiza kuwa mtu anapaswa kuanza mipango ya maisha ya baadaye hata miaka mitano hadi kumi kabla ya kustaafu ili mpito huo uwe mwepesi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi Vijijini, Shedracky Mhagama, amewataka watumishi wa umma kutouogopa mchakato wa kustaafu bali kuuchukulia kama sehemu ya kawaida ya maisha.
“Kustaafu kusitupanikishe; ni hatua muhimu ya maisha. Tunapaswa kujiandaa kisaikolojia na pia kujenga tabia ya kujali afya zetu, kwani uzee huambatana na changamoto mbalimbali za kiafya,” amesema Mhagama.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa watumishi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kuhakikisha wanastaafu wakiwa na afya njema.