Waliohama Chadema na kurejea CCM wakosolewa

Sunday May 02 2021
chadema pc

Waziri Mkuu mwstaafu, Edward Lowassa akisalimiana na wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema alipokuwa akiingia kwenye Ukumbi wa baraza hilo, jijini Mwanza. picha na Maktaba

By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Wakati Lazaro Nyalandu na Seleman Mathew waliokuwa CCM wakahamia Chadema na kisha kurejea chama hicho tawala wakitangazwa juzi katika mkutano mkuu wa CCM mkoani Dodoma, baadhi ya wachambuzi wa siasa wamedai uamuzi wao unatokana na maslahi binafsi na si kwa maslahi ya kitaifa.

Wengine walisema uamuzi wa wanasiasa hao unatokana na kuona kuwa mazingira ya sasa ya shughuli za siasa ni rafiki kwao chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Nyalandu, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati na Mathew (mwenyekiti Kanda ya Kusini) walitangaza uamuzi wao huo juzi, huku wakieleza sababu za kufanya hivyo.

Mbali na wawili hao, baadhi ya waliokuwa makada wa CCM wakajiunga na Chadema na kisha kurejea CCM ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, James Lembeli, Said Nkumba (sasa mkuu wa wilaya Bukombe) na Hamis Mgeja.

Wachambuzi waliozungumza na gazeti hili kwa simu walisema baadhi ya wanasiasa wanahama au kurejea CCM kutokana na maslahi yao binafsi ya kisiasa, hatua inayotokana na mfumo wa vyama uliopo kuruhusu hali hiyo.

“Asilimia kubwa ya wanasiasa wanahama na kuendeshwa kwa masilahi yao binafsi ya siasa, kwa sababu mfumo wa vyama siasa unawapa fursa. Ni vigumu kusema mtu anahama kwa sababu ya masilahi ya Taifa, ingawa wakati wa kuhama wanaotoa sababu ambazo zinakuwa za kuhalalisha,” alisema Dk Richard Mbunda ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Advertisement

Dk Mbunda alisema hivyo ndivyo siasa zilivyo, akifafanua kuwa mchezo wa kuhamahama utaendelea, kwa sababu mazingira yanaruhusu kufanya hivyo na kwamba wananchi watarajie watu wengi kuhama.

Mhadhiri wa mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristomus alisema kurudi kwa wanasiasa hao katika kipindi cha awamu ya Rais Samia, huenda wanasiasa hawakuridhika na utawala wa awamu iliyopita.

Alisema Nyalandu aliamua kuachia nafasi ya ubunge na kuhamia Chadema, kwa sababu alikuwa haridhiki na mtindo wa utawala huo.

“Upande wa Mathew, naye naweza kusema kuwa aliona hakutendewa haki ndani ya CCM ya Magufuli (John) na hata ya Jakaya Kikwete. Ikumbukwe kuwa alihamia Chadema mwaka 2015, baada ya jina lake kukatwa kwenye uchaguzi wa ndani ya CCM wa ubunge.

“Na hata baada ya Magufuli kuwa Rais na Mwenyekiti wa CCM, bado aliona kuwa mazingira ya ndani ya CCM hayakuwa mazuri kurudi. Naona wote wameona sasa hivi Rais Samia anatengeneza mazingira rafiki ya kisiasa ndani ya chama na hata serikalini,’’ alisema.

Alisema hatua hiyo itawafanya kuona CCM kinakuwa chama rafiki kwao kukitumikia, na kwamba huko walikokuwa wanaona mazingira ya kisiasa siyo rafiki kwa miaka ya hivi karibuni hasa baada ya uchaguzi wa 2020.

Wakati wasomi hao wakieleza hayo, mbunge wa zamani wa Longido, Michael Lekule alisema CCM kitaendelea kuwa katika mikono salama chini ya Rais Samia Suluhu, akisema hana shaka naye.

Lekule alisema uzoefu wa muda mrefu aliokuwa nao Rais Samia ndani ya CCM, hautakiwi kutiliwa shaka na kwa vyovyote atakivusha chama hicho hadi mahali kunakohitajika.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema kauli ya Nyalandu ilikuwa na ujumbe maalumu ambao haupaswi kubadilishwa kwa namna nyingine. Alisema kilichosemwa na Nyalandu kinatakiwa kubaki kama kilivyo.

‘‘Kwa kuwa kulikuwa na viongozi wa chama, watakwenda kutafakari,’’ alisema.

Advertisement