Prime
Walioshtakiwa kwa mauaji mtuhumiwa wizi wa blanketi, waachiwa
Muktasari:
- Katika kesi hiyo washtakiwa hao walidaiwa kumuua Herman Ndunguru,aliyetuhumiwa kuiba blanketi ambapo ushahidi wa mashtaka ulidai kundi la watu zaidi ya 10 walimshambulia na kumpiga Herman hadi kufa, wakiwemo washtakiwa hao.
Tanga. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Songea, imewaachia huru Josephine Kapinga na Mathayo Kapinga waliokuwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Herman Ndunguru, ambaye alituhumiwa kuiba blanketi.
Hukumu hiyo imetolewa Julai 14, 2025 na Jaji James Karayemana, huku nakala yake ikiwa imewekwa kwenye tovuti ya Mahakama.
Jaji Karayemana amesema amefikia uamuzi huo baada ya kupitia kwa makini ushahidi wa pande zote mbili na kubaini kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa la mauaji dhidi ya washtakiwa, ikiwemo utambulisho dhaifu wa watuhumiwa katika eneo la tukio.
Josephine na Mathayo walikuwa wakikabiliwa na shtaka la kumuua Herman kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu. Tukio hilo lilidaiwa kutokea Machi 6, 2023 katika Mtaa wa Mji Mwema, Kata ya Masumini, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi tisa: H9339 Koplo Baraka (PW1), Victoria Costantine (PW2), Isaya Conrad Kapinga (PW3, daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu), F.6767 Koplo Yohana (PW4), G.4587 Sajenti Elibariki (PW5), Imani Ndunguru (PW6), Maternus Ndunguru (PW7), January Ndunguru (PW8) na Sintia John (PW9). Pia kulikuwa na vielelezo sita. Jamhuri iliwakilishwa na mawakili wawili, huku washtakiwa wakiwakilishwa na mawakili watatu.
Maelezo ya tukio
Marehemu Herman alikuwa akiishi nyumbani kwa PW2. Mshtakiwa wa kwanza (Josephine) alidai kuwa alikuwa akikumbwa na matukio ya wizi nyumbani kwake.
Januari 2023, PW2 alipoteza bomba lililokutwa kwa PW8 na kubainika kuwa Herman alikuwa amelihifadhi kwa shahidi huyo.
Vilevile ilidaiwa kuwa Herman alipatikana na blanketi ambalo alidai amelipata msituni. Wakati huohuo, Josephine alikuwa amesharipoti kwa PW2 kuhusu kuibiwa blanketi lake.
PW2 alimpigia simu Josephine ambaye alifika kwa usafiri wa pikipiki na kulitambua blanketi hilo kuwa lake. Kisha alibishana na Herman na inadaiwa alianza kumpiga kwa kipande cha kuni kabla ya kupelekwa kituo cha polisi kwa kutumia pikipiki nyingine.
Ushahidi wa upande wa mashtaka ulidai siku hiyo, Josephine alimjulisha PW8 kwamba amemkamata mtu aliyemuibia blanketi.
PW8 alifika na kukuta kundi la watu zaidi ya 10 wakimpiga Herman sehemu mbalimbali za mwili. Miongoni mwa waliomtaja ni Josephine (aliyekuwa na fimbo), Mathayo, Maiko (aliyekuwa na fimbo) na Sele (aliyemtoboa miguu kwa bisibisi). PW8 alidai aliwaeleza Herman si mwizi, wakaacha kumpiga, lakini afya yake ilikuwa mbaya.
Baada ya hapo, PW8 alimjulisha PW6 kuhusu tukio. Waliamua kumpeleka Herman Kituo cha Polisi Mbinga ambako walipatiwa PF3 na kumpeleka hospitali.
“Kabla ya kufika kituoni, Josephine alikuwa ameripoti tukio la wizi na kumpeleka Herman kama mshukiwa,” alidai mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa mashahidi PW5 na PW6, Josephine alimnyooshea kidole Herman kuwa mwizi. Baada ya kufikishwa hospitali, ilibainika Herman alikuwa amefariki dunia kutokana na mshtuko uliosababisha kutokwa damu (kulingana na uchunguzi wa daktari PW3 uliofanyika Machi 7, 2023 mbele ya PW4, PW6 na PW8).
Mshtakiwa wa pili (Mathayo) alikamatwa Septemba 18, 2024.
Utetezi wa washtakiwa
Josephine alikiri kwenda kwa PW2 mara mbili kufuata blanketi lake (kielelezo cha kwanza). Alieleza kuwa walitumia pikipiki mbili zilizotumwa na PW8 kumpeleka Herman kwake. Njiani walishuka kutokana na utelezi na Herman alimvamia. Josephine alidai Julius alichukua fimbo na kuanza kumpiga Herman huku akipiga kelele za “mwizi”.
Josephine alisema alikimbilia polisi kuomba msaada, lakini polisi hawakwenda na baadaye alielezwa kuwa Herman alipigwa vibaya.
Alikiri kumpeleka Herman polisi kama mshukiwa wa wizi lakini alikana kushiriki kumpiga.
Mathayo alijitetea kuwa aliona mkusanyiko wa watu kutoka mbali akiwa njiani kuwarudisha wanafunzi nyumbani na hakukaribia eneo la tukio. Alishangaa kuona akikamatwa miezi mingi baadaye na alikana kuhusika.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Karayemana alisema katika kesi za jinai ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka.
Alieleza kuwa ushahidi wa utambulisho wa watuhumiwa eneo la tukio ulikuwa dhaifu.
Alibainisha kuwa PW8 na PW9 walikuwa mashahidi muhimu waliokuwa karibu na tukio, lakini ushahidi wao haukuwa thabiti katika kuwatambua washtakiwa kati ya kundi la watu zaidi ya 10.
Jaji alisema hakuna ushahidi wa kuaminika uliothibitisha kuwa Mathayo alihusika na mashahidi walitoa ushahidi wenye mashaka kuhusu nani hasa aliyemuua Herman.
Alihitimisha kwa kusema: “Kwa kumalizia, shtaka dhidi ya washtakiwa halijathibitishwa bila kuacha shaka. Ninawaona hawana hatia na ninawafutia shtaka la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu na kuwaachia huru.”