Wamiliki jengo lililoporomoka Kariakoo kizimbani

Mshtakiwa Ashour Ashour (wa kwanza kushoto), Zenabu Islam (katikati) na Leondela Mdete wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya kuua bila kukusudia na kusababisha vifo vya watu 31. Picha na Hadija Jumanne.
Muktasari:
- Wanakabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia wanayodaiwa kutenda Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo wilayani Ilala.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia.
Washtakiwa hao wanaodaiwa kuwa wamiliki wa jengo lililoporomoka katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo na kusababisha vifo vya watu hao, wamefikishwa mahakamani hapo leo, Ijumaa Novemba 29, 2024 na kusomewa kesi ya mauaji ya kuua bila kukusudia.
Washtakiwa hao ambao ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38).

Washtakiwa wamesomewa mashtaka na jopo la mawakili watatu waandamizi wa Serikali, Adolf Lema, Grace Mwanga na Erick Kamala, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini.
Kabla ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mhini amewaeleza hawatakiwi kujibu chochote, kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu Mhini baada ya kutoa maelezo hayo, wakili Kamala aliwasomea mashtaka hayo PI namba 33633/2024.
Wakili Lema alidai washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume cha kifungu 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Amedai shtaka la kwanza hadi la 31 ni kuua bila kukusudia kinyume cha vifungu hivyo vya sheria.
Wakili Kamala amedai katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.

Katika shtaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao siku na eneo hilo wanadaiwa kusabisha vifo vya Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.
Pia wanadaiwa kusababisha vifo vya Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.
Wakili Kamala amedai kuwa katika siku na eneo hilo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusabisha kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.
Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka waliomba wapatiwe dhamana kwa masharti nafuu kupitia kifungu 148 (1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Upande wa mashtaka ulidai hauna pingamizi dhidi ya dhamana na kwamba wanaomba wapewe masharti magumu.
Hakimu Mhini alitoa masharti matatu ya dhamana ambayo, kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa.
Pili, wadhamini hao wanatakiwa kusaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.
Tatu, wadhamini hao wanatakiwa wawe wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Mshtakiwa wa kwanza amekamilisha masharti na kupata dhamana, huku mshtakiwa wa pili Zenabu na watatu Ashour wakishindwa kuyatimiza.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 12, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wawili wamepelekwa rumande.