Wanafunzi 24 Ilemela wakatisha masomo baada ya kupata mimba

Friday March 05 2021
New Content Item (2)
By Mgongo Kaitira

Mwanza. Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza zinaeleza kuwa mwaka 2020 wanafunzi 24 wa shule za sekondari wilayani Ilemela wameacha shule baada ya kupata mimba.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa kitengo cha upelelezi wilayani humo, Shamira Mkomo amesema ili kukabiliana na mimba za utotoni na ulaghai wa wanafunzi ambao ni chanzo cha mimba, polisi wameanza kampeni  ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi juu ya madhara ya mimba za utotoni na dawa za kulevya.

"Tumeanza na shule ya sekondari ya Kangae na  Nyamanoro, lengo ni kuwakumbusha wajikite kwenye masomo na kuachana na vitendo vitakavyowafanya wakatishe masomo yao," amesema Mkomo.

Amesisitiza, “tumewaasa sana wanafunzi waachane na lifti za bodaboda kwani katika kesi ambazo zinaripotiwa katika vituo vyetu wahalifu wakubwa wa mimba za wanafunzi ni madereva boda boda.”

Mwalimu mkuu wa sekondari ya Nyamanoro, Antonia Nkaka amewashauri wazazi kutenga muda kwa ajili watoto wao ili kuzungumza kuhusu changamoto wanazokutana nazo.

"Kwa watoto ambao wamekuwa waathirika wa vitendo hivi baada ya kuwauliza na kuwashauri tumebaini kwamba wazazi pia ni chanzo kwa sababu hawatengi muda wa kutosha kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo watoto wao," amesema.

Advertisement

Naye Mwanafunzi wa Sekondari ya Nyamanoro, Loveness Lucas amesema elimu hiyo itamsaidia kukwepa vishawishi ikiwemo kuomba lifti kwa madereva pikipiki ili aweze kutimiza ndoto yake kielimu.

Advertisement