Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi 500 wanaodai kutapeliwa wafukuzwa

Wanafunzi 500 wanaodai kutapeliwa wafukuzwa

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai ametoa siku saba kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu zaidi ya 500, wanaodaiwa kutapeliwa ajira na Kampuni ya Alliance Motion in Global, mjini Moshi kuondoka mkoani humo na kurudi makwao.


Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai ametoa siku saba kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu zaidi ya 500, wanaodaiwa kutapeliwa ajira na Kampuni ya Alliance Motion in Global, mjini Moshi kuondoka mkoani humo na kurudi makwao.

Kagaigai alisema wanafunzi watakaokiuka agizo hilo, watahesabika ni wahalifu na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia alimuagiza Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro kufuatilia mtandao wote uliohusika na utapeli huo ikiwa ni pamoja na kuwaita na kuwahoji viongozi wake na watuhumiwa wafikishwe mahakamani haraka.

Wanafunzi hao kutoka mikoa ya Mara, Tabora, Singida, Mbeya, Shinyanga, Kigoma na Tanga, wanadaiwa kutapeliwa kupata ajira katika kampuni hiyo na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Joseph.

Wanadai kutozwa Sh200,000 hadi Sh900,000 na kuahidiwa kupewa ajira.

Kwa sasa wamepangishiwa vyumba katika Kata ya Majengo na Njoro mjini Moshi, na chumba kimoja hukaa zaidi ya wanne, huku wakidai kuishi mazingira magumu na hawana chakula.

Akizungumza jana na baadhi ya wanafunzi hao na viongozi wa Serikali za mitaa katika ukumbi wa mikutano katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mkuu huyo wa Mkoa alisema tukio hilo ni la hatari na kumuagiza kamanda wa polisi kuwasiliana na makamanda wa mikoa mingine kufuatilia mtandao huo.

“Ninyi mlikuwa mnashughulika na wezi na mmetapeliwa, poleni sana vijana, hakuna utaratibu wa mtu kuomba kazi na kuambiwa atume fedha kwanza,” alisema Kagaigai.

Aliwataka wenyeviti wa mitaa na watendaji wa Serikali, kurudi kwenye utaratibu wa zamani wa kuwahoji wageni wanaoonekana katika maeneo yao, ili kudhibiti matatizo kama hayo.


Wanafunzi wafunguka

Stephano Chacha, anayetoa Mkoa wa Mara alisema wanaishi mazingira magumu, hawana hata chakula pamoja na nauli za kurudi makwao, huku akieleza kuwa hali hiyo inawaumiza zaidi watoto wa kike.

“Tuko mtaani zaidi ya vijana 500, tuliokuja kwa mkuu wa wilaya leo ni wale jasiri ambao tumeona tuje Serikali itusaidie, ila kuna watu wengi na wasichana wapo zaidi ya 200, hatuna chakula na kuna wagonjwa ambao wamekosa matibabu. wameambiwa wavumilie.

“Na mbaya zaidi bado wanaendelea na huo mchezo wa kupigia watu simu na kwa sasa wanawapeleka mikoa mingine ya Arusha, Manyara, Mbeya na Morogoro ambako wameanzisha matawi mengine. Serikali iangalie hili na kushughulikia kampuni hiyo ili kuzuia vijana wengine kutapeliwa,” alisema.

Kijana huyo alieleza walimpigia simu mzazi wake wakamwambia amefaulu, hivyo zinahitajika Sh600,000, ambazo walidai ni za kununua kompyuta, mavazi ya ofisini, viatu na vifaa vingine na kwamba mzazi wake alituma fedha hizo. Aron Paul kutoka Tabora, alisema aliambiwa kuna fursa za kazi katika kampuni inayojishughulisha na mambo ya afya na alitakiwa kwenda na Sh250,000 na nauli pembeni, lakini alipofika alifundishwa kitu tofauti.

“Kwa kuwa kwenye fomu tunajaza namba za wazazi wetu, bada ya muda walimpigia simu mzee wangu atume pesa, alilazimika kuuza shamba la hekari tatu ili kupata Sh600,000 akiamini nimepata kazi,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema wanaendelea kuwashikilia watu sita na msako unaendelea kumtafuta mmiliki wa kampuni hiyo.

“Yapo madai kuwa watu hawa baada ya kubanwa Kilimanjaro, wamekimbilia Singida, Mbeya na mikoa mingine, niombe makamanda wenzangu, tusaidiane na kupeana taarifa za kundi hili linalotapeli watu kwa mgongo wa kuwapa ajira,” alisema.