Wananchi 854 kulipwa Sh50 bilioni kupishwa uchimbaji dhahabu

Muktasari:
Zaidi ya wakazi 854 wa vijiji vya Sotta na Nyabila Kata ya Igalula Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wanatarajiwa kulipwa fidia ya Sh50 bilioni ili kupisha shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika mgodi wa Nyanzaga unaomilikiwa kwa ubia Kati ya Serikali na Kampuni ya Ore Corp Limited.
Sengerema. Zaidi ya wakazi 854 wa vijiji vya Sotta na Nyabila Kata ya Igalula Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wanatarajiwa kulipwa fidia ya Sh50 bilioni ili kupisha shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika mgodi wa Nyanzaga unaomilikiwa kwa ubia Kati ya Serikali na Kampuni ya Ore Corp Limited.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 4, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla kwenye hafla ya kukabidhi mfano wa hundi ya zaidi ya Sh3.7 bilioni, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi fedha hizo zimelipwa kwa walengwa ikiwa ni muendelezo wa ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha eneo hilo.
Amesema wakazi 152 sawa na asilimia 17.8 ya ambao hawajasaini mikataba ya fidia wanapaswa kufanya hivyo na kujiandaa kupisha kwenye maeneo, hata wanaojengewa nyumba kufanya hivyo mara tu watakapopata nyumba zao akidai Serikali ipo bega kwa bega kusimamia haki za wananchi na mwekezaji kwa manufaa ya Taifa.
Makilagi amesema hatua iliyofikiwa ya ulipaji fidia kwa wananchi ni ishara njema ya kuanza rasmi kwa shughuli za uchimbaji kwenye eneo hilo huku akitoa wito kwa wananchi wa Sengerema kujiandaa na fursa za kiuchumi kama ajira na kufanya biashara kutokana na uwepo wa mgodi huo uliowekeza zaidi ya Sh1 trilioni.t
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi imara uliopelekea ongezeko la Pato la Taifa kwenye sekta ya madini hadi kufikia asilimia 10 kutokana na makusanyo, usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ya kimkakati ambayo inaleta si tu uboreshaji wa huduma za jamii bali ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hata hivyo, ametoa wito kwa kampuni hiyo na makampuni mengine madogo yaliyoingia mkataba na kampuni mama kuhakikisha wanatekeleza vema sheria ya kurejesha faida kwa jamii inayozunguka na ushuru wa huduma kwa kulipa kodi zote stahiki kwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na ile ya halmashauri.
“Kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kumekua na mabadiliko ya tabia nchi hivyo natoa wito kutochafua vyanzo vya maji na kuhakikisha mnatunza mazingira na kuhakikisha mnalilinda ziwa letu na mjiepushe na ukataji wa miti ili kuepusha athari za kimazingira na wananchi naomba tujenge tabia ya kupanda miti,”amesema
Akizungumzia utekeleaji wa mpango wa uhamishaji watu na makazi, msimamizi wa miradi ya kampuni hiyo nchini, Isaac Lupokela amesema hadi Septemba 2, 2023 wananchi 701 wanaopaswa kulipwa fidia wameshapata ufafanuzi wa stahiki zao na wamekwisha saini mikataba akidai mikataba 190 imekamilika, walengwa wameishaichukua na uelimishaji unaendelea.
Amefafanua kuwa leseni namba 653 ya mwaka 2021 iliwapa kampuni hiyo eneo lenye ukubwa wa hekta za mraba 23. 4 na kwamba kwakua kulikua na kaya zinazoishi ndani ya eneo hilo walipashwa kufanya uthaminishaji ili kulipa fidia stahiki kabla ya kutwaa ardhi hiyo kwa mujibu wa sheria jambo ambalo linafika mwisho siku za usoni.