Wananchi Siha walia kufunguliwa kituo cha afya

Izack Laizer Mkazi wa Kijiji mkombozi wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, akiomba kituo hicho kufunguliwa na kuanza kutoa huduma.

Siha. Wananchi wa Kata ya Orkolili wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kufungua kituo cha Afya kilichopo kwenye kata hiyo ili   kuwaepusha kutumia gharama kubwa kufuata huduma hiyo hospitali ya wilaya hiyo.

Wananchi hao wametoa ombi hilo wakati wa ziara ya katibu wa chama cha mapinduzi (CCM),wilayani humo Ally Kidunda kutembelea miradi na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi. 

Wakizungumza mara baada ya katibu huyo kutembelea kituo hicho cha Afya kilichopo Kijiji cha mkombozi, wameombwa kituo hicho kufunguliwa mapema ili waanze  kufurahia kupata  huduma karibu na kuepuka kutumia gharama kubwa 

"Shukrani ni kitu cha kiungwana Tunamshukuru Rais Samia SuluhuuHassan, Mbunge wetu Godwin Mollel na Diwani wa kata yetu, Jonathan Nasari kwa ujenzi wa kituo hiki karibu tulikuwa tunatumia fedha nyingi kufuata huduma ya Afya hospitali ya wilaya hiyo au kwenda hospitali ya wilaya jirani ya Hai " wamesema wananchi hao

Agnes Aminiel amesema wamekuwa wakiteseka kufuata huduma hiyo Kwenda hospitali ya wilaya hii tunapokuwa na mgonjwa au mjamzito gharama shilingi 15,000 au sh 20000 kwa kutumia badoboda hiyo ni kwenda tu wakati mwingine wakina mama wanajifungulia njia kitu ambacho sio kizuri

"Kwa sasa kituo tunaona ujenzi umekamilika ,tunaomba mkifungue ili  kianze kufanya kazi ya kutoa huduma  ili kutuepusha kufuata huduma hiyo mbali"amesema Agnes

Pia Izack Laizer Mkazi wa Kijiji cha mkombozi amesema kufunguliwa kwa kituo hicho kwa haraka kitawasaidia hata wazee kupata matibabu wakati mwingine  hawana hela na kusabisha kuendelea kuteseka na ugonjwa

"Mimi mwenyewe hapa unaponiona nasumbuliwa na mguu na hapa sina fedha za kuchukua usafiri  kwenda hospitali "amesema Laizer

Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Paschal Mbota, amesema kituo hicho kitaanza wakati wowote baadhi ya vifaa vimeshafika bado vitu vidogo vidogo, tunatarajia Septemba mwaka huu huduma ikaanza.