Wananchi wa mijini, vijijini wajumuishwa huduma za kifedha

Muktasari:
- Katika kipindi miaka 20, shirika la FSDT limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba wananchi wanafikiwa na huduma za kifedha kwa njia tofauti ikiwemo kwa miamala ya simu.
Dar es Salaam. Shirika la Financial Sector Deepening Trust (FSDT) limefanikiwa kuwawezesha kiuchumi Watanzania wengi hasa waishio vijijini, katika kipindi cha miaka 20 tangu lilipoanzishwa kwa lengo la kuchochea ujumuishi wa kifedha hapa nchini.
Katika kipindi hicho, shirika hilo limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba wananchi wanafikiwa na huduma za kifedha kwa njia tofauti ikiwemo kwa miamala ya simu.
Hayo yamebainishwa kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 20 ya kuanzishwa taasisi hiyo ya kifedha, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, jumuiya za kimataifa na wadau katika sekta ya fedha.
Akizungumza kwenye hafla hiyo ya FSDT, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Sauda Msemo ametaja juhudi za taasisi hiyo katika kuibadilisha sekta ya kifedha kwa kuongeza ujumuishi wa wananchi.
“Unapozungumzia mchango wa shirika hili, utagusia namna ilivyobadilisha mwelekeo na limeleta suluhisho la haraka, kuwezesha viongozi kufanya uamuzi wa kisera na pia kuwezesha huduma za kifedha kujibu mahitaji ya Watanzania,” amesema.
Msemo amesema juhudi za shirika hilo katika kufanya utafiti, kama vile ule wa National Demand-Side Survey, zimekuwa na mchango mkubwa katika kutoa taarifa za msingi zinazosaidia katika kutunga sera za ujumuishi na kubuni bidhaa za kifedha za kisasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FSDT, Eric Massinda amekumbuka mchango wa marehemu Lawrence Mafuru huku akieleza nafasi yake katika kukuza ujumuishi wa kifedha.
“Maono ya Mafuru yamekuwa chachu kwa sekta ya fedha hapa nchini na mchango wake katika utungaji wa sera zinazotokana na umahiri wake, yanabaki kuwa nguzo muhimu katika dhamira ya shirika hili,” amesema Massinda.
Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dk Charles Mwamwaja amesisitiza mafanikio ya kisera yaliyowezeshwa na shirika hilo.
“Sera ni muhimu katika kuhakikisha mazingira bora kwa sekta ya fedha kufanya kazi, kustawi na kudumu. Mchango wa shirika hili, ikiwa ni pamoja na National Financial Inclusion Framework na mkakati wa ufadhili wa wajasiriamali (SME Financing Strategy), imeweka msingi wa mazingira ya kifedha ya ujumuishwaji zaidi,” amesema.
Pia, Dk Mwamwaja amesema ushirikiano unaoendelea wa FSDT katika kuandaa sheria na mikakati mingine ya ujumuishi wa kifedha, ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kifedha.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la DANIDA, Lise Sorensen amesema ushirikiano wa kudumu kati ya nchi yake na shirika hilo umekuwa wa wakati wote kwa kuwa wanadhamira moja ya kuwaletea wananchi maendeleo.
“Misingi imewekwa, miundombinu ya masoko, upatikanaji wa fedha na sera bora ni muhimu kwa ushirikiano huu ili ulete mabadiliko katika maisha ya kila siku ya Watanzania,” amesema.
Sorensen ameipongeza FSDT kwa ubunifu wake katika kutafuta suluhisho, kama vile bima ndogo (micro-insurence) na miamala kwa njia ya simu. Ameongeza kuwa jukumu lake muhimu katika kuwezesha Watanzania zaidi ya milioni 38 kupata vitambulisho vya taifa.
“Kadri Tanzania inavyoendelea kuongeza ushawishi wake kisiasa na kiuchumi, juhudi za shirika hilo zinabaki kuwa muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya nchi,” ameeleza.
Amesema lengo la shirika hilo ni ubunifu, ushirikiano na utungaji wa sera zinazotokana na ushahidi limebadilisha sekta ya kifedha, kuhakikisha Watanzania wengi wanapata huduma zinazoboreshwa maisha yao.