Wananchi waonywa kutoa taarifa binafsi kwa taasisi zisizosajiliwa
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dk Emmanuel Mkilia, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Ijumaa Juni 12, 2026.
Muktasari:
- Tahadhari hiyo inalenga kuimarisha usalama wa taarifa za faragha na binafsi ili kuwalinda wananchi dhidi ya matumizi yasiofaa.
Dodoma. Wananchi nchini wametakiwa kuwa waangalifu wanapotoa taarifa zao binafsi kwa taasisi mbalimbali, huku wakihimizwa kuhakikisha kuwa taasisi hizo zimesajiliwa rasmi na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ili kulinda haki yao ya faragha na usalama wa taarifa zao.
Onyo hilo limetolewa leo Juni 12, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dk Emmanuel Mkilia, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Dk Mkilia amesema bado kuna baadhi ya taasisi, ikiwemo za sekta nyeti kama afya na elimu, ambazo zinaendelea kukusanya na kuchakata taarifa binafsi za wananchi bila kukamilisha usajili unaotakiwa na sheria, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama na faragha ya wananchi.
Amesema wananchi wana haki ya kujua taasisi inayokusanya taarifa zao na kuhakikisha kuwa imepewa kibali cha kufanya kazi hiyo kabla ya kutoa taarifa muhimu zinazohusu maisha yao binafsi.
"Tume inawakumbusha wananchi kuwa wanayo haki ya kulinda taarifa zao binafsi. Wanapaswa kuepuka kutoa taarifa hizo kwa taasisi ambazo hazina kibali cha kuzikusanya na kuzichakata kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi," amesema Dk Mkilia.
Aidha, amewahimiza wananchi kuwasilisha malalamiko kwa tume hiyo pindi wanapohisi taarifa zao zimetumika vibaya au zimekusanywa kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa Dk Mkilia, baadhi ya taarifa ambazo zinahitaji ulinzi mkubwa ni pamoja na taarifa za kifedha, rekodi za afya, taarifa za ndoa na familia pamoja na taarifa nyingine za siri ambazo zinaweza kusababisha madhara makubwa zikivuja au kutumiwa vibaya.
Amesema matumizi yasiyo sahihi ya taarifa hizo yanaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo wizi wa utambulisho, unyanyasaji wa kidijitali, hasara za kifedha na kupungua kwa imani ya wananchi kwa taasisi zinazotoa huduma.
"Taarifa binafsi ni mali muhimu ya mwananchi. Zinapotumiwa kinyume cha sheria au kwa madhumuni yasiyokusudiwa, zinaweza kuathiri usalama wa mtu mmoja mmoja na hata ustawi wa jamii kwa ujumla," amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Mkilia ameeleza kuwa taasisi zote zilizosajiliwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi hupewa cheti rasmi cha usajili kinachothibitisha mamlaka yao ya kukusanya na kuchakata taarifa za wananchi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuhakikisha wanaomba kuona uthibitisho huo kabla ya kutoa taarifa zao binafsi kwa taasisi yoyote.
"Wananchi wana haki ya kujiridhisha kuwa taasisi wanazoshirikiana nazo zimeidhinishwa kufanya kazi hiyo. Cheti cha usajili ni moja ya vielelezo muhimu vinavyopaswa kuonekana wazi," amesema.
Sambamba na hilo, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi imetoa siku saba kwa taasisi ambazo tayari zimeanza mchakato wa kujisajili lakini hazijaukamilisha kuhakikisha zinamaliza taratibu zote zinazohitajika.
Pia, taasisi ambazo bado hazijaanza kabisa mchakato wa usajili zimetakiwa kufanya hivyo mara moja kuanzia leo ili kuendana na matakwa ya sheria.
Dk Mkilia ameonya kuwa taasisi zitakazobainika kuendelea kukusanya au kuchakata taarifa binafsi bila usajili rasmi zitakabiliwa na hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kutozwa faini au kuchukuliwa hatua za kiutawala kwa mujibu wa sheria.
Mbali na usajili, amezitaka taasisi zote zilizokwishasajiliwa kuhakikisha zinaweka sera madhubuti za ulinzi wa taarifa binafsi, mifumo salama ya kuhifadhi taarifa pamoja na taratibu za kuzuia taarifa hizo kuvuja au kutumiwa vibaya.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, unaenda sambamba na maendeleo ya teknolojia na ongezeko la matumizi ya mifumo ya kidijitali nchini.
Dk Mkilia amesisitiza kuwa ulinzi wa taarifa binafsi si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila taasisi na mwananchi kuhakikisha taarifa hizo zinatunzwa kwa usalama na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
"Kadiri matumizi ya teknolojia yanavyoongezeka, ndivyo umuhimu wa kulinda taarifa binafsi unavyoongezeka. Tunahitaji kujenga utamaduni wa kuheshimu na kulinda faragha za wananchi katika mazingira yote ya utoaji huduma," amesema.