Wanaodaiwa kuiibia Vita Foam, waomba majadiliano na DPP
Muktasari:
- Wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Machi 1, 2023 na Oktoba 31, 2024 jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Jamhuri katika kesi ya wizi inayowakabili wafanyakazi tisa wa kampuni ya Vita Foam (T) Limited, wameieleza Mahakama kuwa wanaendelea na majadiliano na washtakiwa hao ili kuimaliza kesi hiyo.
Washtakiwa ni Herington Sakaya (29), mhasibu na mkazi wa Kigamboni; Buheri Komba(36)ofisa mauzo na mkazi wa Temeke; Hemed Ramadhani(33)ofisa mauzo na mkazi wa Sabasaba Mbagala; Bilal Mtemelo (28) ofisa masoko na mkazi wa Mtoni kwa Aziz Ally na Said Bakari (32), ofisa masoko na mkazi wa Kigamboni.
Wengine ni ofisa mauzo, Simon Magee (37)mkazi wa Mbagala na Nusra Kibuda(26)mkazi wa Kijichi; Salome Sanga(35) mhasibu na mkazi wa Igawilo mkoani Mbeya na Said Hamis Said (27)ofisa mauzo na mkazi wa Kigamboni.
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka tisa yakiwemo ya kutakatisha fedha na wizi ya Sh1.478 bilioni mali ya kampuni hiyo.
Wakili wa Serikali, Pancras Protas ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Julai 8, 2026 wakati kesi hiyo ilipotajwa.
"Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wapo mbele ya Mahakama yako na upande wa Jamhuri bado tunaendelea na vikao vya kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hii, hivyo tunaomba Mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Protas, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.
Hakimu Mwankuga alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha hadi Julai 20, 2026 kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka la kutakatisha fedha linalowakabili, halina dhamana.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Januari 16, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 957 ya mwaka 2026 yenye mashtaka tisa yakiwemo ya wizi na kutakatisha fedha.
Shtaka la kwanza ni la wizi wakiwa wafanyakazi wa kampuni ya Vita Foam (T) Limited linalomkabili Sakaya, Ramadhani, Magee, Kibuda na Saidi.
Amedai washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 1, 2023 na Oktoba 31, 2024 katika jiji la Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa kampuni ya kampuni ya Vita Foam (T) Limited, wanadaiwa kuiba Sh324 milioni, mali ya mwajiri wao.
Shtaka pili ni kutakatisha fedha, linalomkabili Sakaya, Ramadhani, Magee, Kibuda na Saidi, ambapo siku na eneo hilo, washtakiwa walijipatia fedha hizo wakati wakijua, fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la wizi.
Pia, Sayaka, Bakari, Magee, Kibuda na Said, ambapo katika kipindi hicho siku na eneo hilo, wanadaiwa kuiba Sh321.6 milioni mali ya mwajiri wao na shtaka la nne washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha.
Shtaka la tano ni la wizi na linamkabili Sakaya, Mtemelo, Magee, Kibuda na Saidi, ambapo siku na eneo hilo, waliiba Sh241.5 milioni mali ya mwajiri wao, huku shtaka la sita ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha linalokabili washtakiwa hao watano.
Mashtaka mengine ni wizi na linawakabili Sakaya, Komba, Magee, Kibuda na Said, ambapo katika kipindi hicho, wanadaiwa kuiba Sh557.9 milioni mali ya mwajiri wao na pia wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha, wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi.
Vilevile, shtaka la tisa ni la wizi linamkabili Sakaya, Magee, Kibuda, Sanga na Said, ambapo katika kipindi hicho ndani ya jiji la Dar es salaam, wanadaiwa kuiba Sh32.7 milioni mali ya mwajiri wao.