Wanaopisha Dart Dar wadai bilioni saba

Muktasari:

Serikali imesema inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia hiyo kwa wananchi 90 wanaodai Sh7.87 bilioni ili kupisha Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dart).

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi 90 wanaodai Sh7.87 bilioni ili kupisha Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dart).

 Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde ameyasema hayo leo Alhamis Septemba 22, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo.

Profesa Mkumbo alihoji nini hatma ya wananchi wa Ubungo Kisiwani waliofanyiwa tathimini ya kulipwa fidia ili wapishe ujenzi wa DART.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema eneo la makazi ya watu la Ubungo Kisiwani lilifanyiwa uthamini na kuandaa jedwali la uthamini lililothibitishwa na kusainiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali Aprili 2022 lenye jumla ya Sh7.87 bilioni zitakazolipwa kwa wananchi 90 wa eneo hilo watakaopisha ujenzi wa Karakana hiyo.

“Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia hiyo kwa wananchi 90 na mara zinakapopatikana malipo hayo yatafanyika,” amesema.