Wanaotumia magari ya Land Rover wamuenzi Mwalimu Nyerere

Muktasari:

  • Katika kuadhimisha kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Umoja wa wenye Magari aina ya Land Rover kutoka mikoa yote nchini, wametumia magari aina hiyo kutembea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere iliyopo mkoani Morogoro.


Morogoro. Katika kuadhimisha kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Umoja wa wenye Magari aina ya Land Rover kutoka mikoa yote nchini, wametumia magari aina hiyo kutembea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere iliyopo mkoani Morogoro.

Akizungumza jana Oktoba 13 katika lango kuu la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Nyerere mkoani hapa, mratibu wa Umoja huo, Meja Mbuya amesema kuwa Hayati Nyerere kwa muda mrefu alitumia usafiri huo aina ya landrover.

Mbuya amesema katika kumwenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo, wameamua kuhamasisha Watanzania kufanya utalii wa ndani kwa kutembea hifadhi, wakianzia hifadhi ya Mikumi na sasa wanaendelea na hifadhi ya Nyerere.


Ofisa uhifadhi mwandamizi wa hifadhi hiyo iliyo chini ya Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa), Seth  Mihayo, amesema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 30,893 imekuwa ikipokea wageni wa ndani na nje ya nchi, kutokana na kusheheni bionuai za kipekee ukilinganisha na hifadhi nyingine.

Mihayo alitaja baadhi ya vivutio kuwa ni munganiko wa vitu mbalimbali ikiwemo uoto wa kipekee wa asili, mito, mabwawa, miinuko na mabonde yanayofanya makazi ya viumbe wakiwemo wanyama ndege, wadudu, reptilia na amfibia.

Ametaja pia mti wa ajabu wa asili ambao ulikuwa ukitumiwa kufanya matambiko na jamii kwaajili ya utatuzi masuala mbalimbali.

Pia amesema kumekuwa na vivutio na maeneo ya kihistoria ambayo ni pamoja na kumbukumbu ya vita vya majimaji ambapo Mtemi Kinjekitile Ngwale aliyechukua maji kwenye moja ya mito iliyopo hifadhini hapo.

Katika Maadhimisho hayo mmoja wa wanafunzi kutoka shule ya msingi Mloka iliyopo wilayani Rufiji Mkoani Pwani, Mustakimu Kingwande aliyetembelea hifadhi hiyo alisema amefika katika hifadhi hiyo kwaajili ya kujifunza, kumuhenzi baba wa Taifa na kuona vivutio vya wanyama na makazi yao.