Wanawake 2,519 Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wachunguzwa saratani
Baadhi ya wanawake wa eneo la Oldonyosambu, Halmashauri ya Arusha, leo Jumamosi Mei 9, 2026 wakiwa wanasubiri kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti. Zoezi hilo linafanywa na Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan Afrika Mashariki nchini Kenya na Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya afya.
Muktasari:
- Wanawake hao kutoka Kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, wamefanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi,huku , huku wataalamu wa afya wakieleza kuwa huduma za uchunguzi wa mapema zinaendelea kusaidia kubaini viashiria vya ugonjwa huo kabla haujafikia hatua hatarishi.
Arusha. Zaidi ya wanawake 2,500 kutoka maeneo ya pembezoni mwa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wamenufaika na matibabu bure na uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi huku wataalamu wa afya wakisisitiza elimu zaidi inahitajika ili kuongeza mwitikio wa wanawake kujitokeza kupima.
Wanawake hao wamefikiwa kuanzia Mei 4, 2026 katika kampeni ya uchunguzi huo kupitia mradi mtambuka wa kupambana na saratani za wanawake Afrika Mashariki.
Mradi huo wa kikanda unatekelezwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan Afrika Mashariki nchini Kenya na Tanzania, Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan, Chuo Kikuu cha Aga Khan pamoja na Taasisi ya Utafiti ya Curie ya nchini Ufaransa chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Gates Foundation na Mtandao wa Mashirika ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN).
Akizungumza leo Jumamosi Mei 9, 2026 kuhusu utekelezaji wa kampeni hiyo katika Halmashauri ya Arusha, mratibu wa mradi huo, Dk Sarah Maongezi amesema hadi kufikia siku ya nne ya shughuli hiyo walikuwa wamevuka lengo la kuwafikia wanawake 2,200 baada ya kufanikiwa kuwafikia wanawake 2,519.
Amesema kati ya wanawake hao, wanawake 329 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa kina, huku zaidi ya wanawake 15 wakibainika kuwa na mabadiliko katika matiti yaliyohitaji ufuatiliaji zaidi wa kitabibu.
“Hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa ni saratani, lakini wanawake hao wamepewa rufaa kwenda katika hospitali za serikali ikiwemo Hospitali ya Mount Meru na KCMC kwa uchunguzi zaidi,” amesema Dk Sarah.
Kwa upande wa saratani ya mlango wa kizazi, amesema wanawake watano walikutwa na viashiria vya awali vya ugonjwa huo ambapo baadhi yao walipatiwa matibabu kupitia kliniki tembezi zilizokuwa zikitembelea maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.
Ameongeza kuwa wanawake watatu waligundulika kuwa na saratani na kupewa rufaa ya kwenda kupata matibabu zaidi katika hospitali za serikali.
Dk Sarah amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto kubwa ya uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa saratani.
“Bado elimu inahitajika sana. Kuna maeneo tunafika na kukuta wahamasishaji tayari wamepita kutoa elimu lakini wanawake wengi hawajitokezi. Tunatamani kuona wanawake wengi zaidi wakifika kwa ajili ya uchunguzi,” amesema.
Amesema wakimaliza leo kufanya uchunguzi huo,watakuwa wamewajengea uwezo wauguzi na watoa huduma wa Mkoa wa Arusha ili huduma hizo ziendelee hata baada ya mradi huo kuondoka.
“Tunalenga kuacha mfumo endelevu ambao utaendelea kusaidia wanawake hata baada ya sisi kuondoka,” ameongeza.
Dk Sarah amesema pia wanatoa elimu na upimaji wa saratani ya matiti kwa wanafunzi wa Shule za Sekondarii li kuwajengea uwezo wa namna ya kujichunguza na kupeleka elimu hiyo kwa wazazi na walezi wao nyumbani.
“Tunaendelea kupambana kutoa elimu hasa kwa jamii hizi za pembezoni kutokana na wengi kushindwa kupata huduma za afya na taarifa sahihi kuhusu saratani kwani wengi wao kutokana na changamoto kuanzia za kimazingira wanashindwa kupata taarifa sahihi,”amesema
Awali, muuguzi na msimamizi wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto katika Halmashauri ya Arusha, Butolwa Bujiku, amesema upimaji huo umekuwa msaada mkubwa katika kuwafikia wananchi moja kwa moja kwenye maeneo yao.
Amesema saratani nyingi hugundulika katika hatua za mwisho kutokana na kukosekana kwa dalili za wazi katika hatua za mwanzo.
“Kazi yetu ni kuwabaini wananchi mapema kabla ugonjwa haujafikia hatua mbaya. Wanapogundulika na viashiria vya awali tunawatibu mapema,” amesema.
Butolwa amesema timu hizo zimekuwa zikifika katika masoko, shule za sekondari na maeneo mbalimbali ya vijijini ili kutoa huduma na elimu kwa wananchi na kutaja baadhi ya maeneo yaliyofikiwa kuwa ni Bangata, Oljoro, Musa, Oldonyosambu, Sambasha, Lokii pamoja na Soko la Ngaramtoni.
Kwa upande wa shule za sekondari, amesema timu hiyo imefika katika shule za Bangata, Nduruma, Olturmet, Ilkiding’a na Sambasha huku lengo likiwa kufikia shule 10.
“Wanawake wengi hawana mazoea ya kwenda hospitali mpaka waumwe. Ndiyo maana tumeamua kuwafuata moja kwa moja kwenye jamii zao,kwani tunaona pia mbali na matangazo kutolewa kwenye baadhi ya maeneo mwitikio ni mdogo,” amesema.
Ameongeza kuwa katika Halmashauri ya Arusha kuna vituo 70 vinavyotoa huduma ya afya ya uzazi na mtoto ambapo vituo 41 vina uwezo wa kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
Mkazi wa Sanawari, Neema Mollel, aliyefanyiwa uchunguzi huo amesema wanawake wengi wanapaswa kuondoa hofu kuhusu vipimo vya saratani.
“Nimefanya vipimo na nimekutwa niko salama. Wanawake wasiogope kupima kwa sababu vipimo havina maumivu na vinasaidia kujua afya yako mapema,” amesema.
Neema aliwahimiza wanawake hasa wa maeneo ya pembezoni kutumia fursa ya huduma za bure zinazotolewa kupitia kliniki tembezi ili kujikinga na saratani.
“Kwenda hospitali kufanya vipimo mara nyingi ni gharama kubwa, hivyo tunapaswa kutumia vizuri fursa hizi zinazotufuata mpaka tulipo,” amesema.