Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake jamii ya wafugaji walia kuachiwa zigo la malezi, kisa malisho

Muktasari:

  • Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakisababisha uhaba wa majani na kusababisha wanaume wengi wa jamii hiyo kuhamisha mifugo kusaka malisho na kuacha familia zao nyuma chini ya uangalizi wa wanawake.

Longido. Maisha ya kuhamahama ya wanaume wa jamii ya wafugaji kwa ajili ya kusaka malisho imeelezwa kuwa chanzo cha mateso kwa wanawake wengi wa jamii hiyo.

Mateso hayo yanatokana na kuachiwa mzigo wa ulezi wa familia, kujikimu kwa mahitaji muhimu ya chakula, malazi na mavazi bila msaada wa upande wa pili.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Desemba 18, 2023 na baadhi ya wanawake hao kwenye hafla fupi ya utiaji saini ya hati ya makubaliano kati ya vijiji 16 vya Wilaya ya Longido dhidi ya Kampuni ya 'soils for the Future Tanzania ltd' kuhusu utekelezaji wa mradi wa uzalishaji wa hewa ya kaboni kupitia uhifadhi wa nyanda za malisho.

Akizungumzia makubaliano hayo, Katibu wa Nyanda za Malisho Kijiji cha Lesing'eta, Maria Maningo amesema kuwa uhakika wa malisho katika vijiji vyao mbali na faida za kifedha lakini itasaidia pia wanawake kuishi na waume zao kwa uhakika na kuhudumia familia pamoja.

"Kipindi cha ukame majani hukauka na katika kusaka malisho, wanaume wanahamahama kwenda maeneo tofauti kama Wilaya ya Ngorongoro, Kilindi au hata mapori ya mikoa mingine hadi nchini Kenya na kuacha familia bila chochote na kuwa mzigo kwa wanawake walioachiwa," amesema Maria

Akizungumzia mradi huo, mratibu wake nchini Iddi Mfunda amesema kuwa makubaliano hayo yanalenga wananchi wa vijiji 16 kuchangamkia soko la kimataifa na kunufaika nalo kwa biashara ya hewa ya kaboni.

Amesema, mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka 40 ijayo, unalenga kusimamia na kuboresha nyanda za malisho ili kuondoa gesi chafuzi  kutoka angani hadi kwenye udongo.

"Makubaliano yanalenga kushirikiana na vijiji kufanya uhifadhi wa nyanda za malisho kwa ajili ya kunyonya hewa ya kaboni na kuuza kwenye masoko makubwa ya kimataifa na kurudisha faida kwa wananchi na Serikali kuu" amesema Mfunda.

Amesema kuwa wanatumia mfumo wa ubia kati ya kampuni, Serikali na wananchi (PPP) katika biashara hiyo ambayo watakuwa wanalipa kiasi cha dola 2 (Sh5,000) kwa kila unit moja ya hewa ya kaboni katika vijiji kwa ajili ya shughuli mbali mbali za maendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Longido Marko Ng'umbi akishuhudia makubaliano hayo amesema kuwa biashara hiyo mpya na kubwa kwenye soko la dunia, imekuwa na manufaa kwa watu waliowahi kuchangamkia na kuwataka wananchi wake kutoa ushirikiano mkubwa kwa kampuni hiyo kwa ajili ya utekelezaji.

Amesema kuwa Wilaya ya Longido ni moja ya waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi yaliyoikumba dunia hivi karibuni na kusababisha kukosa mvua kwa miaka mitatu mfululizo.