Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake wahamasishwa ushiriki utunzaji mazingira

Muktasari:

  • Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 33.3 pekee ya wanawake ndio wanashiriki katika kamati za utunzaji mazingira nchini.

Dar es Salaam. Taasisi ya The Climate Hub imesema ushiriki wa wanawake na vijana katika usimamizi wa mazingira unakabiliwa na changamoto kubwa, huku ikisema hali hiyo inaweza kuchelewesha juhudi za kufikia malengo.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 33.3 pekee ya wanawake ndio wanashiriki katika kamati za mazingira.

Hayo yamesemwa leo Julai Mosi, 2025 na Msimamizi wa Miradi kutoka The Climate Hub Tanzania, Aron Sanga wakati wa majadiliano ya wanawake na vijana kuhusu ushiriki wao kwenye utunzaji wa mazingira, yaliyofanyika Julai Mosi, 2025 katika makao makuu ya taasisi hiyo yaliyopo Goba, jijini Dar es Salaam.

"Vijana ni nguvu kazi ya Taifa na wanatakiwa kushirikishwa moja kwa moja katika kamati za mazingira. Hata hivyo, kamati nyingi zimekuwa na ubaguzi ambao unawakandamiza wanawake na vijana kwa sababu ya kukosa imani nao," amesema Sanga.

Sanga ameongeza kuwa, moja ya changamoto kubwa inayokwamisha wanawake kushiriki kikamilifu ni upungufu wa elimu ya mazingira.

Mkurugenzi wa The Climate Hub Tanzania Laurel Kivuyo, akizungumza na wanawake na vijana wakati wa majadiliano ya changamoto zilizopo kuhusu uhusishwaji wa wanawake na vijana katika kamati za maendeleo na usimamizi wa mazingira yaliyofanyika leo Julai 1, 2025 kwenye makao makuu ya ofisi zao zilizopo Goba jijini Dar es Salaam.

Ofisa Mazingira kutoka Wilaya ya Kinondoni, Mustapha Hamisi amesema kuwa wanawake wengi hawana ujasiri wa kushiriki katika kamati za utunzaji wa mazingira kwa sababu ya mtazamo hasi wa jamii, kutojiamini na umaskini

 Hamisi ameongeza kuwa, ili kuondokana na changamoto hizo, ni muhimu kutoa elimu na mafunzo ya kutosha kwa wanawake, pamoja na kutunga sera ambazo zitawawezesha kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.

Ofisa Mazingira kutoka Wilaya ya Kisarawe, Godfrey Ambele amesema changamoto kubwa inajitokeza hasa katika maeneo ya vijijini, ambapo mfumo dume bado unachangia kwa kiasi kikubwa kutoshirikisha wanawake katika kamati za maendeleo na usimamizi wa mazingira.

“Katika maeneo mengi ya vijijini, wanawake wanakosa nafasi za uongozi kutokana na mifumo ya kijamii inayowabagua. Hata hivyo, ni muhimu kwa wanawake kujitokeza na kuchukua nafasi yao katika utunzaji wa mazingira,” amesema Ambele.

Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo, Mary Sang’wa, ameeleza kuwa ufuatiliaji wa mikakati ya utunzaji wa mazingira umekuwa mdogo, licha ya kuwa na mipango mizuri ya kutunza mazingira, utekelezaji wake unakosa ufanisi kwa sababu ya ukosefu wa usimamizi madhubuti.

Viongozi hao wametoa wito kwa wanawake, vijana na jamii kwa ujumla kuungana na kushiriki katika utunzaji wa mazingira.