Wanawake wapewa mbinu za kutoboa kiuchumi
Baadhi watoa mada wakiwa katika hafla ya asubuhi iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani wakiwa wanacheza na kupiga picha.
Dar es Salaam. Wanawake wafanyabiashara na wafanyakazi wamepewa mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kufikia uhuru wa kifedha, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kuwapa utulivu wa akili na uwezo wa kupanga maisha yao kwa ufanisi zaidi.
Imeelezwa kuwa ili mwanamke anayeanzisha au kuendesha biashara afanikiwe katika shughuli zake za kifedha, anapaswa kuwa na malengo yaliyo wazi pamoja na mpango wa bajeti unaoeleweka, ili kudhibiti matumizi na kuongeza tija katika biashara.
Rai hiyo imetolewa leo Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ushirikiano na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja wa Mafunzo na Usimamizi wa CRDB Bank Foundation, Joshua Mwakalobo amesema wanawake wanaomiliki biashara wanaweza kufikia mafanikio makubwa iwapo watasimamia vyema maeneo muhimu ya uendeshaji wa biashara zao.
Baadhi ya wanawake walioshiriki mkutano wa asubuhi ulioandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Mwakalobo ameeleza kuwa kuna maeneo matatu muhimu ambayo wanawake wafanyabiashara wanapaswa kuyazingatia, ili kupata matokeo chanya na kuongeza faida katika shughuli zao.
Amesema eneo la kwanza ni kuwa na mpango mkakati wa biashara unaoeleweka, utakaowawezesha kujua malengo ya biashara zao, hatua zinazopaswa kuchukuliwa pamoja na muda sahihi wa kuzitekeleza.
“Hakikisha una mpango mkakati wa biashara yako, huo utakusaidia kujua nini kinapaswa kufanyika kwa wakati gani na jambo la pili hakikisha kama mwanamke mfanyabiashara unao uwezo wa kutofautisha kati ya faida na gharama za uendeshaji wa biashara yako,” amesema.
Amesema hilo liende sambamba na msingi namba tatu wa mmiliki kuwa na uwezo wa kutathmini mwenendo wa biashara yake, kwani kuna wakati ambao biashara inakuwa juu au chini.
“Kuna biashara nyingine hujui inakwenda wapi, hujui inatoka wapi na nini unapaswa ufanye, hivyo ni muhimu kusimamia hili,” amesema.
Maneno yake yaliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Juin Construction LTD, Anna Mafoka ambaye aliwataka wanawake wafanyabiashara na Wajasiriamali kuwa na nidhamu ya fedha ili waweze kuona mafanikio wanayoyatamani.
“Ni muhimu kujua namna ya kutenganisha pesa ya biashara na pesa yako binafsi kama mwanamke unapokuwa katika biashara yako, hiyo ndiyo silaha itakayokupa maendeleo unayoyatamani,” amesema.
Anna ambaye anamiliki kampuni ya ujenzi, amesema ili kuhakikisha wanawake wanapata mafanikio zaidi amekuwa akiwashika mkono na kuwatengenezea fursa.
Baadhi ya wanawake walioshiriki mkutano wa asubuhi ulioandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
“Tumewekeza zaidi kwenye kuajiri wanawake na wanaume vijana kwa kuwasaidia katika kufanya internship (mafunzo kwa vitendo) na kutoa mikopo midogomidogo ili waweze kujisimamia na kujitegemea na kuweza kuwasaidia wanawake wengine,” amesema.
Katika hilo, Mtoa elimu ya fedha aliyethibitishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Neema Chammy amesema kuwa na mipango na kulipa bili kwa wakati ni moja ya njia inayoweza kulinda afya ya akili ya mwanamke.
Amesema wanawake wanabeba majukumu mengi kuliko wanavyoweza kuyasimamia na ili kufanikisha hilo, ni lazima wajenge utaratibu wa kulipa bili zao kwa wakati na kuepuka kuchanganya fedha binafsi na za biashara.
“Angalia huwa mnajiandaa vipi? Kuwa msimamizi thabiti wa maisha yako kwa kujua matumizi na akiba kwa mwezi husika. Hakikisha kila mwezi unakuwa na kiwango cha fedha unachoweka kama akiba, fedha ya dharula, fedha ya starehe na fedha kwa ajili ya jamii.
“Hii itakusaidia sana, itakusaidia kuepuka kuchanga kila kadi unayopewa,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori alitumia jukwaa hilo kuwahimiza wanawake kufuata malengo yao huku wakihakikisha kunakuwa na uwezo wa kusimamia kazi zao za kitaaluma sambamba na majukumu ya kifamilia.
“Usichague kati ya kazi na familia. Kuwa na ndoto zako na taaluma yako huku ukibeba familia yako pamoja nawe,” amesema.
Amesema hilo liendane na kujua namna ya kutengeneza kipato binafsi huku akiwahimiza wanawake kujifunza tabia ya kuweka akiba kidogokidogo, hata kwa kutumia kipato kidogo wanachokipata.
“Anza na kiasi kidogo ulicho nacho, hifadhi mara kwa mara na utagundua tofauti kadri muda unavyopita,” amesema.
Nini Benki inafanya
Katika kuendelea kuwajenga kiuchumi wanawake, Mkuu wa kitengo cha fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema benki hiyo imechagua kutatua changamoto za kinamama kupitia dirisha lao la biashara linalosimamia uwekezaji ili kuhakikisha wanashiriki vyema katika ujenzi wa uchumi.
Amesema kupitia dirisha hilo wamewafundisha wanawake namna ya kuendesha biashara kupitia programu, kwani hapo awali ushiriki wao ulikiwa wa kiwango kidogo.
“Hadi sasa tumetoa zaidi ya Sh560 bilioni chini ya dirisha hili kwa kinamama zaidi ya 100,000 tunajivunia kuwa matokeo yake ni makubwa,” amesema na kuongeza kuwa hilo limewezesha wanawake kudumisha na kuongeza ustawi wa jamii hasa kwenye familia zao,” amesema.
Amesema hadi sasa zaidi ya kinamama na vijana 500,000 wamewezeshwa na hilo lisingewezekana kwani kwa utaratibu wa kawaida ingehitajika kuleta dhamana au biashara ambayo imeshaanza ambapo kinamama wengi wasingeshiriki kujenga uchumi.
“Kwa CRDB tunaamini bado kuna kinamama wengi hawajaweza kujumuishwa kwenye uchumi na huduma jumuishi za kifedha, ndiyo maana mwaka 2023 ilianzishwa CRDB Foundation ambapo kupitia hiyo wamekuwa wakiwezesha vijana na kinamama,” amesema.
Baadhi ya wanawake walioshiriki mkutano wa asubuhi ulioandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Uongozi na wanawake
Mbali na kuwa na uhuru wa kiuchumi, Profesa Mori amesema upo umuhimu wa kukuza uongozi miongoni mwa wanawake huku akibainisha kuwa uongozi hauishii tu kwa wale wenye nafasi rasmi.
“Ninaamini kuwa kiongozi hahitaji kushikilia nafasi rasmi. Unaweza kuongoza kutoka pale ulipo. Sote tulio hapa ni viongozi, ndiyo maana ni muhimu kuandaa viongozi wanawake,” amesema.
Profesa Mori alieleza kuwa shauku yake ya kukuza uongozi ilisababisha kufanya utafiti kuhusu programu mbalimbali za uongozi zinazotolewa sehemu nyingine za dunia.
Kupitia mchakato huo, aligundua haja ya kutengeneza mpango wa aina hiyo unaolenga kujenga uwezo wa wanawake viongozi.
Amesema wazo hilo baadaye liliendelea na kuwa programu ya Women Leading Change, baada ya kupata msaada kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho anafanya kazi na kutengeneza ushirikiano na Sasamani Foundation.
“Tulianza kuota ndoto za programu hii mwaka 2016 na baadaye tukaanzisha kile tunachokiita leo Women Leading Change,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Mori, programu hiyo ilianza rasmi mwaka 2019 na inalenga wanawake viongozi wanaochipukia katika ukanda wa Afrika ya Mashariki ambao wanatamani kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao na katika nchi zao.
Alibainisha kuwa mpango huo tayari umefundisha makundi kadhaa ya washiriki na hadi sasa umezalisha wahitimu 129 kupitia makundi matano.
“Tunaamini kwamba unapowekeza kwa mwanamke, hujawekeza tu kwake yeye, bali pia katika jamii anayohudumia,” amesema.
Profesa Mori aliongeza kuwa programu hiyo ni moja ya njia anazochangia katika kuwawezesha wengine na kusaidia kukuza uongozi miongoni mwa wanawake katika eneo hilo.
Amesema hilo linafanyija kwa sababu ni vyema kutengeneza mifumo ya msaada inayowahamasisha wanaume na wanawake kushiriki kwa usawa katika nafasi za uongozi na fursa za kitaaluma.
Profesa Mori amesema kwa kutambua hilo Benki ya CRDB imekuwa ikihamasisha ushiriki sawa katika nafasi za uongozi na fursa za maendeleo ya kazi.
“Tunaweka mkazo kuhakikisha kuwa kila mtu anashirikishwa kila mahali. Ikiwa kuna nafasi zinapatikana, tunahimiza wanaume na wanawake wote kuomba. Ikiwa kuna fursa, tunahakikisha zinafikika kwa wote,” amesema.
Amesema ili kufanikisha hilo, CRDB imeanzisha miradi kadhaa inayolenga kusaidia wanawake nje ya kazi.
Hii ni pamoja na programu za upatikanaji wa fedha kwa wanawake wajasiriamali, miradi ya ustawi wa jamii na programu za uwezeshaji wa jamii zinazotekelezwa kupitia CRBD Foundation.
Profesa Mori amesema kuwa miradi hii ni sehemu ya dhamira pana ya taasisi hiyo ya kuongeza fursa kwa wanawake na kuimarisha ushiriki wao kiuchumi.